10 Sept 2015

ANGALIZO: Makala hii iliandikwa kwa ajili ya kuchapishwa katika toleo la wiki iliyopita lakini haikuchapishwa kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. 

HATIMAYE ‘wapinzani wakuu’ katika Uchaguzi Mkuu ujao, yaani chama tawala CCM na Ukawa wamefanikiwa kuzindua rasmi kampeni zao na kuwaeleza wapigakura nini watarajie kutoka kwa vyama hivyo.
Kabla ya kuingia kwa undani kuchambua uzinduzi wa kampeni za vyama hivyo pamoja na ilani zao, ningependa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba historia inaandikwa katika Uchaguzi Mkuu huu. Mie ni mpenzi wa teknolojia, na kubahatika kwangu kuwa huku kwa wenzetu ambao teknolojia sasa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, sio tu kumeniongezea mapenzi hayo bali kutamani isambae katika sehemu mbalimbali duniani.
Kwa mara ya kwanza kabisa, teknolojia imekuwa na mchango muhimu katika historia ya chaguzi nchini Tanzania. Pengine hili halionekani sana kwa wenzetu mlio huko nyumbani, lakini kwa sie tulio mbali, teknolojia imekuwa ikituwezesha kufuatilia mengi ya yanayojiri katika pilika za uchaguzi kana kwamba yanatokea huku tulipo muda huu.

