23 Sept 2015

BAADA ya harakati na pilika lukuki za vyama vyetu na wanasiasa kusaka fursa ya kumrithi Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, hatimaye tumefikia takriban mwezi mmoja tu kabla ya ‘siku ya hukumu’ kutimia.
Kufikia Septemba 23, tumebakiwa na mwezi mmoja na siku mbili kabla Watanzania hawajapiga kura kumchagua rais mpya, sambamba na kuwachagua wabunge na madiwani katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25, 2015.
Pengine ni mapema mno kufanya tathmini inayoweza kutoa mwelekeo wa chama kipi kitaibuka kidedea au mgombea gani wa urais atashinda, lakini angalau sote twatambua kuwa kwa upande wa urais, mshindi atakuwa aidha Dk. John Magufuli, mgombea kwa tiketi ya chama tawala CCM au Edward Lowassa, mgombea wa Ukawa kupitia Chadema.
Pamoja na changamoto nyingine zitakazomkabili mshindi katika uchaguzi huo, moja kubwa ni kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja baada ya uchaguzi. Sio siri kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umetugawa mno. Na sio kati ya wafuasi wa vyama pinzani tu bali hata walio ndani ya vyama husika na sie wengine tunaojitambulisha kama tusio na vyama.
Kwa upande wa CCM, mchakato wa kumpata mgombea wake umeacha makovu kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizotangulia maara baada ya chama hicho kuruhusu ushindani katika kumpata mgombea wake. Wakati CCM ilipompitisha Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995 kulikuwa na manung’uniko kwamba kada huyo ‘alibebwa’ na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na ‘kuwawekea ngumu’ makada wengine Kikwete na Edward Lowassa waliokuwa wakiwania fursa hiyo pia.
Mchakato wa CCM kumpata mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 uliacha majeraha makubwa zaidi, hasa kwa vile Mwalimu hakuwepo kusimamia mchakato huo, na kwa upande mwingine, Rais aliyekuwa madarakani, Mkapa, ni kama alizidiwa nguvu na kundi la mtandao wa Kikwete. Uchaguzi huo uliacha mpasuko mkubwa zaidi ambao umeigubika CCM hadi muda huu.
Lakini kilichojiri katika uchaguzi wa mwaka huu ni kikubwa zaidi kiasi kwamba kwa mara ya kwanza kabisa, chama hicho tawala kinakabiliwa na upinzani mkali ambao kimsingi ni matokeo ya mpasuko uliokigubika chama hicho tangu mwaka 2005. Kwa mara ya kwanza, CCM sio tu kinakabiliwa na upinzani uliotokana na ushirikiano wa vyama mbalimbali lakini pia mpinzani wake katika nafasi ya urais ni kada wake wa zamani, Lowassa, ambaye hadi anaondoka CCM alikuwa na nguvu kubwa kabisa katika chama hicho.
Kwa upande wa vyama vikuu vya upinzani, hali kwao pia ni tofauti kwa kiasi kikubwa. Kwa mara ya kwanza vyama vikuu vitatu, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, vikishirikiana na NLD, vimeweza kuruka kihunzi kilichowakwaza katika kila uchaguzi, yaani kuafikiana kusimamisha mgombea mmoja. Awali, wazo zima la umoja wa vyama hivyo unaojulikana kama Ukawa, kumsimamisha mgombea mmoja lilionekana kama ndoto ya alinacha, hasa kwa kuzingatia historia. Kwamba kila jitihada iliyofanyika huko nyuma kujenga ushirikiano miongoni mwa vyama vya upinzani haukuweza kufanikia.
Lakini kadri siku zilivyokwenda, taratibu wazo la ushirikiano wa vyama hivyo likaanza kujenga picha kamili kuwa safari hii wamedhamiria kuwa kitu kimoja. Hata hivyo, kosa la msingi na ambalo pengine litawagharimu katikia uchaguzi wa mwaka huu ni kutotumia vema fursa kubwa waliokuwa nayo kukamilisha mchakato wa kumpata mgombea wao na kumnadi kabla CCM hawajafanya hivyo. Ninachomanisha hapa ni kwamba, kwa vile vyama vya upinzani vinauelewa vema mchakato wa CCM kupata mgombea wake- ni kama vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo waweza kudhani itakipasua chama hicho kikongwe- wangetumia fursa hiyo wao kujimmarisha na mgombea wao kiasi kwamba CCM baada ya kumpata mgombea wao wangekutana na mgombea wa Ukawa ambaye sio tu amejiandaa vya kutosha lakini pia anatambulika kwa wapigakura.
Hatimaye, kitendawili cha kwa nini Ukawa walikuwa wakisuasua kumtangaza mgombea wao kiliteguliwa baada ya Lowassa kukatwa CCM na hatimaye kujiunga na Chadema na baadaye kupitishwa kuwa mgombea urais. Kumbe muda wote tulipokuwa tunahoji kwanini Ukawa hawatangazi mgombea wao, wenzetu walikuwa wanamsubiri kitakachodondoka kutoka CCM.
Licha ya ujio wa Lowassa huko Ukawa kuonekana umeleta msisimko na matumaini makubwa kwamba angalau upinzani mwaka huu una mgombea ‘anayeweza kuisumbua CCM,’ kisichoongelewa sana ni mpasuko wa kawaida tu kati ya wanaodhani ni sahihi kumtumia Lowassa katika azma ya kuing’oa CCM madarakani na wale wanaoona kuwa suala hilo sio tu ni usaliti lakini pia linaonyesha mapungufu ya vyama hivyo vya upinzani, kwa maana ya kwamba ilivibidi visubiri mtu kutoka CCM ili kufanikisha azma yao ya kuingiza Ikulu.
Tukiweka kando mazingira ambayo CCM na Ukawa wamepitia hadi tulipo sasa, kuna mambo kadhaa yanaanza kujitokeza ambayo yanaweza kutoa taswira ya matokeo ya uchaguzi huo japo ni muhimu kutambua kuwa, kwanza, si rahisi kubashiri kwa usahihi kabisa matokeo ya uchaguzi wenye ushindani kama wa mwaka huu, na pili, kama wiki moja katika siasa ni sawa na takriban mwaka (kwa maana ya lolote laweza kutokea) muda uliosalia kabla ya uchaguzi ni kipindi kirefu kinachoweza kuathiri ubashiri wowote utakaofanyika muda huu.
Miongoni mwa mambo ya msingi yaliyojitokeza katika kampeni zinazoendelea ni pamoja na lile ambalo wana-Ukawa hawataki kabisa kulisikia, nalo ni mapungufu ya mgombea wao, yaani Lowassa. Sote twaifahamu CCM, na japo mgombea wake, Magufuli ni mgombea kama Lowassa, lakini kimsingi kwa huko Ukawa Lowassa si mgombea tu lakini yeye ndio kama Ukawa yenyewe. Kwa lugha nyingine, uchaguzi huu unakuwa kama vita kati ya CCM na Lowassa, hasa kwa sababu mgombea wa CCM anajinadi kichama zaidi ilhali Lowassa anajinadi na kunadiwa kama Lowassa zaidi.
Moja ya madhara ya wazi ya suala hilo ni uwezekano wa Ukawa kupoteza viti vingi vya ubunge kwa gharama ya kumnadi zaidi Lowassa. Niliwahi kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kuwa nina wasiwasi kuwa mmoja au hata wawili wa viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa kwa upande wa Bara, yaani Freeman Mbowe wa Chadema, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Emmanuel Makaidi wa NLD, anaweza kushindwa katika uchaguzi huo. Pamoja nao ni viongozi wengine wakuu wa vyama hivyo ambao pia ni wabunge, hususan kwa upande wa Chadema.
