26 Sept 2013

NIANZE makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi na pole kwa ndugu zetu wa Kenya kutokana na shambulio la kigaidi lililotokea mwishoni mwa wiki jijini Nairobi. Kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab kimekiri hadharani kuwa ndicho kilichofanywa shambulio hilo la kinyama.
Hadi wakati ninaandika makala hii, idadi ya waliouwa katika shambulio hilo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 60, wengi wakiwa Wakenya na baadhi raia wa nchi nyingine kama Uingereza, Marekani na Ghana.
Wakati tunaungana na wenzetu wa Kenya katika kipindi hiki kigumu, ni vema kuliangalia kwa undani tishio la ugaidi duniani, na hususan huko nyumbani ambapo siku za hivi karibuni neno ‘ugaidi’ limeanza kutumika kama mtaji wa kisiasa.
Pengine kabla ya kwenda mbele pengine ni muhimu kufahamu ugaidi ni nini. Kuna kutoatifikiana kuhusu maana halisi ya ugaidi, hasa linapokuja suala la mtizamo kati ya wahusika na wahanga. Mfano mwepesi ni hali ilivyokuwa katika zama za mfumo wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini. Kwa makaburu, wanaharakati kama Nelson Mandela waliitwa magaidi, japo sote tunafahamu kuwa walikuwa wapigania uhuru.
Lakini tukiweka kando kutokuafikiana huko, kimsingi ugaidi ni matumizi ya nguvu au vitisho kwa minajili ya kushinikiza serikali au taasisi za serikali za kimataifa (kwa mfano Umoja wa Mataifa) au umma au sehemu ya jamii ili kufikia malengo ya kisiasa, kidini, kiitikadi au asili ya mtu (racial causes).
Pasi kuingia ndani kwenye mjadala kuhusu maana ya ugaidi, ukweli unabaki kuwa ugaidi ni tishio kubwa kwa usalama. Na kama ilivyo vigumu kupata maana sahihi ya ugaidi, ndivyo ambavyo ilivyo kwa kubaini  vyanzo na ufumbuzi wa ugaidi.
Kuna msemo mmoja kuwa “wakati gaidi anahitaji japo sekunde moja tu kutimiza unyama wake, taasisi za dola zinahitaji kila sekunde kumzuia gaidi asifanikiwe kutimiza malengo yake.” Kwa lugha nyingine, kupambana na ugaidi kunahitaji vyombo vya dola kuwa macho muda wote. Taasisi za dola zinahitaji kuzuwia kila fursa ya kutokea kwa ugaidi, ilhali gaidi anahitaji fursa moja kutimiza malengo yake.
Sote tunatambua kuwa si jambo jema kutumia majanga ili kupata fursa ya kunyoosheana vidole. Hata hivyo, wakati mwingine majanga hutupa fursa nzuri ya kuchukua tahadhari stahili ili, aidha yasitokee tena, au kama yametokea kwa wenzetu, kuyazuia yasitokee kwetu.
Huu ni ukweli usiopendeza lakini hauepukiki: kilichotokea nchini Kenya kimekwishawahi kutokea huko nyuma (katika shambulizi la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, Agosti 2008), kinaendelea kutokea japo si kwa kiwango cha kutisha kama ilivyotokea kwa jirani zetu (hapa narejea mashambulizi ya kutumia tindikali na risasi dhidi ya Mapadre huko Zanzibar na  shambulizi la bomu kanisani huko Arusha), na-japo naomba Mungu aepushie - kitaendelea kutokea hasa kwa vile tuliowakabidhi jukumu la kupambana na ugaidi ni kama wameshindwa kazi.
Nimekuwa nikitahadharisha mara kadhaa huko nyuma kuhusu uwezekano wa kurejewa kwa matukio mengine ya ugaidi, na kwa bahati mbaya hali imekuwa hivyo. Lakini kwa makusudi, hadi sasa hakuna japo mtu mmoja aliyewahi kuwajibishwa kwa kuzembea au kutotimiza majukumu ipasavyo kuzuwia matukio hayo ya kigaidi.
Ugaidi una tabia ‘mbaya’ kama majipu. Jipu likitokea sehemu flani kisha lisipotibiwa ipasavyo, laweza kujitokeza sehemu nyingine ya mwili. Kwa ugaidi ni hivyo hivyo, na tumeshuhudia yaliyojiri Zanzibar dhidi ya Kanisa Katoliki yakirejea tena huko Arusha.
Ninatamani nisingeandika haya, lakini kilichotokea Kenya kinaweza kuhamasisha ‘magaidi halisi’ tulionao, ambao wamekuwa ‘huru’ kufanya watakavyo (japo si kwa kiwango kikubwa kama Kenya) kunakili tukio hilo la kinyama na kulitenda huko nyumbani.
Natambua kuna watakaoniona kama ‘nabii wa kiama’ (prophet of doom) lakini kuuchukia ukweli hakuufanyi uwe uongo. Udhaifu wa taasisi zetu za usalama, sambamba na uzembe wa watawala wetu kupambana na kukua kwa tishio la ugaidi huko nyumbani kunaweza kuzua majanga makubwa zaidi huko mbeleni.
Kama ‘maana ya jumla’ (general definition) ya ugaidi ilivyoeleza hapo juu, kwa kiasi kikubwa ugaidi hulenga kupambana na serikali kwa namna ya kuifarakanisha na wananchi. Hapa nina maana kuwa pindi magaidi wakifanya shambulio, moja ya matarajio yao ni wananchi kuitupia lawama serikali na taasisi zake, hususan vyombo vya dola, aidha kwa kushindwa kuzuia shambulio husika au kwa kukaidi kusikia matakwa ya magaidi hao.
Mfano mzuri ni katika tukio hili la majuzi la ugaidi nchini Kenya. Kwa mujibu wa kikundi cha Al-Shabaab, ‘ugomvi’ wao na serikali ya Kenya ni kuhusu uwepo wa majeshi ya nchi hiyo huko Somalia. Kikundi hicho cha magaidi kinataka Kenya iondoe majeshi yake Somalia. Sasa magaidi hao wanadhani kuwa shambulio hili la majuzi linaweza kusababisha baadhi ya Wakenya kuhoji umuhimu wa majeshi yao kuwepo huko.
Lakini kwa kiasi kikubwa, Al-Shabaab hawajafanikiwa katika azma yao hiyo ya kidhalimu. Shambulio hilo la kigaidi limewaunganisha mno Wakenya kuliko kuwatenganisha, na kuna uwezekano mkubwa wananchi wataelewa kwa nini ni muhimu kwa majeshi yao kuwadhibiti Al-Shabaab huko Somalia badala ya kudai majeshi hayo yaondoke huko.
Sasa tukiangalia hali ilivyo huko nyumbani (Tanzania) vyombo vya dola kama Idara ya Usalama wa Taifa ni kama vile imeshindwa kupambana na ugaidi huko Zanzibar na Arusha, sambamba na uharamia wa biashara ya dawa za kulevya, utoroshwaji wa rasilimali zetu, na ufisadi kwa ujumla, kwa nini basi tusihofie kuwa taasisi hiyo inaweza kuwa na wakati mgumu kuzuia uwezekano wa ugaidi mkubwa kama uliotokea huko Kenya?
Ninatambua kuna watakaotafsiri tofauti ukweli huu mchungu na kuniona kama ‘nabii wa kiama’ (prophet of doom), lakini ninachoweza kuwaeleza ni kuwa kuuchukia ukweli hakuufanyi uwe uongo. Na ukweli ninaobainisha hapa ni udhaifu wa taasisi zetu za dola kupambana na uhalifu ‘wa wastani’ ulio ndani ya uwezo wao wa kuudhibiti. Sasa kama wanashindwa kudhibiti vilivyo ndani ya uwezo wao watawezaje kudhibiti majanga ya ugaidi mkubwa ambao kimsingi ni kama upo nje ya uwezo wa kawaida wa taasisi zozote zile za dola?
Badala ya kupambana na maharamia wanaojaribu kuufanya ugaidi uwe jambo la kawaida kama ufisadi (kwa mfano mashambulizi ya tindikali), taasisi zetu za dola zipo ‘bize’ na porojo za akina Mwigulu Nchemba kuutumia ugaidi kama turufu ya kisiasa dhidi ya wapinzani wao, hususan CHADEMA. Tumeshuhudia kesi zenye shaka dhidi ya akina Lwakatare na Kileo wa CHADEMA ilhali mashambulizi ya tindikali yakiendelea kutokea pasi kudhibitiwa.
Adui mkubwa dhidi ya ufanisi wa taasisi zetu za dola ni kutanguliza mbele maslahi ya itikadi za kisiasa (kukitumikia chama tawala) badala ya maslahi ya taifa. Mashushushu wetu wapo ‘bize’ kuwadhibiti wapinzani badala ya magaidi wanaochipukia ambao wakiachwa waendelee na unyama wao wanaweza kutuletea balaa kama hilo la Kenya.
Mwisho, wakati tunaendelea kuwafariji ndugu zetu wa Kenya kwa janga lililowakumba, ningependa kutoa wito kwa serikali na taasisi za dola kutambua kuwa mapungufu yao katika kupambana na matukio ya ugaidi ‘ wa wastani’ huko nyumbani yanaweza kuhamasisha magaidi wa ndani na/au nje kutumia fursa hiyo kufanya mashambulizi makubwa ya kigaidi.
Pamoja na kumwomba Mungu aepushie, na licha ya kutamani nisingeandika maneno haya, ‘hisia yangu ya sita (6th sense) inanipa hofu kuwa pasipo jitihada za makusudi, muda si mrefu tutashuhudia janga kama hilo lililotokea nchini Kenya. Kwa tunaofahamu uimara na ujasiri wa taasisi za usalama nchini Kenya, sambamba na uelewa kuwa magaidi kama wa Al-Shabaab walikuwa wanaiwinda nchi hiyo, lakini bado ikashindikana kuzuia janga hili la majuzi, jambo pekee linaloweza kutuepusha na janga hilo ni kudra za Mwenyezi Mungu (kwa sababu kelele zetu za kuwataka watawala wetu ‘waamke’ na kuakabiliana na ugaidi zimegonga mwamba). Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/magaidi-wanahitaji-sekunde-dola-inahitaji-kila-sekunde#sthash.QaGTY6nR.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.