10 Nov 2016


JUMAMOSI iliyopita ilikuwa siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja kamili tangu Dk. John Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Siku moja kabla ya maadhimisho hayo, Magufuli alifanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari.
Mkutano huo umeibua lawama za aina mbili. Kwanza, lawama nyingi dhidi ya wanahabari kwa kutouliza maswali ya msingi na pili, dhidi ya Rais kwa kutotoa majibu ya kuridhisha.
Kuhusu hizo lawama dhidi ya wanahabari, binafsi sikushangazwa maana tunawaelewa vema wanahabari wetu. Wengi wao wamezoea kupewa habari na kuziandika (mara nyingi kwa mujibu wa matakwa ya mtoa habari). Wanahabari wetu wengi ni waoga katika kuuliza maswali magumu.
Kwa mtazamo wangu, chanzo cha tatizo hilo ni kasumba iliyojengeka zama za chama kimoja, ambapo kimsingi viongozi walikuwa waongeaji na wananchi (ikiwa ni pamoja na wanahabari) ni wasikilizaji tu. Huu utaratibu wa kuuliza maswali viongozi (ambao walikuwa kama miungu-watu katika zama za chama kimoja) bado unaonekana kama mgeni na hakuna jitihada za kutosha miongoni wa wanahabari kuondokana na kasumba hiyo.
Malalamiko kwamba Magufuli hakutoa majibu ya kuridhisha kwa maswali aliyoulizwa, yanategemea mtoa malalamiko hayo. Binafsi, ninampongeza Rais sio tu kwa kujibu maswali kwa umahiri na maelezo ya kina bali pia kwa kuwapa wanahabari wetu muda wa kutosha kuuliza maswali yao.
Siku moja kabla ya mkutano huo, baadhi ya wafuasi wa Chadema walisambaza taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikidai kuwa wanahabari watakaohudhuria mkutano wao na Rais wamekwishaandaliwa maswali ya kuuliza. Kwa lugha nyingine walikuwa wanajaribu kupoteza ‘credibility’ ya mkutano huo. Kwa vile njia ya mwongo ni fupi, jinsi wanahabari walivyopewa uhuru mkubwa wa kuuliza maswali ilionyesha bayana kuwa hakuna mwanahabari aliyepewa maswali ya kuuliza kabla ya mkutano huo.
Wengi wa wanaolalamikia majibu ya Rais ni hao hao wenye tofauti za kiitikadi na CCM, chama ambacho Magufuli ni mwenyekiti wake wa taifa. Kwa hiyo, hata kama Rais angejibu vizuri kiasi gani maswali aliyoulizwa, bado wapinzani wake wa kisiasa wangemlaumu. Ndio siasa zetu zilipofikia.
Pamoja na uchaguzi mkuu uliopita kutimiza mwaka mzima sasa tangu umalizike na kutupatia Magufuli kama Rais wetu, bado kuna kundi kubwa tu ambalo, kwa upande mmoja, ni kama haliamini kuwa mpinzani mkuu wa Magufuli kwenye uchaguzi huo, mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, kweli alishindwa katika uchaguzi huo.
Hali hiyo inaendana na upinzani mkali dhidi ya kila linalofanywa na Rais Magufuli na serikali yake. Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mwenendo wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema baada ya uchaguzi mkuu na yayumkinika kuhitimisha kuwa ajenda kuu ya chama hicho kwa sasa ni kumpinga Dk. Magufuli kwa nguvu zote, hata katika masuala yenye maslahi kwa taifa.
Kwa namna fulani, upinzani huo, ambao sio kosa kisheria, umezaa genge dogo lakini lenye ushawishi mkubwa miongoni mwa wafuasi wa Chadema ambalo kwa ‘anything goes’ (lolote sawa tu) ilimradi urais wa Dk. Magufuli na uongozi wa serikali yake uonekane bomu.
Utekelezaji wa ahadi zake mbalimbali umepokelewa na watu hao kwa mtazamo hasi. Si suala la elimu ya bure au kutumbua majipu, sio kufufua Reli ya Kati au ununuzi wa ndege mbili ili kufufua Air Tanzania kunakowafanya watu hao wathamini jitihada za kiongozi huyo.
Na alipoanzisha operesheni ya kuhakiki vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma, ikaibuliwa hoja ya kizandiki kuwa kabla hajaanza kuhakiki vyeti vya watumishi wa umma, aanze na shahada yake ya uzamivu (PhD) ambayo waliituhumu kuwa ni feki.
Na mmoja wa wahubiri wa tuhuma hiyo kuhusu elimu ya Magufuli aliandika makala katika toleo lililopita la gazeti hili akitetea ‘haki ya kuhoji PhD’ ya kiongozi huyo. Tatizo sio kuhoji bali kumtuhumu Rais kuwa shahada yake hiyo ni feki. Na licha ya kutoa mifano mingi ya hadaa mbalimbali za kitaaluma, mtoa lawama alishindwa kuthibitisha tuhuma zake. Unapomtuhumu mtu kuhusu kosa fulani ni jukumu lako mtoa tuhuma kuzithibitisha tuhuma hizo na sio mtuhumiwa. 
Dk. Magufuli hakujipa shahada ya uzamivu, alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Yeyote mwenye shaka kuhusu shahada hiyo au mbili zilizotangulia (BSc na MSc) anaweza kuwasiliana na chuo hicho au Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kupata uhakika. Kuhoji sio tatizo. Kutuhumu ni zaidi ya tatizo. Ni uzandiki. Na uzandiki (kumfarakanisha Rais na wananchi anaowaongoza kwa kumtuhumu kuwa ana PhD feki) ni tishio kwa usalama wa taifa.
Lakini tatizo hasa sio ndege mbili za Magufuli au PhD yake au majibu yasiyoridhisha kwenye mkutano kati ya Rais na wanahabari. Tatizo ni hao wenzetu ambao ni kama bado wapo kwenye ‘mode’ ya uchaguzi (election mode), hawataki kukubali kuwa mgombea wa chama chao alishindwa kihalali, na sasa tuna Rais mpya ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwaka sasa. Na wenye nia njema na Tanzania yetu wanaridhishwa mno na utendaji kazi wa Rais huyo, hususan katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi, ajenda iliyokuwa nguzo ya Chadema kabla ya kumpokea Lowassa (mwanasiasa ambaye chama hicho kilimtuhumu kwa miaka tisa mfululizo kuwa ni fisadi, kabla ya kugeuza ‘gia’ angani na kumteua kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho).
Japo kila mgombea anapaswa kuwaaminisha wafuasi wake kuhusu fursa za kushinda katika uchaguzi, binafsi ninaona kama matumaini ambayo Lowassa aliwapatia wafuasi wake yalikuwa ya kina mno kiasi kwamba mwaka mmoja baada ya mwanasiasa huyo kubwagwa kwenye uchaguzi mkuu, bado wafuasi wake wengi hawaamini kilichotokea.
Lakini pia kuna kundi ambalo sio tu liliamini kuwa ushindi wa Lowassa ulikuwa sio wa mwanasiasa huyo pekee bali nao walikuwa na matarajio ya nyadhifa fulani, hususan wale ambao jitihada zao za kuwania nafasi kama ubunge ziliishia kwenye ngazi ya kura za maoni tu. Kwa Lowassa kushindwa kwenye uchaguzi huo ilimaanisha kuwa nao ndoto zao za madaraka ziliota mbawa.
Nimalizie makala hii kwa kumpongeza Dk. Magufuli kwa kutimiza mwaka mmoja wa urais uliosheheni mafanikio lukuki. Amefanikiwa sio tu kuitoa Tanzania yetu kutoka chumba cha wagonjwa mahututi bali pia ameweza kurejesha nidhamu ya kazi na kuondoa dhana kwamba uhalifu (ufisadi, ujangili, kuuza unga, nk) ndio njia halali ya kipato. Wengi wa wanaomlaumu Dk. Magufuli kuwa amefanya maisha kuwa magumu ni watu waliokuwa wakiishi kwa kutegemea ‘dili.’
Na kwa wanaolalamika kuwa Dk. Magufuli ni dikteta, anaminya uhuru wa vyama vya upinzani labda kwanza waanze kudai demokrasia ndani ya vyama vyao ambavyo baadhi vimekuwa kama vya kisultani kwa kuwa na sura zile zile za viongozi wakuu miaka nenda miaka rudi pasi chaguzi kuu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.