17 Apr 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii na gazeti zima la KULIKONI.Hapa mambo yanakwenda hivyohivyo-kimgongomgongo kama watoto wa mjini huko nyumbani wanavyosema.

Katika makala iliyopita niliwapa picha ambayo kwa namna flani ingeweza kukufanya udhani kuwa kila kitu hapa “kwa mama” ni shaghlabaghala.Hapana.Hapa kuna mambo kadhaa ya kujifunza. Miongoni mwao ni haki za walaji au watumiaji wa huduma mbalimbali, kwa lugha ya hapa “kwa mama” tunawaita consumers au service users. Kilichonipelekea kuandika mada hii ya leo ni matukio mawili yaliyotokea sehemu mbili tofauti: moja hapa nilipo na moja huko nyumbani. La hapa lilikuwa hivi: siku moja nilikuwa nasafiri kutoka Aberdeen, Scotland (mji ninaoishi) kwenda London.Basi nililokuwa nasafiri nalo huwa kwa kawaida linaondoka saa 1.15 usiku na kufika London saa 12 asubuhi. Hawa wenzetu muda ni kila kitu. Hakuna kucheleweshana. Hadithi za “samahani wateja wapendwa, tunasikitika kuwatangazia hili na lile litakalowachelewesha” ni vitu vya nadra sana, japo huwa vinatokea mara chache. Sasa siku hiyo hadi saa 1.30 usiku bado basi lilikuwa halijaondoka. E bwana ee, kasheshe iliyozushwa na abiria hapo ikawa si ya kawaida. Baadhi walianza kudai warejeshewe nauli zao, wengine wakawa wachungu kama pilipili wakiilaani kampuni inayoendesha huduma hiyo ya mabasi. Hatimaye ilitangazwa kuwa basi litaondoka na kwamba kampuni itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa muda wa kufika London utakuwa uleule wa saa 12 asubuhi. Angalau hiyo ilipoza munkari wa abiria, japokuwa baadhi yao walisisitiza kurudishiwa nauli zao na kuchukua usafiri mwingine.

Tukio la huko nyumbani lilikuwa hivi: Mimi nilikuwa naenda Ifakara kuwajulia hali wazazi. Matatizo yalianzia hapohapo kituo kikuu cha mabasi Ubungo.Japo kwenye tiketi ilionyesha basi lingeondoka saa 1.30 asubuhi lakini hadi saa 2.30 hakukuwa na dalili za basi hilo kuondoka. Abiria walikuwa wakilalamika chinichini kwamba tunacheleweshwa bila sababu ya msingi lakini hakuna hata mmoja wao aliefanya jitihada za kuwafahamisha wahusika kuwa wanapuuza haki zetu. Hatimaye kwenye majira ya saa 3 kasoro hivi ndio basi liliondoka. Kati ya Dar na Morogoro basi lilisimama katika maeneo ambayo sio vituo, aidha kwa vile dereva au kondakta alitaka kuchimba dawa au kuongea na akinadada ambao inaelekea walikuwa ni nyumba ndogo zao. Kuna tetesi kuwa madereva wa mabasi yanayokwenda/kutoka mikoani huwa na vimwana kila mji au kijiji kilichopo katika ruti ya basi husika. Madereva msinifungulie mashtaka ya umbeya, mimi sina takwimu zozote kuthibitisha tetesi hizo. Kwa hesabu za harakaharaka tulisimama njiani zaidi ya mara tano, zote zikiwa ni kwa matakwa ya dereva au utingo wake. Badala ya kufika Ifakara majira ya saa 9 tulifika saa 11.Kwa bahati mbaya ndani ya basi hilo kulikuwa na jamaa kama watano hivi waliokuwa wakienda kuwahi mazishi Ifakara.Katika hali ya kawaida watu watano (hasa kama ni ndugu) wana uwezo wa kutosha kushinikiza kutekelezewa haki zao. Lakini hao jamaa waliishia kulalamika chinichini tu kwamba wanacheleweshwa kwenye mazishi.

Ukilinganisha matukio hayo mawili japo yalitokea sehemu mbili tofauti unapata picha kuwa walaji au watumiaji huduma huko nyumbani wanachangia sana kupuuzwa kwa haki zao kwa vile mara nyingi huishia kulalamika chinichini hata pale ambapo umoja wao ungeweza kuhakikisha kuwa haki zao za msingi zinatekelezwa bila mushkeli. Hivi dereva wa daladala na konda wake wanapoamua kuwachelewesha kituoni kwa kisingizio cha kula vichwa wangeweza kweli kufanya hivyo laiti abiria wakitishia kushuka kwenye daladala hiyo au kumshurutisha azingatie muda? Naamini hata kama tungekuwa na akina Mwaibula 100 bado isingekuwa rahisi kuhakikisha kuwa haki za abiria zinatekelezwa ipasavyo iwapo abiria wenyewe hawajishughulishi kuzidai haki zao.

Jamani, tuamke. Hakuna NGO au mtu atakaeweza kuhakikisha kuwa haki zetu zote za msingi kama walaji au watumia huduma zinapatikana ipasavyo iwapo sisi wenyewe tutajifanya hatujali adha tuzopata kila kukicha tunapotumia huduma mbalimbali. Ari, kasi na nguvu mpya ni pamoja na wananchi kuchangamkia kudai haki zao (kwa amani, of course).

Hadi wiki ijayo, alamsiki.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube