3 Nov 2016


JUMAMOSI wiki hii, Rais Dk. John Magufuli atatimiza mwaka mmoja kamili tangu aingie madarakani kama Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufanya tathmini ya tangu Magufuli atangaze nia ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM, na hatimaye kuchaguliwa kuwa mgombea wake, kabla ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana na kuapishwa, kabla ya kuanza jukumu zito la kuiongoza nchi yetu, ni kitu kinachohitaji kitabu kizima.
Bahati nzuri, huko nyuma niliandika kitabu kuhusu ‘safari’ hiyo ya Dk Magufuli, japo tathmini iliisha kwenye takriban miezi mitatu tangu aingie rasmi madarakani. Wakati huu, ninaandaa kitabu kitakachochambua mwaka mzima wa kiongozi huyo tangu aingie madarakani.
Hata hivyo, hata bila kutumia kitabu, yawezekana kufanya muhtasari wa tathmini ya kipindi cha mwaka mmoja wa Magufuli na serikali yake ya Awamu ya Tano kwa ujumla. Na njia nyepesi ya kufanya tathmini hiyo ni kuangalia maeneo tunayoweza kuyaita mafanikio na yale yasiyo mafanikio.
Katika mafanikio, Rais Magufuli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza ahadi alizotoa binafsi kama mgombea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na zilizotolewa na chama chake katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Moja ya ahadi hizo ilikuwa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Katika eneo hili, Rais Magufuli amefanikiwa mno.
Kwa vile tayari Magufuli na serikali yake wameonyesha kuwa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ni kitu kinachowezekana, ni rahisi kwa baadhi ya watu kuona kuwezekana huko ni suala la kawaida tu. Ni rahisi pia kusahau ugumu uliotawala suala hilo kwa miaka kadhaa, kiasi kwamba baadhi ya tafiti kuhusu maoni ya wananchi kuhusu rushwa na ufisadi zilionyesha kuwa idadi kubwa tu ya wananchi “walishasalimu amri” kwa rushwa na ufisadi kuwa ndio hatima yao. Kwamba hata zifanyike jitihada za aina gani, rushwa na ufisadi vitaendelea kushamiri.
Kwa hiyo, licha ya kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi, Dk. Magufuli amekuwa akipambana na mfumo pia ulitoa mizizi kwenye saikolojia ya taifa letu. Kwa mafanikio yaliyokwishapatikana hadi muda huu, huku tukisubiri kuanza rasmi kwa mahakama ya ufisadi, kwa hakika Magufuli anastahili pongezi.
Ndio, kuna changamoto kadhaa kwenye sekta mbalimbali kama vile afya na elimu, lakini ni muhimu kufahamu kuwa ili tuwe na ufanisi kwenye sekta mbalimbali ni lazima kwanza tujenge nidhamu ya mapato na matumizi, sambamba na kubana mianya ya rushwa na ufisadi, ambayo kimsingi ndio iliyodidimiza sekta hizo. Sasa, kama ambavyo maradhi huingia mwilini na pengine kusambaa kwa kasi lakini huchukua kitambo kuyatibu, ndivyo ambavyo tunahitaji ustahimilivu kabla ya jitihada za Magufuli hazijaanza kuonekana kwa wingi na kwa wazi zaidi zikileta mabadiliko katika maeneo mbalimbali.
Eneo jingine ambalo Magufuli amefanikiwa ni kurejesha heshima ya kazi. Kwa muda mrefu, kulikuwa na imani fyongo kwamba ‘uhalifu unalipa’ (crime pays) na wenzetu waliofanya bidii kwenye kazi halali au kujiajiri kwa biashara au kilimo walionekana kama vituko. Lakini sasa tunashuhudia wimbi kubwa la wenzetu wakiwekeza kwenye kilimo na shughuli nyingine za kujiingizia kipato halali. Kadhalika, imani kwamba mtu anaweza kuishi kwa kutegemea kipato halali imeanza kurejea kwa kasi. Hili nalo si jambo dogo kwa sababu sio tu linahusu mfumo bali pia saikolojia ya taifa.
Awali nilikuwa miongoni mwa wasiopendezwa na jinsi Serikali ya Magufuli ilivyoonekana kuvibana vyama vya upinzani. Na katika kuthibitisha hilo, niliandika makala moja kuishauri serikali kuhusu suala hilo. Hata hivyo, nilichokishuhudia tangu wakati huo hadi sasa, kinaweza kuhalalisha umuhimu wa serikali kuchukua msimamo mkali dhidi ya baadhi ya vyama vya siasa au wafuasi wa vyama hivyo.
Sawa, kila mwananchi ana haki ya kumkosoa rais au serikali yake. Hata hivyo, kuna kukosoa kwa ajili ya kujenga na kukosoa kwa ajili ya kubomoa. Kwa makusudi, baadhi ya Watanzania wenzetu huko kwenye upinzani, pengine kutokana na kukosa ajenda yoyote kwa maendeleo ya vyama vyao, wamewekeza nguvu kubwa mno kuchochea chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao.
Kwa vile hatupaswi kutoa fursa yoyote ile ya kuruhusu uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki ambapo serikali ya Magufuli inafanya jitihada kubwa za kuiweka Tanzania yetu katika mahali inapostahili kuwepo, ninaunga mkono hatua za serikali dhidi ya yeyote anayejaribu kuchochea uvunjifu wa amani. Demokrasia ya kuchochea wananchi dhidi ya serikali yao ni uhuni. Watanzania wanahitaji maendeleo na sio kuwachonganisha na serikali yao.
Kama kuna eneo ambalo ninaweza kumkosoa Rais Magufuli ni kuhusu baadhi ya watu aliowakabidhi dhamana ya kumsaidia. Awali alieleza kuwa angeunda baraza la mawaziri dogo tu lenye ufanisi na atakayevurunda atawajibishwa. Nina hakika rais anawafahamu vema baadhi ya mawaziri ‘mizigo’ ambao wana kila dalili ya kumchafua kwa wananchi. Naam, wakiboronga wao, atakayelaumiwa ni aliyewateua. Ingekuwa vema rais akitumia maadhimisho haya ya mwaka mmoja madarakani kutathmini utendaji wa baadhi ya mawaziri wake na wale walioshindwa kuendana na kasi yake, wapumzishwe.
Sambamba na hilo ni doa la kisiasa huko Zanzibar linaloendelea kuchafua sura ya Tanzania. Wakati ni Wazanzibari wenyewe wanaoweza kufikia mwafaka wa kudumu wa mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa visiwani humo, kuna haja kubwa tu kwa Serikali ya Muungano ‘kutomwagia petroli kwenye moto,’ kwa maana ya kujiepusha na kauli ambazo zinaweza kuchochea mfarakano zaidi visiwani humo.
Nimalizie makala hii kwa kukupongeza Rais Magufuli kwa kutimiza mwaka mmoja tangu uapishwe kuwa rais wetu. Wengi wanaokupinga au kukulaumu ni watu waliozoea kula vya bure, waliovuna wasichopanda, waliofakamia keki ya taifa kifisadi, watu ambao zama za Ujamaa tuliwaita kupe. Endelea kukaza uzi ili mabadiliko unayokusudia na yanayohitajiwa mno na Watanzania yatimie. Asante kwa kuanzisha safari ya Tanzania yetu kuelekea mahali inapostahili kuwa na kamwe usiyumbishwe na wanaotaka kutukwaza.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube