16 Mar 2017


MAJUZI, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilifanya Mkutano wake Mkuu Maalum huko Dodoma, ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa na ajenda kuu ya "kujadili na kupitisha marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la 2012, pamoja na kanuni za chama hicho na jumuiya zake."
Nimeyawekea msisitizo maneno "kujadili na kupitisha" kwa sababu inaonekana kuwa wazi kuwa majadiliano yaliyofanyika hayakupaswa kutoyapitisha marekebisho hayo.
Ni rahisi kutafsiri hatua hiyo kama ya kuminya demokrasia (kwa maana kwamba kujadili pekee hakutoshi bali pia kuwepo uhuru wa kuyakubali au kuyakataa mapendekezo husika) lakini pengine ni rahisi pia kutambua kwanini CCM "ilijihami" mapema.
Mabadiliko hayo ya katiba ya chama hicho yamepelekea kupungua idadi ya wajumbe wa vikao vya ngazi za juu vya chama hicho na kupunguza 'kofia mbili' kwa viongozi wenye vyeo ndani ya chama, serikalini au bungeni.
Kutokana na mabadiliko hayo, mwanachama anatakiwa kushika nafasi moja tu ya uongozi, katika ngazi za Mwenyekiti wa Tawi, Kijiji, Mtaa, Kata, Wadi, Jimbo, Wilaya na Mkoa. Wengine ni Makatibu wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote, Diwani na Mbunge/Mwakilishi.
Kwa hiyo ni wazi kuwa mabadiliko hayo yanawaathiri 'vigogo' kadhaa wa chama hicho, na pengine ndio maana ikaamuliwa kuwe na "mjadala na kupitisha mabadiliko hayo" badala ya "mjadala na kupitisha au kutopitisha mabadiliko husika."
Kadhalika, mabadiliko hayo yatapelekea kupungua kwa idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, kutoka 34 hadi 24.
Vilevile, idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho imepungua zaidi ya nusu, kutoka 388 hadi 168.
Miongoni mwa 'vigogo' waliotarajiwa kuathiriwa na mabadiliko hayo kutokana na kushika nyadhifa zaidi ya moja ni pamoja na William Lukuvi, Makame Mbarawa, Dk. Hussein Mwinyi, na Shamsi Vuai Nahodha.
'Kigogo' mwingine ni Mama Salma Kikwete, ambaye licha ya kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa wa Lindi, hivi karibuni aliteuliwa na Rais  Magufuli kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.
Wengine ni wenyeviti wa CCM mikoa ambao pia ni wabunge, kama vile Joseph Musukuma, Martha Mlata na Deo Simba, ilhali Godfrey Zambi ni mbunge na mkuu wa mkoa, Adam Kimbisa ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma.
Kuna usemi mmoja, kwamba sio kila kitu sahihi ni kizuri, na sio kila kitu kizuri ni sahihi. Uamuzi wa CCM kuwapunguzia wanachama wake kofia zaidi ya moja kwenye uongozi ni sahihi lakini sio mzuri kwa watakaoathiriwa nao.
Jicho la uchambuzi litaelekezwa kwa 'wahanga' hao kadri chama hicho kinavyoingia kwenye mchakato wake wa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, na kwenye kinyang'anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao, mwaka 2020.
Siku moja kabla ya Mkutano huo Mkuu Maalum, chama hicho tawala kilitangaza adhabu kwa viongozi wake kadhaa, kubwa zaidi ikiwa kuwavua uanachama viongozi 12 akiwemo Sophia Simba, kada mkongwe wa chama hicho na ambaye hadi anapewa adhabu hiyo alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT), mjumbe wa Kamati Kuu na Mbunge.
Hatua hizo kali zilizochukuliwa na CCM chini ya uenyekiti wa Rais Magufuli, sambamba na mabadiliko niliyoyaongelea awali, yana tafsiri kuu mbili.
Kwanza, hatua kali za kinidhamu zinapeleka ujumbe kwa wana-CCM wa kada mbalimbali kuwa Rais Magufuli amepania kwa dhati kukisafisha chama hicho tawala.
Pili, mabadiliko kusudiwa, sambamba na hatua kali zilizochukuliwa dhidi ya viongozi kadhaa wa chama hicho, ni mtihani mkubwa, kwa Mwenyekiti Magufuli na CCM kwa ujumla.
Kwa Mwenyekiti Magufuli, hatua hizo zimemwongezea idadi ya maadui zaidi ya wale ambao tayari ni waathirika wa msimamo wake dhidi ya ufisadi na rushwa, ambapo watendaji kadhaa wa serikali wametumbuliwa huku wakwepa kodi wakidhibitiwa, na majangili na 'wauza unga' wakibanwa.
Japo ni mapema mno kufanya tathmini timilifu kwa hatua hizo, ile kuzichukua tu sio tu kwaonyesha dhamira lakini pia ni wazi zimetengeneza maadui wa kutosha dhidi ya Dk. Magufuli.
Katika hili, ni muhimu kutambua kuwa ni bora kuwa na kiongozi atakayechukiwa na kwa kutenda vitu sahihi kuliko atakayependwa kwa kufanya madudu.
Siku moja kabla ya Mkutano huo Mkuu Maalum zilipatikana taarifa za kukamatwa kwa makada watatu wa chama hicho, Msukuma, Hussein Bashe na Adam Malima.
Kilichonisikitisha ni maelezo kuwa "walikamatwa na kuhojiwa na polisi kwa tuhuma za kupanga njama za kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa CCM."
Katika mazingira ya kawaida, sio rahisi kwa makada hao watatu kupanga kuvuruga mkutano mkubwa kama huo ila yayumkinika kuhisi kuwa kilichofanyika ni kuzuwia kile nilichogusia awali, yaani "sio kujadili na kupitisha tu mabadiliko husika" bali pia "kujadili na kupitisha au kutopitisha mabadiliko hayo."
Hili la kuminya fursa ya upinzani kwa mabadiliko hayo linaweza kuwa na athari kwa chama hicho huko mbeleni. Sauti za manung'uniko ni kitu cha kawaida lakini sauti hizo zikiakisi mtazamo wa watu wengi, zinaweza kuathiri mshikamano wa chama hicho.
Hata hivyo, kwa wanaotarajia kuwa "CCM itakufa kutokana na mabadiliko haya" wanapaswa wazielewe vema siasa za Tanzania yetu.
Si kwamba CCM itatawala milele, lakini kwa mazingira tuliyonayo hivi sasa, hakuna chama mbadala. Huo ndio ukweli mchungu.
CCM wanaweza kukandamiza upinzani dhidi ya mabadiliko ya Katiba yao lakini angalau wameitisha mkutano mkuu, wamejadiliana na kupitisha mabadiliko ya katiba yao, sambamba na wameadhibu waliokiuka taratibu za chama hicho.
Sio kamili, lakini hiyo yaakisi demokrasia kwa kiasi fulani. Kwa takriban vyama vyetu vyote vya upinzani, jaribio la kufanya kilichofanywa na CCM wiki iliyopita linaweza kutishia “kukiuwa” chama husika.
Ukiangalia wapinzani wakuu wa CCM, yaani Chadema, sio tu "wamegoma kabisa" kufanya tathmini ya kilichowaangusha katika uchaguzi mkuu uliopita bali pia wametelekeza turufu yao kubwa na iliyowajengea imani kubwa kwa Watanzania, yaani mapambano ya dhati dhidi ya ufisadi, yaliyoibua 'List of Shame,' skandali nzito kama Richmond, EPA, Kiwira, nk.
Cha kusikitisha ni kwamba vyama vyetu vya upinzani sasa vimekuwa kama vinachezeshwa ngoma na CCM. Wafuasi wa vyama hivyo "wapo bize" kujadili matukio yanayoihusu CCM badala ya kuwekeza nguvu kwenye mustakabali wa vyama hivyo.
Jiulize, hivi ajenda kuu ya Chadema, au CUF au ACT- Wazalendo ni ipi muda huu?
Ni katika mazingira hayo, baadhi ya viongozi wa CCM watavumilia mabadiliko yanayoendelea ndani ya chama chao kwa sababu hakuna mbadala wa chama hicho tawala kwa sasa. Tumebaki na miaka mitatu na miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu ujao lakini wapinzani wetu wapo bize kuijadili CCM na serikali yake badala ya kujipanga vyema kwa uchaguzi ujao.
Moja kati ya vitu vilivyoiangusha UKAWA katika uchaguzi mkuu uliopita ni "kusubiri makapi ya CCM" badala ya kutangaza mgombea wao mapema na kisha kumnadi kwa nguvu zote, kipindi ambacho CCM ilikuwa na shika-nikushike ya makada wake 40+ waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho tawala.
Nihitimishe makala hii kwa kupigia mstari uwezekano wa aina mbili
Kwanza, CCM kuibuka imara zaidi baada ya Mkutano huo Mkuu Maalum pamoja na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya makada kadhaa, kwa sababu nidhamu katika taasisi yoyote ile ni nguzo ya mafanikio, na pia, ili maendeleo yafikiwe shurti kuwepo na mabadiliko, na mabadiliko hukumbana na vikwazo ambavyo vyaweza kurukwa iwapo kuna nidhamu bora.
Japo yaweza kuwa mapema mno kuhitimisha hili, yayumkinika kusema kuwa “mahesabu ya Magufuli yamelipa” kwa maana ya uamuzi wake wa kumteua Mama Salma kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri hivi karibuni unaweza kuwa umesaidia “kumweka karibu” Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM Taifa, na mwenye ushawishi mkubwa katika chama hicho kuliko Dk. Magufuli mwenyewe.
Pili, mambo mawili – hatua dhidi ya makada walioadhibiwa na mabadiliko yaliyopelekea baadhi ya viongozi kupunguziwa nyadhifa – yanaweza kuzua manung’uniko ndani ya chama hicho. Ni wazi kuwa waliochukuliwa hatua za kinidhamu na walioathirika wa kuvuliwa kofia zaidi ya moja za uongozi hawatofurahishwa na hatua hizo. Hata hivyo, je wana pa kukimbilia? Na hapo ndipo utapobaini kuwa siasa za nchi yetu "zingechangamka sana" laiti tungekuwa na upinzani imara.
Na upinzani imara sio lazima upewe ruhusa na serikali kufanya mikutano/maandamano bali kama ule ulioibua 'List of Shame,' Richmond, EPA, nk…hawakuwa na ruhusa ya kufanya hivyo, na pia wanasiasa kama Dk. Willibrord Slaa na Zitto Kabwe walinusurika kwenda jela kwa ajili ya kuwapigania Watanzania.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.