22 Aug 2006

KULIKONI UGHAIBUNI


Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa safu hii na gazeti zima la KULIKONI.Natarajia mambo huko nyumbani yametulia.Hapa napo ni shwari.

Kwa takriban mwezi na ushee sasa Naibu Waziri Mkuu wa hapa,bwana John Prescott amejikuta akiwa katika wakati mgumu sana kwenye maisha yake ya kisiasa.Lakini huyu bwana sijui ni lini amekuwa na wakati rahisi licha ya ulaji alionao katika serikali inayoongozwa na Tony Blair.Kuelezea yote yaliyomkumba kunahitaji si chini ya makala kumi kwa vile inaonekana kama mwisho wa balaa moja kwake ni mwanzo wa sekeseke jingine.Hebu anagalia mfano wa vichwa vya habari kwenye baadhi ya magazeti ya hapa na utapata picha ya namna gani anavyoandamwa.“Fungieni mabinti zenu ndani…Prescott ameachiwa madaraka” liliandika Scotland on Sunday baada ya Blair kwenda Marekani,ambapo kwa kawaida itokeapo hivyo nchi inaachwa mikononi mwa bwana Prescott (japo safari hii Blair aliamua kuendesha nchi kutokea ugenini), “Prescott ni mpumbavu (dunce)” liliandika The Sun,na vichwa vya habari kadha wa kadha ambavyo ni nadra kuviona kwenye magazeti ya kwetu.Skendo inayomkabili sasa inahusiana na ziara yake kwenye ranchi ya bilionea wa Kimarekani Philip Anschutz ambapo anatuhumiwa kuvunja sheria za kiuongozi kwa kukaa katika ranchi hiyo na kupokea zawadi ya mavazi ya ki-cowboy (kofia,buti na mkanda) bila kutoa taarifa aliporejea Uingereza.Polisi wa Scotland Yard wamethibithisha kuwa wanachunguza madai yaliyowasilishwa kwao kuhusiana na bwana Prescott kulingana na Sheria za Kuzuia Rushwa za mwaka 1906 na 1916.Hisia za rushwa zinatokana na ukweli kwamba bilionea huyo wa Kimarekani ana mpango wa kujenga casino kubwa kabisa hapa Uingereza na imeonekana kama ukarimu wake kwa Prescott ulilenga kuweka mambo sawa kinyume na maadili.

Rushwa.Ndio,hata huku mambo ya rushwa yapo na tuhuma za hapa na pale si mambo ya ajabu japo ni nadra.Nimesoma gazeti la Nipashe kwenye mtandao ambapo kulikuwa na taarifa kwamba kati ya mwaka 1995 na 2005 Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB au TAKURU) imefanikiwa kuwatia hatiani watu 54.Hivi kweli idadi hiyo ni sahihi au kulikuwa na makosa ya uchapaji?Kwa sababu kama ni kweli basi inabidi Taasisi hiyo iuthibitishie umma wa Watanzania kama kweli ina umuhimu wa kuendelea kuwepo.Watu 54 katika miaka kumi ni wastani wa watu watano tu kwa mwaka.Ifahamike kwamba rushwa ni tatizo sugu sana katika nchi yetu na athari zake zinamgusa takriban kila mmoja wetu,awe kiongozi au mwananchi wa kawaida.Hivi hawa jamaa wa PCB wanataka kutuambia kuwa hata kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambapo baadhi ya watu walikuwa wanapitisha rushwa ovyoovyo tu mitaani wao walishindwa kuwadaka angalau watu kadhaa red-handed?Hivi vita dhidi ya rushwa imekuwa ngumu kiasi hicho au kuna udhaifu flani katika mkakati mzima wa kupambana nayo?Sote tunafahamu kwamba tofauti na nchi zilizoendelea ambapo rushwa inafanywa kitaalamu sana na pengine kuwa vigumu kuwadaka wahusika,huko nyumbani rushwa iko wazi sana kiasi kwamba haihitaji sayansi ya kurusha roketi kuweza kuleta tofauti na hali ya sasa.