Iwapo hilo litamtokea, na iwapo Ukawa watashindwa, basi hatma ya vyama hivyo itakuwa mbaya. Kwa Chadema, yayumkinika kuhisi kuwa salama yake pekee ni kufanikiwa kwa jaribio (experiment) la kumtumia Lowassa kuiong’a CCM. Ikishindwa, kuna uwezekano mkubwa chama hicho kikaingia katika mgogoro wa ‘kumsaka mchawi’ ambao waweza kutishia uhai wa chama hicho kilichokubali kutelekeza ajenda yake ya kupambana na ufisadi ili kumtengenezea mazingira mazuri Lowassa.
Kwa NCCR-Mageuzi, ili Mbatia aendelee kubaki kiongozi wa chama hicho itambidi lazima ashinde ubunge anaowania huku akitegemea Lowassa kushinda urais. Kinyume cha hapo yeye na chama chake watakuwa matatani, na hatma ya uhai wa chama hicho kuwa tete. Angalau kwa NLD, Makaidi anaweza kuendelea kuwa kiongozi wa chama hicho hasa ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu ‘chama hicho kimekuwa ni yeye na yeye ndio chama hicho,’ angalau kwa mwonekano.
Lakini kubwa zaidi ni upungufu wa Lowassa kisera na kujinadi. Ajenda ya mabadiliko imekuwa shaghala baghala kiasi kwamba watu wanaimba na kuhubiri mabadiliko pasipo hata kubainisha yatakuwaje. Ukiuliza unaambiwa la muhimu ni kuiondoa CCM kwanza, mengine baadaye. Baadaye lini? Hakuna mwenye jibu.
Kwa upande mwingine, Lowassa ameshindwa kabisa kujinadi. Haiingii akilini kuona umati mkubwa unaojitokeza kwenye mikutano yake ya kampeni ukiishia kuambulia hotuba ya dakika chache tu. Sawa, tumeshasikia hotuba nyingi za wanasiasa na nyingi zimebaki kuwa hotuba tu pasi kubadilisha chochote, lakini huu ni wakati wa uchaguzi, na hotuba ya mgombea ni fursa nzuri ya kubainisha nini atawafanyia wapiga kura na wananchi kwa ujumla pindi wakimchagua. Laiti Lowassa angetumia vema ‘mafuriko’ ya wanaojitokeza kumsikiliza, basi hata hiyo utata kuhusu ajenda ya mabadiliko isingekuwepo kwani angeweza kuwaeleza Watanzania kwa undani kuhusu suala hilo.
Kwa upande wa CCM, licha ya mgombea wake kusimama kama mgombea anayewakilisha chama na si ‘mtu binafsi,’ mtihani mkubwa umekuwa ni jinsi ya kumshambulia Lowassa pasipo kumjengea huruma kwa wapigakura. Lakini mtihani mwingine umekuwa ni kipi hasa cha kukizungumzia kuhusu Lowassa na Ukawa ambao kwa kiasi kikubwa wananadi ajenda ya mabadiliko pasi kuielezea kwa undani. Kwa kutambua hilo, Magufuli amekuwa akijinadi kwa kutumia rekodi yake mwenyewe na zile za chama chake badala ya kuelekeza mashambulizi kwa mpinzani wake. Ni wazi, ili umshambulie mpinzani wako basi angalau awe na cha maana cha kukishambulia, vinginevyo yaweza kutafsiriwa kama uonevu.
Nimalizie makala hii kwa ahadi ya kuendelea na uchambuzi zaidi kuhusu Uchaguzi Mkuu, kwa matarajio ya kuwa na nafasi nzuri ya kufanya ubashiri wa matokeo angalau siku chache kabla ya uchaguzi huo, sambamba na kukumbushana wajibu wetu kijamii kuutumia uchaguzi huo kama fursa ya kuboresha mustakabali wa Tanzania yetu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.