Na eneo la teknolojia ambalo linahusika zaidi na habari za harakati za uchaguzi huko nyumbani ni kile kinachofahamika kitaalam kama Web 2.0, yaani maendeleo ya teknolojia ya mtandaoni yanayohusisha vitu vinavyowekwa mtandaoni na watumiaji wa kawaida. Tumeingia katika zama ambapo badala ya kusubiri taarifa ya habari ya Redio Tanzania enzi zile, sasa mtu aliyepo Ifakara, kwa mfano, anaweza kutuma habari mtandaoni na ikapatikana dunia nzima.
Teknolojia inawezesha habari mbalimbali za uchaguzi kupatikana katika namna inayofahamika kama ‘in real time’ yani kitu kinatokea na kuripotiwa muda huo huo na kuwafikia wasomaji/watazamaji/wasikilizaji muda huo huo.
Licha ya Katiba yetu kutunyima fursa Watanzania tulio nje ya nchi, teknolojia imetuwezesha kushiriki katika siasa zinazohusiana na uchaguzi huu kwani baadhi yetu tunaweza kumudu kuandika habari zinazohusu kana kwamba tupo huko, ingawa ukweli ni kutokana na kufuatilia kinachoendelea huko kupitia mtandaoni. Ni katika mazingira hayo, wakati huu nimekuwa nikiandika kitabu kuhusu uchaguzi huo (kinatarajia kuchapishwa mwezi huu) kwa kutegemea taarifa na habari zilizopatikana kupitia teknolojia ya mtandao kwa takriban asilimia 100.
Tukiachana na tukio hilo la kihistoria, uzinduzi wa kampeni za CCM na Ukawa umeweza kupigia mstari hisia zilizokuwepo awali kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu una upinzani ambao kwa hakika haijawahi kutokea katika historia ya taifa letu. Cha kusikitishwa, hata hivyo, ni kwamba badala ya ushindani huo kuelemea kwenye sera, suala lililogusa wengi, angalau huko mtandaoni, ni idadi ya wahudhuriaji.
Badala ya wafuasi kushindana kuhusu ubora au mapungufu ya sera, suala liloonekana muhimu zaidi ni ‘uzinduzi wa nani uliohudhuriwa na watu wengi zaidi.’ Lakini hili si la kushangaza sana kwa tunaofuatilia mengi ya yanayoendelea huko nyumbani. Watanzania wengi wanaendeshwa na matukio. Na kibaya zaidi, ni wepesi wa kusahau. Kwa wana-CCM, wingi wa watu kwenye uzinduzi wa kampeni zao waonekane ni kila kitu bila kujali iwapo chama chao kimebadilika na kutambua kuwa kina deni kubwa kutoka kampeni na awamu zilizotangulia.
Kwa wana-Ukawa, hali sio tofauti. Wanaonekana kupuuzia ukweli kuwa hata katika chaguzi zilizopita, walikuwa wakipata umati mkubwa katika kampeni zao lakini haukuweza kuwasaidia kushinda nafasi ya urais.
Uzoefu watuonyesha kuwa uzinduzi wa kampeni huwa fursa nzuri kwa chama husika kuelezea japo kwa ufupi kuhusu mipango yake ya kuwatumikia wananchi iwapo kitapewa ridhaa ya kuwaongoza. Kwa kulinganisha uzinduzi wa kampeni za CCM na Ukawa, yayumkinika kuhitimisha kuwa Magufuli alimudu kuelezea japo kwa kifupi kuhusu ilani ya chama chake, na pengine kutoa mwanga kwa wapigakura watarajie nini kutoka kwake iwapo atashinda uchaguzi huo.
Lowassa, kwa upande mwingine, ameshindwa kufuta ‘tuhuma’ dhidi yake kwamba amekuwa akishindwa kutumia vema fursa ya umati mkubwa unaojitokeza kumsikiliza, na hotuba zake zimekuwa fupi mno.
Japo ‘watetezi wa Lowassa’ wanadai kuwa kinachohitajika si hotuba ndefu au maneno mengi bali vitendo, lakini utetezi huo hauondoi hisia kwamba mwanasiasa huyo ana upungufu katika kubainisha kwa maneno mpiango au mikakati yake. Ni muhimu kutambua kuwa asilimia kubwa ya wapiga kura sio wanachama au wafuasi wa vyama vya siasa, na moja ya vityu vinavyoweza kuwasaidia kufanya uamuzi kuhusu nani wampe kura yao ni yanayobainishwa katika hotuba za wagombea.
Lakini kingine ambacho ninaweza kukieleza kama kosa la kimkakati ni maelezo ya Ukawa kupitia Chadema kuwa ilani yao itawekwa kwenye tovuti yao. Ndio, nimebainisha hapo juu kuhusu mchango wa teknolojia katika uchaguzi mkuu huu. Hata hivyo, takwimu za hivi karibuni zaonyesha kuwa ni takribani Watanzania milioni nane tu wenye kuweza kupata huduma (access) ya Intaneti. Na tukichukulia makadirio ya idadi ya sasa ya Watanzania kuwa ni watu milioni 50 (ninasisitiza ni makadirio tu), basi takriban watu milioni 40 hawataiona ilani ya uchaguzi ya Ukawa/Chadema kwa vile hawana Intaneti.
Na hadi muda huu ninapoandika makala hii, kilichopo kwenye tovuti ya Chadema ni hotuba tu ya Lowassa aliyoitoa siku ya uzninduzi wa kampeni. Nimejaribu kuuliza iwapo hotuba hiyo ndio ilani ya Chadema/Ukawa lakini sijapewa jibu.
Kwa upande wa CCM, bado ninaona kuna tatizo la kuendeleza ahadi badala ya kukiri makosa katika maeneo ambayo, baadhi yetu twaamini yamechangia kuimarisha vyama vya upinzani kama vile Chadema. Chama hicho tawala kinapaswa kutambua kwamba hali ya nchi yetu sio nzuri, na binafsi ninaiona hiyo ndio sababu kuu ya sapoti kubwa anayopata Lowassa: imani ya wanaomuunga mkono kwamba “hata kama ana mapungufu yake, atatusaidia kuiondoa CCM madarakani.”
Hadi muda huu sijaona jitihada za maana kwa Magufuli na CCM kuwa honest kwa Watanzania kwa kuwaeleza bila ‘kuuma maneno’ kuwa “jamanai, hapa tulikosea na tunakiri makosa. Ili kurekebisha makosa hayo na kutoyarudia tena, tutafanya hili na lile.” Hatua ya kwanza ya kuondoa tatizo ni kulitambua na kulibainisha, kisha kuandaa mkakati wa kuliondoa. Kukiri kosa si upungufu bali dalili ya uelewa wa changamoto zinazomkabili mhusika.
Lakini Lowassa na Ukawa yake wasitegemee sana hisia kuwa ‘upungufu wa CCM, ni ubora wao.’ Laiti CCM wakifanikiwa kubainisha upungufu wao na kueleza jinsi watakavyoyakabili, Ukawa watalazimika kuwaeleza Watanzania nini wao watakifanya bila kujali CCM wanasema nini.
Wakati Magufuli na CCM wameendeleza mlolongo wa ahadi zilezile zilizozoeleka masikioni mwa wapigakura, kuna maeneo ambayo binafsi ninayaona ‘hatari’ kwa Lowassa na Ukawa. Kwa mfano, Lowassa ametoa ahadi ya kuwaachia huru watuhumiwa wa ugaidi huko Zanzibar, jambo ambalo limepelekea moja ya Jumuiya za Kikristo kumlaumu kwa vile miongoni mwa kesi zinazowakabili watuhumiwa hao ni ya mauaji ya padre huko Visiwani. Kutafuta pointi rahisi za kisiasa kwaweza kuwa na madhara makubwa kwa mwanasiasa.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa watumie fursa hii ya kampeni kuwapima kwa makini wagombea wote, si wa urais tu bali pia katika nafasi za ubunge na udiwani, na kuwachagua wale tu wanaowaamini watawatumikia kwa dhati. Pia nitumie fursa hii sio tu kukipongeza chama cha ACT Wazalendo kwa uzinduzi wa kampeni unaoweza kuhitimishwa kuwa bora zaidi ya wa CCM na ACT bali pia kuonyesha dalili kuwa chama hicho kinaweza kuwa ngome kuu ya upinzani huko mbeleni.
Nitaendelea na uchambuzi kuhusu uchaguzi mkuu katika makala zijazo.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.