Tuambiane ukweli,hayo ambayo wenyewe PCB wanayaita mafanikio ni sawa kabisa na ile hadithi ya akina avae ambapo mtu anauza ng’ombe kwa ajili ya kesi ya kuku.Gharama za kuiendesha PCB ikiwa ni pamoja na mishahara,semina,magari,majengo na vikorokoro kibao hazilingani na mafanikio waliyoyapata katika kipindi hicho cha miaka 10 iliyopita.Hizi hadithi kwamba kuna mikakati inapangwa hazina maana kwa sababu wanaweza kuweka mikakati hiyo kuwa ya siri na sie tukaona matokeo tu.Na hicho ndio tunahitaji:matokeo na sio hadithi kwamba kuna mikakati kabambe huku watu wakiendelea kula rushwa kama desturi vile.Mkurugenzi wa Elimu kwa Jamii wa PCB Lilian Mashaka alikaririwa akisema kuwa dhamira ni kuijenga taasisi hiyo kuwa imara na yenye ufanisi na kuwa mstari wa mbele katika kuzuia na kupambana na rushwa.Maneno hayo yanatia moyo lakini nilishawahi kuyasikia mwaka kati ya mwaka 2001-2002 (sikumbuki vizuri ni lini hasa).Je inamaanisha taasisi hiyo inahitaji karne nzima ya kutengeneza visheni yake halafu karne nyingine ya kujiweka sawa kabla ya kutuletea ufanisi unaohitajika?Na ikumbukwe kuwa katika kipindi hicho tunachosubiri miujiza ya PCB mamilioni ya Watanzania wataendelea kukosa haki zao kutokana na kero ya rushwa.Wapo watakaopoteza maisha yao kwa vile hawana uwezo wa kutoa kidogodogo hospitalini ili wapatiwe matibabu wanayostahili,wapo watakaofariki au kujeruhiwa kwa ajali kwa vile tu trafiki flani wataachia magari mabovu yatembee barabarani na kusababisha ajali,tutaendelea kupata viongozi wabovu ambao wanaingia madarakani kwa vile tu wana uwezo wa kuhonga,wapo watakaoambukizwa ukimwi baada ya kudaiwa rushwa ya ngono wapate ajira au kuwa Miss flani kwenye mashindano ya urembo,wanamuziki wetu wataendelea kutoa rushwa ili nyimbo zao zisikike redioni,na nchi yetu itaendela kuuzwa kwa wawekezaji feki ambao hawana hiana ya kutoa teni pasenti kwa wale walio tayari kusaini mikataba isiyo na akili.

Kinachohitajika PCB ni kujibidiisha zaidi,kuwajibika kwa nguvu zote na uadilifu wa hali ya juu ambao kwa hakika uko kwenye Idara ya Usalama wa Taifa ambayo naamini imekuwa ikishirikiana na TAKURU kuhakikisha watoa na wapokea rushwa wanafikishwa mbele ya pilato.Au pengine PCB ifanywe kuwa sehemu ya taasisi hiyo madhubuti ambayo japo haivumi lakini ipo imara sana katika kuhakikisha usalama wa ndani na nje ya nchi yetu (kigezo kimoja cha udhubuti wa taasisi kama hizo duniani ni kuwepo kwa amani katika nchi zilizo katika maeneo yaliyotawaliwa na matatizo kama ilivyo amani ya nchi yetu ndani ya eneo la Maziwa Makuu.Sio bahati bali naamini hawa wazalendo wanajituma sana katika kutuweka salama).PCB ina faida moja kubwa:ina watoa habari watarajiwa (potential sources) wengi sana.Ni nani hao?Ni mamilioni ya Watanzania wanaotakiwa kutoa rushwa pale wanapohitaji huduma ambazo ni haki yao kuzipata.Kwa mfano,ushirikiano kati ya PCB na madereva unaweza kuisadia sana taasisi hiyo kuwanasa trafiki wala rushwa,vilevile kushirikiana na taasisi za habari kama magazeti kama ThisDay na Kulikoni ambayo yamekuwa yanafichua skandali za rushwa karibu kila siku.Pia ikishirikiana kwa karibu zaidi na wafanyabiashara itakuwa rahisi kuwakamata wanaodai rushwa kupitisha bidhaa bandarini au mipakani,ukadiriaji wa kodi,upatikanaji wa vibali na kadhalika.

Mwisho,najua kwamba makala hii itajibiwa katika namna ya kupingana na hoja yangu.Naomba nisisitize kwamba hoja zangu hazijajengwa kama mkazi wa ughaibuni bali Mtanzania mwenye uchungu na nchi yake.Badala ya kulumbana au kukanusha nawasihi jamaa wa TAKURU wakubaliane na changamoto ninayowapatia.Kasi yao ya kufatilia kesi ni ya konokono,na mwishowe ndio tunaambiwa imepata mafanikio ya kuwatia hatiani wastani watu watano tu kwa mwaka.Watambue kuwa kuchelewesha haki ni sawa na kunyima haki (wamombo wanasema justice delayed is justice denied).

Mwenyezi Mungu tunakuomba uwalaani wala rushwa wakati unaibariki nchi yetu,Amen.

Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube