9 Mar 2020


#Thread: Naamini kwamba takriban kila mmoja wetu - hata wale wenye uadui na news - wanafahamu kuhusu balaa jipya la virusi vya #Corona.

Na ni balaa kubwa kweli kweli, maana licha ya wataalam wa afya kutofahamu kwa undani hukusu virusi hivyo, kuna mambo kadhaa yanayoweza kulifanya janga hilo kuwa kubwa zaidi. Hadi wakati naandaa #thread hii, idadi ya maambukizi imevuka watu 100,000 na zaidi ya nchi 90 duniani zimeripoti kufikwa na janga hilo. Japo takriban nusu ya waliokumbwa na virusi hivyo wamepona, idadi ya maambukizi mapya inazua tafaruki kubwa. 

Lakini hofu kubwa zaidi ni pindi janga hilo litakaposambaa barani Afrika, bara ambalo linakabiliwa na changamoto lukuki. Tayari takriban nchi 8 za Afrika zimeripoti maambukizi ya virusi hivyo. Nchi hizo ni Misri, Aljeria, Naijeria, Senegal, Kameruni, Togo, Moroko, na karibu nasi (Afrika Mashariki) ni Afrika Kusini ambakoidadi ya maambukizi hadi jana ni watu wawili. 

Siku chache zilizopita nilihudhuria mkutano flani hapa Uskochi, na japo haukuhusu masuala ya afya, suala la virusi vya #corona liliibuka kwenye maongezi. Kilichonisikitisha ni kwamba watu wengi walionekana kudhani kuwa (a) hofu kuhusu virusi hivyo inakuzwa kuliko hali halisi (b) virusi hivyo ni sawa tu na vya mafua (flu)

Tunaishi katika zama ngumu kwa kweli. Ofkoz, tuna janga jingine (japo si hatari kama virusi vya #corona) na #fakenews. Na kwa hakika watu wana sababu za msingi kutoamini baadhi ya vyombo vya habari hasa kutokana na kasumba ya "kuongeza chumvi" au kuongopa waziwazi. 

Hata hivyo, licha ya kasoro hizo, tegemeo kubwa zaidila kupata jabari ni kwa kupitia vyombo vya habari hivyo hivyo ambavyo baadhi ya watu hawana imani navyo. Na yayumkinika kuamini kuwa endapo vyombo vya habari vikipuuzia kuhusu virusi vya #corona vitaishia kulaumiwa. 

Kuna "janga" jingine huko Marekani. Janga hili ni Donald Trump na wapambe wake. Kwa upande mmoja Trump na wapambe wake wanaamini kuwa "janga hilo la virusi vya #corona linakuzwa makusudi ili yeye aonekane hafai, na hivyo asichaguliwe tena kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo Novemba."


Kwa upande mwingine, Trump na chama chake ni "maadui wa kudumu dhidi ya sayansi." Kwahiyo si jamba la kushangaza kusikia wengi wao wakidai "virusi vya #corona havina tofauti na vile vya mafua (flu)," na kwamba taarifa za wanasayansi na vyombo vya habari ni #fake news. 

Virusi vya #corona ni janga pia kwa sababu kutokana na "upya" wake, inawawia vigumu wataalam wa afya kufahamu vya kutosha kuhusu janga hilo, na hivyo kuwa ngumu kwao kupambana nalo. Ni vigumu kukabiliana na adui usiyemjua vizuri. 

Lakini kama "upya" huo wa virusi hivyo hautoshi kuwa janga kubwa, kuna tatizo jingine la jinsi maambukizi yanavyosambaa kwa kasi. Kwahiyo kwa upande mmoja kuna "race against time" kutafuta chanjo na/au tiba, na kwa upande mwingine ni kukabiliana na maambukizi mapya. 

Ni kwamba, hata mtu akiona dalili zakuwa na virusi vya #corona, anapokwenda hospitali anaweza asipatiwe tiba "ya maana" zaidi ya "tiba ya mafua" kwa sababu hadi muda huu hakuna tiba dhidi ya virusi hivyo. Nimetanabaisha awali kuwa janga hili likisambaa barani Afrika itakuwa balaa kubwa hasa kwa sababu bara hilo linakabiliwa na chngamoto nyingi.

Changamoto hizo ni pamoja na umasikini. Licha ya umasikini ambao umedumu miaka nenda miaka rudi huku baadhi ya wanasiasa wakishindana kutumia #fakenews kuwaaminisha wananchi kuwa umasikini unapungua, kuna umasikini unaochangiwa na vipaumbele fyongo vya serikali zilizo madarakani. 

Pengine ni vema kutumia mifano hai. Kwa mfano wa Tanzania yetu, wakati ununuzi wa bombadia ni muhimu, uwekezaji kwenye sekta ya afya ni muhimu zaidi. Na hauhitaji kuwa mwelewa sana wa Tanzania yetu kubaini kuwa mabilioni yaliyotumika kununua bombadia yalihitajika zaidi mahospitalini.

Kwahiyo moja ya sababu zinazochangia umasikini wa nchi nyingi za Afrika ni vipaumbele fyongo vya watawala. Na japo twaombea Mola aepushe janga hilo lisifike huko nyumbani, vipaumbele vya watawala wetu ni moja ya vikwazo hata wakati huu. 

Kama ambavyo Trump yupo bize kuonyesha kila kitu kipo vizuri huku maambukizi yakisambaa, watawala wetu nao wapo bize kujigamba kuwa "tupo vizuri" ilhali twaelewa vema kuwa wababaishaji hawa hawana A wala B wajualo katika kujiandaa kukabiliana na janga hilo. 

Na majuzi tu tumeshuhudia lundo wa watalii kutoka China wakiwasili huko KIA. Yaani wakati nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo zikidhiditi wasafiri kutoka China, sie hohehae twafanya ubishi katika suala hatari kama hili. Niliandika kirefu kuhusu hilo katika makala hii "Hatuna Uhaba Wa Vingozi Wapumbavu Lakini Hili La Kupuuza #Coronavirus Ni Zaidi Ya Upumbavu (bit.ly/2wHI8oA)

Wakati tunapaswa kuendelea kumuomba Mola ili janga hilo lisitie mguu huko nyumbani, ni muhimu pia kujiandaa kisaikolojia endapo (God forbid) hatimaye litafika huko.atuna Uhaba wa Viongozi Wapumbavu Lakini Hili La Kupuuza #Coronavirus Ni Zaidi Ya Upumbavu

Kuna watakaolaumu kuwa "unatisha watu bure) lakini naamini kuwa ni vema kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Majuzi, Rais Cecil Ramaphosa wa Afrika Kusini alipotangaza kuwa tayari nchi hiyo ina mgonjwa mmoja (wapo wawili hadi wakati naandika makala hii), alitanabaisha kuwa haoni haja ya kuficha ukweli kuwa nchi hiyo nayo imekumbwa na janga hilo. 

Nimegusia hilo kwa sababu utawala wa wa Rais @Magufuli umekuwa maarufu mno kwenye "kanusha,kanusha, na kanusha zaidi." Ni utawala unaotaka kuongelea "habari njema" tu. Je kwa bahati mbaya, virusi hivyo vikiingia Tanzania (Mola aepushie mbali hili), hawatokanusha pia? 

Enewei, lengo la #thread hii sio kuzungumzia vitu vya kufikirika - kwa mfano hali itakuwaje pindi virusi vya #corona vikiingia Tanzania - japo ni muhimu kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Badala yake, lengo ni kutoa elimu kuhusu virusi hivyo, kwa lugha rahisi kueleweka. Na kwa vile mie sio tabibu, nitaeleza kwa lugha isiyo ya kitalaamu/kitaaluma, kwa kimombo wanasema "in layman's language."

Kwanza, wakati janga hilo linafahamika zaidi kwa jina la virusi husika, yaani #coronavirus, maradhi yanayotokana na maambukizi ya virusi hivyo yanafahamika kama COVID-19, kifupi cha "Corona Virus Disease 2019."

Japo kama nilivyoeleza awali kuwa mengi hayafahamiki kuhusu virusi na maradhi husika, watu walio kwenye hatari zaidi ya maambukizi ni ambao tayari wana magonjwa mengine na watu ambao kinga za mwili ni pungufu. Kundi hili linajumuisha watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi. 

Lakini kana kwamba habari hiyo sio mbaya, kwa Afrika kuna tatizo la ziada kuhusu "uhusiano kati ya virusi vya #corona na watu ambao tayari wana maradhi mengine." Kutokana na sababu mbalimbali, kuna idadi kubwa ya watu barani Afrika ambao wana "maradhi mengine" lakini hawafahamu. Aidha hawafahamu kwa vile hawajafanya jitihada ya kufahamu kuhusu afya zao au hawajafahamu kwa sababu wana vipaumbele vingine muhimu zaidi ya kufahamu kuhusu afya zao.

 Kuna watu wanakwepa kupima ukimwi kwa vile "wana mambo mengi mno kichwani, na wasingependa kuongeza mengine (kama kubaini wana ukimwi baada ya kupima).Na huwezi kumlaumu mtu "anayekwepa habari mbaya kwa vile hata akijua hatojua cha kufanya kuhusu habari hiyo mbaya.

Kingine cha kuogofya kuhusu virusi hivyo ni ukweli kwamba ni vigumu mno kukwepa "mikusanyiko" katika maisha yetu ya kila siku barani Afrika. Hebu pata picha ya sehemu kama "Shimoni Kariakoo" au kwenye jinsi daladala zinavyopenda "nyomi" (hivi msamiati huu bado hai?)

Kama nilivyotanabaisha awali, kuna wanaodai "COVID-19 ni sawa na mafua tu." Japo mie si mwanasayansi, lakini kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wakati "kiwango cha vifo" (mortality rate) kwa mafua ni 0.1%, kwa upande wa COVID-19 tayari ni 2.5% na huenda kiwango hicho kikaongezeka. 

Hata hivyo, kiwango hicho ni kidogo kulinganisha na "majanga" mengine kama Ebola, ambayo "mortality rate" yake ni kati ya 25% na 90%. Again, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa upande wa COVID-19 kutokana na kusambaa kwake kwa kasi. 

Wengi wa wanaopatwa na maambukizi ya virusi vya #corona huwa na dalili kama za homa kidogo, kikohozi na kupumua kwa shida kidogo. Takriban 20% ya wagonjwa afya zao huwa mbaya na kupatwa na "numonia" (pneumonia) na matatizo makubwa ya kupumua yanayoweza kupelekea mtu apumue kwa mashine.

Lakini si kila anayeambukizwa virusi vya #corona huugua sana au kwa wastani. Makundi yaliyo kwenye hatari zaidi ni watu ambao tayari wana maradhi mengine kabla ya kuambukizwa virusi hivyo: 5.6% kwa wenye kansa; 6% kwa wenye "BP," 6.3%; 7.3% kwa wenye kisukari na 10.5% kwa wenye ugonjwa wa moyo. 

Kundi lililo kwenye hatari kubwa zaidi ni wazee wenye miaka 80 na kuendelea, wakiwa na takriban 15 ya maambukizi ya virusi hivyo hatari. Hata hivyo, habari njema ni kwamba watoto hasa wenye chini ya umri wa miaka 9 wanaonekana kutoathiriwa na janga hilo. 

Kadhalika, takwimu zilizopo zinaashiria kuwa wanaume wapo hatarini zaidi kuliko wanawake, lakini takwimu hizo zinaweza kuathiriwa na ukweli kwamba kwa mahali zilipokusanywa, yaani China, wanaume wengi huvuta sigara kuliko wanawake. Hadi muda huu wataalamu hawajui inachukua muda gani kwa virusi hivyo. 

Hata hivyo kwa wanaopatwa na maambukizi ya virusi vya #corona na hatimaye kuugua ugonjwa wa COVID-19, dalili huwa homa, kikohozi na "kuishiwa pumzi," lakini ni za muda mfupi tu. Kadhalika, mtu akifikia hatua ya kuugua COVID-19, seli za njia ya hewa kwenye mapafu huathirika, lakini kuathirika huko "hushtua" kinga ya mwili ambayo hatimaye hukabiliana na virusi vilivyosababisha maradhi hayo, yaani vya #corona. Ndio maana watu wenye mapungufu kwenye kinga ya mwili wanakuwa kwenye hatari pindi wakiambukizwa virusi hivyo.

Njia zinazoshauriwa "kupunguza uwezekano wa maambukizi ya virusi vya virusi hivyo" ni pamoja na kutowajongelea watu wenye maambukizi; kuepuka kufikicha macho na kuepuka kugusa mdomo na pua; kutotoka nyumbani pindi endapo unaumwa; kuziba mdomo kwa tishu pindi unapopiga chafya au kukohoa, na kutupa tishu baada ya kuitumia;


Ushauri wa muhimu zaidi ni kunawa mikono mara kwa mara, na kwa wastani wa sekunde 20, hususan baada ya kwenda msalani, kabla ya kula, baada ya kupiga chafya au kukohoa. Sijui kama unafahamu hili, ila "kanuni isiyo rasmi" ya kunawa mikono ni "kunawa mikono huku unaimba wimbo wa hepi besidei mpaka uishe." Kwa wastani, wimbo huo una sekunde 20

Nimalizie #thread hii kwa kurudia kukumbusha kuwa mie si mwanasayansi wala mtaalam wa afya. Nimeandika #thread hii kwa msaada wa machapisho mbalimbali kuhusiana na virusi vya #corona na ugonjwa wa COVID-19. Nakaribisha kukosolewa na wataalam.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.