Showing posts with label Didas Masaburi. Show all posts
Showing posts with label Didas Masaburi. Show all posts

7 Aug 2011

Picha kwa hisani ya Je Unajua Hii

Masaburi awatusi wabunge

• ATISHIA KULIPUA UFISADI WAO HADHARANI

na Ramadhani Siwayombe, Arusha

MEYA wa jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi, ambaye ametakiwa na wabunge wa jiji la Dar es Salaam kujiuzulu kupisha uchunguzi kutokana na kashfa ya uuzaji kifisadi Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), amewajibu wabunge hao na kusema kuwa kuna baadhi yao wanashindwa kufikiri kwa kutumia vichwa na badala yake wanafikiri kwa kutumia 'makalio'.

Masaburi alitoa kauli hiyo nzito jana mjini hapa alipozungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Naura Spring ambapo anahudhuria mkutano wa pamoja wa kamati za uongozi za serikali za mitaa za nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EACLAT).

Alisema wabunge katika kuchangia hoja ya suala la UDA wamegawanyika katika mafungu matatu ambao alisema katika mafungu hayo moja halijui lolote kuhusiana na sakata hilo na limedandia tu hoja na kuwataja miongoni mwao ni mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, na mbunge wa Mafia, Abdukarim Shah.

Alitaja kundi la pili kuwa ni la wabunge wa jiji la Dar es Salaam ambao ni mbunge wa Ubungo, John Mnyika, na mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambao alisema wanatafuta umaarufu wa kisiasa kupitia sakata la UDA.

Alisema Mnyika aliweza kuhoji hata katika vikao rasmi, lakini Mdee hajui chochote kwa kuwa hajawahi kuhudhuria vikao vya jiji mpaka sasa.

Aidha, kundi la tatu ambalo ndilo alilituhumu zaidi kufikiri kwa kutumia makalio badala ya kichwa ni la wabunge Abasi Mtemvu (Temeke), Musa Azzan 'Zungu'(Ilala) na Makongoro Mahanga (Segerea) ambao alidai kuwa wanajua ukweli wa jambo hilo lakini wanapotosha ili kuficha madhambi yao ambayo alisema yataibuliwa muda si mrefu ya ufisadi ndani ya jiji hilo.

"Hawa wabunge ambao wana nyadhifa toka kipindi kilichopita ndio wanaohusika na kulifilisi shirika hilo na mashirika mengine ya jiji kwa kuwa mchakato wa kuuzwa kwa shirika hilo ulianza toka mwaka 2008 ambapo mimi nilikuwa hata sijawa diwani," alisema Masaburi.

Alieleza kuwa toka kipindi hicho kwa mujibu wa madokezo yaliyopo kuhusiana na uuzwaji wa shirika hilo, yanaonyesha maamuzi yalipitishwa na vikao halali hadi kuuzwa kwake mapema mwaka huu ambapo yeye hajashiriki kwa lolote mpaka wanauziana.

"Mimi ndiye niliyeibua hii tuhuma ya kuuzwa kwa UDA wakati nikihoji mali zinazomilikiwa na jiji na kuambiwa UDA imeishauzwa; nilipofuatilia nikakuta imeuzwa shilingi milioni 285! Nilipofuatilia hizo fedha kama zipo nikakuta milioni 200 zimeshaliwa; nikaamua kumsimamisha meneja wa shirika hilo na mhasibu. Sasa leo nageuziwa kibao kuwa mimi ndiye nimeuza inashangaza sana!" alisema Masaburi.

Aliendelea kusema wabunge hao wanang'ang'ania ajiuzulu kutokana na hofu iliyotanda baada ya kuanza kazi ya kuibua ufisadi ndani ya jiji hilo kwa kuanzia na UDA.

"Baada ya kuibua ufisadi UDA sasa nimepanga nihamie shirika la DDC ambako Mtemvu ni mwenyekiti wa bodi; shirika ambalo nalo kuna ufisadi mkubwa umefanyika ikiwemo kuuza mashamba ya shirika hilo na baadhi ya nyumba," alisema.

Alisema akimaliza suala hilo atahamia kuhakiki matumizi ya ujenzi wa Machinga Complex ambapo alidai inashangaza kusikia zimetumika bilioni 1.2 kujenga zile nyavu za vizimba ambavyo alifananisha na nyumba za wanyama wafugwao.

Alisema kutokana na mkakati wake huo anaomba wabunge wampe muda wa kutekeleza hayo.

Masaburi alisema hawezi kujiuzulu kwa shinikizo la mafisadi na kudai endapo akifuatilia mashirika yote hayo na kubaini yapo sahihi yuko radhi kujiuzulu kama itahitajika.

"Naomba wanipe muda kidogo nisafishe ufisadi ndani ya jiji la Dar es Salaam kutokana na mikataba ya ajabu iliyoingiwa baina ya viongozi waliokuwepo madarakani kipindi cha nyuma wakishirikiana na wabunge na kulitia umaskini jiji ili kama kuna hoja za msingi wabunge wapate hoja za kujadili bungeni," alijinasibu Masaburi.

Alifafanua kuwa kuhusu suala la malipo ya mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo, Iddi Simba, kutoka kwa wanunuzi wa shirika hilo yeye hatambui kwa kuwa hakuna risiti yoyote ya UDA inayoonyesha malipo hayo.

Aliongeza kuwa hata baada ya yeye kupata barua za kuwepo kwa malipo ya sh milioni 320 zilizofanywa kupitia akaunti ya Iddi Simba alimfuata mwenyekiti huyo na kuhojiana naye na alikiri kupokea malipo hayo, lakini alisema hayahusiani na mauzo ya UDA na kusema yanahusiana na biashara zao binafsi.

Alisema kutokana na majibu hayo ya Iddi Simba hakuwa na mamlaka ya kung'ang'ania kuwa malipo hayo ni sehemu ya malipo ya UDA hivyo vyombo kama Takukuru ndio nafasi yao ya kuchunguza suala hilo.

Akizungumzia tamko la Waziri Mkuu kuviagiza vyombo vya Takukuru, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ofisi ya DCI kushughulikia suala hilo, aliunga mkono uamuzi huo kwani ndio utabainisha wazi wote waliohusika katika kuliuza shirika hilo.

Sakata la kuuzwa kwa UDA lilichukua nafasi katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ambapo ilifikia wakati wabunge kutishia kutoipitisha bajeti hiyo na kutaka wote waliohusika katika uuzaji wa shirika hilo wawajibishwe ikiwemo Masaburi kwamba ajiuzulu kabla ya Waziri Mkuu kuingilia kati na kuunda tume kuchunguza suala hilo.

CHANZO: Tanzania Daima

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.