18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI

Habarini za huko nyumbani.Hapa shwari.

Mada yangu ya leo najua dhahiri itawakera wateule wachache wa aina flani.Lakini kabla ya kuwapa somo ngoja tuongelee suala la imani na dini hapa napoishi.Nilipofika hapa kwa mara ya kwanza nilionyeshwa majengo kadhaa ambayo hapo awali yalikuwa makanisa lakini sasa yamegeuzwa kuwa kumbi za disko na klabu za usiku.Na hao walioyageuza makanisa hayo kuwa sehemu za starehe wala hawakujishughulisha kubadili mwonekano wake bali wameyaacha yatoe ushuhuda kuwa huko nyuma yalikuwa sehemu za ibada.Nilipofanya udadisi kwa wenyeji niliambiwa kuwa makanisa hayo yaliuzwa baada ya kuwa matupu kutokana na ukosefu wa waumini.Wengi wa waumini wa makanisa ya mji huu naoishi ni aidha wageni (waliotoka nje ya nchi hii kama mimi) au vikongwe.Na si ajabu kukuta kanisa lenye uwezo wa kuchukua watu 500 likiwa na waumini 50 tu.

Binafsi sina majibu ya moja kwa moja kuwa tatizo la hawa wenzetu ni nini.Ila nachofahamu ni kwamba kuna watu kadhaa ambao wanajitambulisha kuwa hawana dini,au hawaamini kuwa kuna Mungu.Pengine labda kwa vile wengine wamezaliwa na kukuta maisha ni mteremko basi hawaoni umuhimu wa kuamini kuwa kuna Mungu.Hata hivyo,imani ni suala la mtu binafsi hivyo pengine si mwafaka kuhoji kwa nini flani anaamini au haamini kuwepo au kutokuwepo kwa Mungu.Japo mie ni muumini wa aina flani huwa sisiti kuwasifu wale wasio waumini lakini hawaoni aibu kuelezea msimamo wao wa kidini.Kwa lugha nyingine watu hao sio wanafiki,wanaelezea bayana kile wanachokiamini au kutokiamini.

Kuna tatizo la msingi huko nyumbani japokuwa natambua dhahiri kwamba watu wengi hawapendi kujadili mambo ya dini.Tatizo hilo ni UNAFIKI.Hivi ndugu zanguni,kama imani unayoifuata na kujidai nayo inakukataza kuvuta sigara si bora usivute tu kuliko kuwachanganya watu?Baadhi ya viongozi wetu wa dini wamekuwa mstari wa mbele sana kuwakemea wale ambao wanakwenda kinyume na imani zao,lakini wakati huohuo viongozi hao wanashirki kwenye maovu wanayoyakemea.Ndio tunatambua kuwa mara nyingi viongozi wetu wa dini wana wafadhili wao nje ya nchi,lakini hicho sio kigezo cha wao kuishi maisha tofauti kabisa na wafuasi wao.Utakuta katika kijiji flani ambacho kimegubikwa kabisa na umasikini,kiongozi flani wa dini anaishi kama yuko peponi vile.Na bila huruma,huku akitumia kisingizio cha maandiko matakatifu,anawashurutisha waumini wake kujipigapiga kuongeza sadaka wanazotoa.Pengine ni ule msemo kuwa alie nacho atazidi kuongezewa na yule asie nacho atanyang’anywa hata kile kidogo alichonacho.

Kinachokera zaidi ni hili ni suala la baadhi ya viongozi wa madhehebu flani kuwa na watoto mtaani huku sheria za madhehebu yao haziwaruhusu kufanya hivyo.Hivi unapomzalisha mwanamke ambae huwezi kumuoa kwa vile majukumu uliyonayo yanakukataza kufanya hivyo si ni sawa tu na kumharibia maisha huyo mwanamke uliezaa nae.Tatizo hili ni sugu sana hususan maeneo ya vijijini.Kinachosikitisha ni ukweli kwamba waumini wanafahamu kuwa kiongozi flani wa dini anaishi kinyume na maadili lakini hawachukui hatua yoyote zaidi ya kulalamika chinichini.Mimi binafsi nina mifano hai ya baadhi ya viongozi wa madhehebu yangu ambao wana watoto lukuki mitaani.Baadhi yao wanatoa huduma kwa wazazi wa watoto hao lakini wengine wamewatelekeza tu.Hawa watu ni wanafiki ambao hawastahili kuachwa wanaendeleza uhuni kwa kisngizio kuwa daraja walilofikia haliwezi kutenguliwa.Mitume wetu waliishi maisha ya uadilifu ambayo yalishabihiana kwa asilimia mia moja na kile walichokuwa wakikihubiri.Na sio kwenye uzinzi tu,bali hata kwenye dili za kibiashara.Wapo wanaopokea kitu kidogo ili,kwa mfano,mtu akiagiza gari lake kutoka nje apunguziwe ushuru kwa vile linaonekana limeagizwa na taasisi ya kidini.Huu ni ukwepaji wa kodi ambao joho la utumishi wa Mungu halipaswi kuwa ngao ya kuzuia mhusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hivi majanga kama ukimwi yataondoka vipi iwapo baadhi ya wale wanaopaswa kukemea vitendo vya ngono kwa vile vinavunja amri ya Mungu nao ni washiriki wa vitendo hivyo?Ndio,maandiko yanataka tufuate yale yanayosemwa na sio matendo ya msemaji lakini katika hali halisi mzazi anayeendekeza ulabu hawezi kueleweka pale anapomkemea mwanae anaefuata mkumbo wake.

Tafadhalini jamani,naomba mhubiri kile mnachokiamini na kukifuata ili kuwasaidia kuwafikisha peponi hao naowahubiria.Na hilo si ndio jukumu lenu?

Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.