5 Dec 2014


NIANZE kwa kuelezea kuhusu hatua mbili zilizochukuliwa na mamlaka za hapa Uingereza na jinsi zilivyobadili maisha kwa wakazi wengi wa nchi hii.
Lengo la kuelezea hatua hizo ni kuhusisha na tatizo kubwa linalokwaza utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali huko nyumbani: ukosefu wa dhamira.
Hatua ya kwanza ilihusu dhamira ya serikali kuhamasisha wavuta sigara kuachana na tabia hiyo ambayo si tu ina gharama kifedha bali pia kiafya.
Kwa hapa Scotland, mwaka 2006 serikali ilipiga marufuku uvutaji sigara hadharani. Hatua hiyo, sambamba na mikakati mbalimbali ya kuwasaidia watu wanaotaka kuacha uvutaji wa sigara, imekuwa na mafanikio makubwa.
Mwaka jana, serikali ilitangaza sheria ya kuyataka maduka makubwa (supermarkets) yote kutuonyesha sigara katika maeneo yaliyotengwa kwa uuzaji wa bidhaa hiyo. Sambamba na hatua hiyo ni kutuonyesha bei za pakti za sigara hadharani.
Sheria hiyo itaanza kutekelezwa na maduka yote kuanzia Aprili mwakani. Hatua zote hizo ni utekelezaji wa mkakati wenye lengo la kuifanya Scotland kuwa ‘smoke-free’ kufikia mwaka 2034.
Hatua nyingine ya hivi karibuni ni ile ilivyoanza kutekelezwa Oktoba mwaka huu, ambapo kila biashara ya bidhaa imeagizwa kutoza ushuru wa pence 5 (takriban shilingi 136) kwa kila mteja atakayetaka mfuko wa kubebea bidhaa alizonunua.
Lengo la hatua hii ni kuhamasisha utumiaji tena wa mifuko iliyokwishatumika (re-use) na kupunguza takataka. Hatua hii imekuwa na mafanikio makubwa mno, kwani wateja wengi sasa wanakwenda madukani wakiwa na mifuko yao wenyewe ili kuepuka ushuru huo.
Kama nilivyotanabahisha mwanzoni, lengo la kuelezea kuhusu hatua hizo mbili ni kuzihusisha na tatizo linaloikabili nchi yetu la kukosa dhamira katika hatua mbalimbali tunazozichukua kwa manufaa ya jamii au Taifa kwa ujumla.
Wiki iliyopita tumeshuhudia sokomoko kubwa kuhusiana na skandali ya ‘Tegeta Escrow.’ Kwa kifupi, skandali hii ilihusu uchotwaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, katika mazingira yanayoashiria ufisadi.
Kamati husika ya Bunge chini ya uongozi wa Mbunge Zitto Kabwe ilifanya kazi kubwa ya kufuatilia suala hilo, na hatimaye kuwasilisha ripoti iliyotokana na uchunguzi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na Taasisi ya Kupambana na Kuzuwia Rushwa (Takukuru).
Tarehe 26 ya mwezi uliopita yaweza kuingia katika historia ya taifa letu, ambapo kwa sisi tunaofuatilia masuala mbalimbali ya huko nyumbani kwa kutumia mitandao ya kijamii tulishuhudia kiu kubwa ya Watanzania kuhusu undani wa skandali hiyo ya Escrow hususan majina ya wahusika na hatua pendekezwa dhidi yao.
Kwa siku nne mfululizo, wengi wa Watanzania walionekana ‘kusahau takriban kila kitu’ ikiwa ni pamoja na ‘vipaumbele vyetu vya kawaida’ kama vile maendeleo ya ligi za soka barani Ulaya, na kuwekeza nguvu zao kufuatilia mjadala wa skandali hiyo huko Bungeni, Dodoma.
Hatimaye, Jumamosi iliyopita, ripoti hiyo iliridhiwa na wabunge wetu japokuwa wananchi wengi (angalau katika mitandao hiyo ya kijamii) wakibaki na kinyongo kidogo kutokana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ‘kuokolewa.’ Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa, wengi wa waliokuwa wakifuatilia tukio hilo walionekana kuridhishwa na maamuzi yanayotaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka na kuchukua hatua stahili dhidi ya wahusika.
Nisingependa kurejea yote yaliyojiri wakati wa mjadala huo mkali, lakini masuala muhimu yaliyojitokeza waziwazi ni pamoja na, kwanza, kuwapo baadhi ya wawakilishi wa wananchi ambao hawataki kabisa kusikia vilio vya wanaowawakilisha, na badala yake kutetea misimamo na maslahi yao binafsi.
