8 Aug 2013


Kwa nini Rais anyamazie siri hizi kuhusu dawa za kulevya?

Evarist Chahali
Uskochi
Toleo la 310
7 Aug 2013

WIKI iliyopita, Rais Jakaya Kikwete aliendeleza utaratibu wake wa kulihutubia taifa takriban kila mwisho wa mwezi. Japo wakati mwingine hotuba zake huonekana kama maelezo tu ya masuala ambayo tayari wananchi wanayafahamu au pengine maelezo tu ambayo hayana majibu kwa maswali yanayowasumbua wananchi, ukweli kuwa Rais anathamini kuzungumza na taifa mara kwa mara ni jambo linalostahili pongezi.
Hata hivyo, nilishangazwa kuona amekwepa kuzungumzia kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya. Ni vigumu kukimbilia kumlaumu moja kwa moja pasipo kuelewa taratibu za maandalizi ya hotuba zake.
Kama ambavyo Mwalimu Julius Nyerere alivyowahi kutufunza, urais ni mzigo mzito, kuna nyakati kiongozi mkuu wa nchi hubebeshwa lawama kutokana na makosa au uzembe wa wasaidizi wake.
Kwa uelewa wangu, hotuba za Rais huandaliwa na wasaidizi wake japo kwa kiasi kikubwa maandalizi hayo hutegemea mtazamo binafsi wa Rais kuhusu atakayoyazungumza kwenye hotuba husika.
Sasa, je kukosekana kwa kipengele cha dawa za kulevya katika hotuba iliyopita ya Rais Kikwete ni matokeo ya wasaidizi wake kutokiweka kipengele hicho au Rais mwenyewe hakuona umuhimu wa kuzungumzia suala hilo? Ikulu pekee ndio yenye majibu.
Iwe ni uamuzi binafsi wa Rais au wa wasaidizi wake, hotuba hiyo kutozungumzia tatizo la dawa za kulevya imejenga picha kuwa aidha watawala wetu hawadhani kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo hilo, au pengine wanaelewa uwepo wa tatizo hilo lakini hawadhani ni kubwa kiasi cha kupaswa kuwamo katika hotuba ya Rais.
Lakini yawezekana pia kuwa uamuzi wa Rais Kikwete kutozungumzia suala hilo ni kutokana na ‘nafsi yake kumsuta’. Itakumbukwa takriban miaka saba iliyopita (Septemba 18, 2006), alikabidhiwa orodha ndefu yenye majina 58 yenye majina ya vigogo wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Orodha hiyo ilijumuisha majina ya wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa dini, sambamba na mbinu wanazotumia kufanikisha biashara hiyo haramu.
Kwa mujibu wa maelezo husika, kundi la kwanza lilikuwa na  majina 12, miongoni mwao ni wafanyabiashara maarufu Dar es Salaam, Morogoro, Zanzibar, Arusha na Bagamoyo na baadhi ya viongozi wa dini.
Katika kundi la pili kulikuwa na watu 19, miongoni mwao wamo wanasiasa wakubwa, wamo kutoka taasisi ya fedha na wafanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam na Zanzibar.
Kundi la tatu lilikuwa na majina 27 ya watu ambao si wenye majina makubwa lakini ndio waliokuwa wakitumika kusambaza mitaani dawa hizo za kulevya.
Mbali ya kushiriki katika kusambaza dawa za kulevya, baadhi ya waliotajwa katika kundi hili walidaiwa kushiriki katika kuingiza silaha nzito, zinazotumika kwa ajili ya ujambazi kutoka nchi jirani.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere ulitajwa kutumika kuingiza dawa hizo kutoka nje ya nchi, huku baadhi ya maofisa wa polisi wakitajwa kutoa ulinzi kwa wanaopitisha dawa hizo.
Nyumba ya ofisa wa juu mstaafu katika idara nyeti iliyopo Dar es Salaam ilitajwa kutumika kuhifadhi vijana wanaoingiza dawa za kulevya nchini, huku nyumba ya mfanyabiashara mmoja iliyopo Mikocheni Dar es Salaam ikitajwa kutumika kama kituo cha kutolea pipi tumboni kwa vijana wanaotumika kuingiza dawa hizo kutoka nje ya nchi.
Kitendo hicho cha kijasiri kilitokea chini ya mwaka mmoja tangu Rais Kikwete aingie madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahusika.
Mwishoni mwa wiki, gazeti moja liliandika kwa kirefu kuhusu kushamiri kwa biashara hiyo haramu, na kwa kiasi kikubwa, liliakisi kilichokuwa kinatokea mwaka 2006 wakati wananchi hao wazalendo walimpomwandikia barua Rais Kikwete.
