13 Oct 2016

NIANZE makala hii kwa kueleza masikitiko yangu kutokana na tukio lililoripotiwa wiki iliyopita ambapo walimu wanafunzi kadhaa walionekana katika video wakimwadhibu mwanafunzi katika namna isiyofaa na isiyokubalika kabisa. Laiti mtu akiiona video husika bila ya maelezo anaweza kudhani mwanafunzi aliyekuwa akipigwa na walimu hao wanafunzi alikuwa mwizi.
Pamoja na kukerwa mno na kitendo hicho, sikushangazwa na suala zima la vurugu (violence) dhidi ya mwanafunzi husika. Sikushangazwa kwa sababu jamii yetu imekuwa ikisherehesha vurugu. Ni mara ngapi tumeshuhudia polisi wetu wakitumia nguvu nyingi zaidi hata pale ambapo busara tu ingetosha? Ni watumishi wa nyumbani wangapi ambapo tulichokishuhudia kwenye video husika ndio maisha yao ya kila siku, kwa maana ya unyanyasaji wanaofanyiwa na waajiri wao na hawana sehemu ya kukimbilia?
Na je, ni watoto wangapi – hususan watoto wa kambo – ambao kila siku ya maisha yao ni zaidi ya unyanyasaji aliofanyiwa mwanafunzi wa kwenye video husika? Je, ni Watanzania wenzetu wangapi ambao ulemavu wao wa ngozi yaani ualbino umekuwa chanzo cha wao kuwindwa, kukatwa viungo na kuuawa? Na wazee wetu wangapi wameuawa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa vile tu wana macho mekundu (imani fyongo kuwa ni dalili ya ushirikina)?
Na kuhusu vurugu shuleni, kama hilo tukio la walimu hao wanafunzi, sheria za nchi zimehalalisha vurugu kwa kuendelea kuruhusu adhabu za kikoloni kama hiyo ya viboko. Tatizo letu ni kuamini zaidi katika adhabu badala ya kukarabati tabia. Angalia magereza zetu zilivyojaa vibaka na wezi wa kuku badala ya kuwapa kifungo cha nje na kuweka mkazo katika kuwageuza kuwa raia wema.
Tukio hilo sio tu liifumbue macho serikali kuhusu umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kutuhabarisha yale ambayo pengine vyombo vyetu vya habari vya asili visingeweza kuripoti (na hili ni angalizo kwa Rais Dk John Magufuli kuhusu matamanio yake kuona malaika wakishuka na kuifunga mitandao ya kijamii) bali pia liiamshe kuhusu suala la viboko shuleni. Adhabu ya viboko imepitwa na wakati, ni kandamizi, ni mwendelezo wa vurugu dhidi ya watoto na si ya kistaarabu.
Baada ya kuzungumzia suala hilo la kipigo cha walimu hao kwa mwanafunzi, nigusie mada ya wiki hii ambayo pia inahusu elimu. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipiga marufuku wanafunzi kwenda shuleni pekupeku au na nguo zilizochanika.
Alitoa maagizo hayo katika ziara yake mjini Kibiti, Pwani wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo kwenye mkutano wa hadhara. Waziri Mkuu alisema;  “Zile fedha mlizokuwa mnatumia kulipa ada na michango sasa zitumieni kununua sare na chakula cha watoto wenu, ni marufuku mtoto kwenda shule huku akipekua au akiwa amevaa sare zilizochanika,”
Hivi kweli Majaliwa anadhani wazazi wa watoto wanaokwenda shuleni wakiwa pekupeku au na nguo zilizochanika wanafanya hivyo kama ‘fasheni’ ya suti za waheshimiwa wetu? Hivi kweli Majaliwa hajui kuwa ni umasikini wa kupindukia unaosababisha baadhi ya Watanzania wenzetu kutomudu uwezo wa kuwanunulia watoto wao viatu na sare nzuri?
Moja ya masuala yaliyonikera sana katika miaka 10 ya Awamu ya Nne ni pale viongozi wakuu wa serikali, Rais na Waziri Mkuu wake, wakieleza bayana kuwa hawajui kwa nini Tanzania ni masikini. Lakini angalau wao, licha ya kutoelewa chanzo cha umasikini wetu, hawakuja na amri ya kushangaza kama hiyo ya Majaliwa.
Pamoja na heshima kubwa niliyonayo kwa Waziri Mkuu wetu, ninaomba kutofautiana naye kuhusu amri hiyo. Anachopaswa kufanya ni kutilia mkazo sera zitakazoziwezesha familia masikini sio tu kumudu fedha za kuwanunulia watoto wao sare na viatu, bali angalau kuwa na uhakika wa mlo ujao.
Ni hivi, Waziri Mkuu, kimsingi amri yako ina- criminalise umasikini, kwamba ni kosa kisheria kwa mzazi kuwa masikini kiasi cha kushindwa kumnunulia mwanaye sare bora za shule.
Amri hiyo ya Waziri Mkuu inaonesha jinsi baadhi ya viongozi wetu walivyo mbali na wananchi wanaowaongoza kiasi cha kutoelewa shida wanazokabiliana nazo katika maisha yao.
Nihitimishe makala hii kwa kumsihi Majaliwa atafakari upya kuhusu amri yake hiyo na kwa vile ninaamini anawajali Watanzania wote, wenye kujimudu kimaisha na masikini wasiomudu kununua sare bora za shule kwa watoto wao, atatengua amri hiyo.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.