Baadhi ya wabunge wa CCM, hususan wa kuteuliwa, walionekana kama ‘wametoka sayari nyingine’ kwa jinsi walivyosimama kidete kuwatetea watuhumiwa katika skandali hiyo.
Pili, na pengine hili ni la muhimu zaidi, ni jinsi tofauti za kiitikadi zilivyowekwa kando kwa kiasi kikubwa na wengi wa wabunge kuhakikisha kuwa maslahi ya umma na Taifa yanawekwa mbele, na hatimaye kufikiwa mwafaka wa ‘pande tatu,’ kwa maana ya CCM, Ukawa na Kamati husika ya Bunge. Tukio hili sio tu ni la kihistoria bali lina umuhimu wa kipekee.
Iwapo wanasiasa wetu wataendeleza ari hiyo ya kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya maslahi yao binafsi, au ya vyama vyao, basi kwa hakika twaweza kupiga hatua kubwa katika kukabili changamoto mbalimbali zinazoikabili Tanzania.
Hata hivyo, ukweli mchungu kuhusu hitimisho la suala hilo ni kwamba baadhi ya watuhumiwa ‘wameokolewa.’ Ikumbukwe kuwa taarifa zilizopatikana awali, na hatimaye kuwekwa hadharani na Mbunge Tundu Lissu ni uhusika wa IKulu, ambayo inaelezwa iliidhinisha malipo hayo kutoka katika akaunti ya Escrow huko Benki Kuu. Sambamba na hilo ni kauli za mara kwa mara za Waziri Mkuu Pinda kuwa fedha hizo si za umma.
Na kama kutonesha ‘kidonda kibichi,’ wakati anaahirisha kikao cha Bunge hilo, ambacho pamoja na mambo mengine, kilisomewa na kujadili ripoti kuhusu skandali hiyo ya Escrow, Pinda aligusia tena swali ambalo limeonekana kama ‘utetezi’ na ‘tuhuma’ kuhusu utoaji wa fedha hizo, yaani “je fedha hizo ni za umma?”
Watuhumiwa wanadai si za umma ilhali watuhumu, ikiwa pamoja na wananchi wengi, wanaamini kuwa fedha hizo ni za umma, na kitendo cha kuzitoa Benki Kuu ni cha kifisadi.
Na hapa ndipo maelezo niliyoyatoa hapo awali kuhusu hatua mbili zilizochukuliwa hapa Scotland yanapokuwa na umuhimu  kwa hali ya huko nyumbani. Kama kweli tungekuwa na dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, hakukuwa na haja ya ‘kuchuja’ wahusika. Je, kwanini hoja iliyotolewa na Mbunge Lissu kuhusu kuhusika kwa Ikulu ilitelekezwa?
Japo wakati anarejea nyumbani kutoka Marekani kwa matibabu, Rais alieleza kuwa “hafahamu kwa undani kuhusu kilichokuwa kikiendelea Dodoma (kwa maana ya mjadala huo wa skandali ya Escrow), ukweli ni kwamba taasisi ya urais si mtu aitwaye Jakaya Kikwete pekee bali wasaidizi na taasisi mbalimbali kama vile Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Idara ya Usalama wa Taifa, nk.
Licha ya ukweli kwamba Rais alikwenda Marekani kwa matibabu, sitaki kabisa kuamini kuwa alikuwa hafuatilii kinachoendelea kuhusu skandali ya Escrow. Kama aliweza kusoma ‘meseji’ mbalimbali alizotumiwa na Watanzania kumtakia afya njema, ninaamini alipata muda pia wa kufahamishwa kinachoendelea huko nyumbani kuhusu sakata la Escrow.
Mbunge Lissu pia aligusia kuhusu utendaji kazi mbovu wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa. Aliishutumu vikali huku akihoji ilikuwa wapi wakati ‘ufisadi wa Escrow’ ukitendeka.
Licha ya mchango wa mbunge huyo machachari kuhusu taasisi hiyo kutopewa uzito kabisa katika maazimio ya Bunge juu ya skandali ya Escrow, Kamati ya Zitto, kwa sababu ambazo si vigumu kwa sisi wengine kuzielewa, ilikwepa kuitwisha lawama Idara ya Usalama wa Taifa.
Licha ya kutoafikiana na hatua hiyo ya Kamati ya Zitto kutomgusa Rais Kikwete wala Idara ya Usalama wa Taifa, binafsi ninaamini kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kiufundi zaidi kwa maana kwamba ya kuepusha kuwaunganisha CCM, ambayo ndio iliyotoa wengi wa wajumbe wa Kamati hiyo, kuipinga ripoti nzima.