Hivi karibuni nilizungumza na ‘mwandamizi’ mmoja katika taasisi fulani nyeti kuhusu kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya akanieleza; “mtandao wa biashara dawa za kulevya hapa nchini ni mkubwa mno kiasi kwamba kupambana nao ni mithili ya kufanya mapinduzi.
Alikwenda mbali zaidi na kunitajia majina ya baadhi ya wahusika wakuu wa biashara hiyo, na wasifu wao ulionyesha kuguswa kwa takriban kila nyanja ya jamii yetu; kuanzia watoto wa vigogo mbalimbali, wanasiasa na wafanyabiashara maarufu hadi baadhi ya viongozi, wafadhili wa soka na wasanii mbalimbali wa muziki au filamu (japo alisema wasanii hao wenye majina makubwa ni kama associates (washirika) tu katika biashara hiyo, huku umaarufu wao ukitumiwa ipasavyo na wahusika wakuu).
Alinitahadharisha kuwa miongoni mwa wahusika ni watu hatari, hawasiti kumdhuru yeyote anayeonekana kikwazo katika biashara hiyo. Kadhalika, alinifahamisha mbinu zinazotumika kufanikisha biashara hiyo ni za kisasa mno mithili ya kundi maarufu la kihalifu la Mafia la nchini Italia.
Mwandamizi huyo ambaye kitaaluma ni mchambuzi wa intelijensia (intelligence analyst) katika taasisi moja nyeti serikalini alinieleza kuna kila dalili Uchaguzi Mkuu ujao 2015 utahusisha matumizi makubwa ya fedha zinazotokana na biashara ya dawa za kulevya, na akabashiri biashara hiyo kuendelea kushamiri kadri uchaguzi huo unavyokaribia.
Kuhusu kuongezeka kwa idadi ya Watanzania wanaokamatwa nchi za nje wakisafirisha dawa hizo, mzalendo huyo alisema soko la ndani la dawa za kulevya ni kama limeelemewa, huku uwezo wa wanunuzi (watumiaji) ukizidi kushuka, na njia muhimu ya kupata faida ya kutosha kwa sasa ni kutegemea soko la nje.
Pia alitaja kitu cha kuogofya alichokiita (kwa utani) ‘recruitment drive’, alieleza baadhi ya ‘wauza unga’ wanatoa bure kiasi cha dawa kwa watoto mitaani hususan wanafunzi, kwa matarajio kuwa ‘watanogewa’ (dawa hizo ni addictive mno), na hivyo kuongeza idadi ya wateja wao.
Swali, je Rais Kikwete hafahamu kuhusu suala hili kiasi kwamba hakuona umuhimu wa kulizungumzia katika hotuba yake ya hivi karibuni? Ni majuzi tu, Watanzania wawili walikamatwa Afrika Kusini wakiwa na ‘shehena ya kihistoria’ ya dawa za kulevya, na tungetegemea angalau watawala wetu waonyeshe kuguswa na kushamiri kwa biashara hiyo haramu.
Hadi sasa ni kiongozi mmoja tu wa kisiasa, Waziri Mkuu wa zamani Edward Sumaye, ambaye angalau ametahadharisha uwezekano wa ‘muuza unga’ (mfanyabiashara ya dawa za kulevya) kuingia Ikulu. Unaweza kujiuliza kwa nini wanasiasa wanaotajwa kuwania urais ‘kwa udi na uvumba’ wapo kimya kuhusu suala hili? Jibu ni kwamba “hawawezi kukata tawi wanalokalia.”
Tumelea ufisadi hadi kufikia hatua ya mafisadi kuwa tabaka la kawaida katika jamii yetu. Tunakoelekea, biashara ya dawa za kulevya inaweza pia kufikia hatua hiyo; kuonekana kama chanzo halali cha mapato kwa watu binafsi na taifa kwa ujumla.
Tatizo ni kwamba ‘unga’ ni kitu hatari sana. Tunazalisha taifa la mataahira, ambao wakikosa ‘fix’ (dozi ya dawa hizo) wapo tayari hata kuchinja wazazi wao ili wapate fedha za kununulia ‘unga.’
Inaelezwa kuwa japo biashara ya dawa za kulevya ilikuwepo kabla ya zama hizi za ufisadi, ukweli mchungu ni kuwa ufisadi umewezesha kwa kiasi kikubwa biashara hiyo haramu kuwa kama halali.
Huu ni wito wangu kwa Rais Kikwete: ‘unga’ au ‘sembe’ (yaani dawa za kulevya) unaangamiza taifa letu. Wahusika wanafahamika lakini hawachukuliwi hatua. Rais asipolifanya tatizo hili kuwa janga la kitaifa litamgharimu.
Muuza ‘unga’ hana tofauti na gaidi au mtu anayeambukiza Ukimwi kwa makusudi, wote wauaji. Tukiwaruhusu wanaharamu hawa waendelee na biashara hiyo kana kwamba ni chanzo halali cha kipato, hatima ya taifa itakuwa shakani.
SAY NO TO DRUGS

- See more at: http://raiamwema.co.tz/kwa-nini-rais-anyamazie-siri-hizi-kuhusu-dawa-za-kulevya#sthash.lakQ6Qzv.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.