Kama ambavyo CCM imefanikiwa kumwokoa Pinda, laiti Kamati hiyo ingemtuhumu Rais Kikwete na Idara ya Usalama wa Taifa basi huenda isingemudu japo kufikia hatua ya kujadiliwa.
Sasa matokeo yake tumefanya kile Waingereza wanaita to settle for less yaani angalau tumepata chochote kitu. Lakini msemo huo wa Kiingereza unaonya kuwa ‘when you settle for less, you end up getting even lesser than what you deserved’ (unapokubali kupewa kitu pungufu ili mradi upate tu, waishia kupata pungufu zaidi ya unachostahili).
Pengine Rais Kikwete atatekeleza maazimio yote ya Bunge. Pengine utekelezaji huo utafanyika mapema iwezekanavyo. Lakini ukweli utabaki kuwa licha ya skandali ya Escrow kuwa moja tu ya skandali nyingine kadhaa ambazo bado zinaitesa Tanzania yetu, na nyinginezo zinazoweza kuibuka huko mbele, hatujafanikiwa kukata mzizi wa tatizo la ufisadi ambalo kwa kiasi kikubwa limegubika utawala wa Rais Kikwete. Na kama nilivyotanabaisha katika makala iliyopita, Rais wetu ni mgumu katika kuchukua hatua stahili, na matokeo yake twajikuta kila mara tukirejea kulekule tulikotoka. Tunapiga hatua 50 mbele, baadaye twarejeshwa hatua 100 nyuma.
Kinachosababisha haya ni kile ambacho wenzetu hapa Scotland wamefanikiwa: si tu kuwa na sera au mipango mizuri, bali pia kuitafsiri katika vitendo.
Japo ningetamani sana kuona skandali ya Escrow kuwa ya mwisho angalau hadi Rais Kikwete atakapomaliza muda wake, ukweli kwamba kuna mabilioni ya fedha tuliyoibiwa na kufichwa kwenye akaunti za Benki huko Uswisi, sambamba na ‘uhalifu uliozoeleka’ wa biashara haramu ya madawa ya kulevya na ujangili, sintoshangaa tukikumbana na ‘Escrow nyingine’ hivi karibuni.
Nihitimishe makala hii kwa kukumbushia mambo haya: wenye ufahamu wanaelewa ukaribu uliopo kati ya Rais Kikwete na Waziri Muhongo (inaelezwa kuwa ndiye aliyemshawishi kutoka kwenye taaluma na kuingia kwenye siasa kwa uteuzi) wanaona ni mtihani mkubwa mno kwa Rais Kikwete kumtimua waziri huyo ambaye siku zote amesimama kidete kuwaaminisha Watanzania kuwa fedha za Escrow si za umma.
Kwa upande mwingine, kumwajibisha Mwanasheria Mkuu Werema kutamaanisha ‘kumweka huru’ mtu mwenye uelewa mkubwa wa ‘mambo mengi’ yaliyotokea, yanayotokea na yatakayotokea katika utawala wa Rais Kikwete.
Katika mazingira ya kawaida tu, si rahisi mtu ‘kujitenga’ na ‘mwandani’ wake, hasa ikizingatiwa kuwa ‘hasira za kutimuliwa’ zaweza kumshawishi kuweka hadharani mengi ya tusiyoyajua (kwa mfano majina ya walioficha fedha zetu kwenye mabenki ya Uswisi.)
La mwisho kabisa ni Singasinga. Bila haja ya kudadisi nani aliyemleta wala kujua washiriki wake wa kibiashara nchini Tanzania, ni muhimu mapendekezo ya kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yake yakatekelezwa haraka pengine kabla ya hatua dhidi ya watendaji wa serikali waliohusishwa na skandali hiyo.
Ushauri wangu mwepesi ni kuwa huyo mtu atangazwe kuwa ‘persona non grata’ (mtu asiyetakiwa kuwapo katika nchi husika) mara moja.
Idara ya Usalama wa Taifa inafahamu bayana tishio la kiusalama linalosababishwa na kuwapo kwake, na huenda CCM pia yatambua madhara aliyosababisha mtu huyo kwa kilichokuwa chama tawala nchini Kenya, KANU. Atimuliwe.
Tanzania yetu ni kama nyumba zilizojengwa bonde la Jangwani (Dar), msimu wa kiangazi tupo salama, msimu wa mvua ukiwasili inakuwa tabu. Ikumbukwe kuwa hata Nabii Nuhu alijenga safina kabla gharika haijaanza. Tujipange kupambana na ‘Escrow nyingine’ sasa badala ya kusubiri hadi ziibuke.
INAWEZEKANA, TUKITIMIZA WAJIBU WETU IPASAVYO


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.