22 Aug 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-25

Asalam aleykum,

Leo tuzungumzie UKIMWI.Lakini kwa vile mie sio mtaalamu wa afya,sintoingia kwa undani kwenye sayansi ya ugonjwa huo hatari.Kuna usemi kwamba takriban kila mmoja wetu ni “mwathirika” wa Ukimwi.Naomba nieleweke hapo.Napozungumzia “kuathirika” namaanisha kuguswa kwa namna moja au nyingine.Ni nani kati yetu anayeweza kusema hajawahi kuguswa au kuumwa na kifo cha ndugu,rafiki au jamaa yake kutokana na ugonjwa huo?Waajiri wamepoteza waajiriwa,walimu wamepoteza wanafunzi,marafiki wamepoteza marafiki zao,wazazi wamepoteza watoto,majirani wamepoteza majirani wenzao,wafanyabiashara wamepoteza wateja,viongozi wa dini wamepoteza waumini,na kadhalika na kadhalika.Kila mmoja wetu kwa hakika anaguswa au amewahi kuguswa na ugonjwa huo.

Kinachosikitisha ni namna jitihada za mapambano dhidi ya ugonjwa huo yasivyoridhisha.Najua wapo watakaopingana na hoja zangu lakini hiyo hainizuii kuendelea na kelele zangu.Nashawishika kusema kwamba jitihada za kudhibiti Ukimwi zinakwamishwa na ukosefu wa maadili mema miongoni mwetu wanajamii ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wetu.Nasisisitiza BAADHI kwa vile wapo viongozi wanaojitahidi kupiga kelele kila siku kuhusu balaa hilo kwa vile wanajua athari zake kwa sasa na muda ujao.Kiongozi mzinzi hawezi kusimama jukwaani kuwataka watu wawe makini katika mapambano dhidi ya Ukimwi ilhali yeye mwenyewe ana nyumba ndogo za kumwaga.

Kujua ukubwa wa tatizo hilo nchini sio jambo rahisi kwa vile tofauti na nchi za wenzetu ambapo uchunguzi wa afya wa mara kwa mara ni suala la kawaida,huko nyumbani wengi wetu tunakwenda hospitali pale tu tunapojisikia hovyo.Sasa kama walioathirika kwa ugonjwa huo wanafahamika tu kwa aidha kupimwa kwa hiari (na idadi ni ndogo ya wenye ujasiri wa namna hiyo) na wengi ambao wanapimwa kutokana na kufikishwa hospitali wakiwa wagonjwa,tunawezaje kufahamu idadi halisi ya waathirika ambao hawajapimwa?

Nimesoma kwenye tovuti ya Darhotwire kwamba chama cha wanaoishi na virusi hakiridhishwi na mwenendo wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) na kwamba baadhi ya watendaji wa Tume hiyo wanawatumia waathirika kwa manufaa yao binafsi (watendaji hao).Wakati sina ushahidi kama tuhuma hizo ni za kweli,nashawishika kuafiki wasiwasi wao kwa vile huko nyumbani sasa ugonjwa huo umekuwa kama mradi flani.Kuna taasisi kibao ambazo zinadai zipo kwa ajili ya kushiriki katika vita dhidi ya ugonjwa huo,lakini sanasana matokeo yake ni kuwaona wahusika wanabadili tu aina ya mashangingi wanayoletewa na wafadhili na maisha wanayoishi hayawiani kabisa na “uanaharakati” wao dhidi ya ukimwi.

Ni kweli kwamba kwa nchi za Dunia ya Tatu ugonjwa huu una uhusiano wa karibu na umasikini.Lakini pia Ukimwi unahusiana pia na watu wenye nazo.Ngoja niweke mambo bayana unielewe namaanisha nini hapa.Kwenye miaka ya 90 niliwahi kuhudhuria kongamano flani kwenye ukumbi wa British Council hapo Dar.Mada ilikuwa ni iwapo wafanyabiashara wa wenye asili ya Kiasia wanafanikiwa zaidi katika biashara kwa vile wanawazibia wazawa.Mtoa mada mmoja ambaye ni mfanyabiashara na mwanadiplomasia mzawa alieleza bayana kwamba kinachowakwamishwa wazawa wengi ni ile tabia ya kuendekeza matanuzi badala ya kuwekeza kwenye mambo muhimu ya maisha.Na hakutaka kuficha imani yake kwamba watu wengi wakipata fedha wanawekeza kwenye uzinzi.Akaendelea kusema anawafahamu watu kadhaa waliofilisi mashirika ya umma ambao fedha zao ziliishia kwa wao kuongeza idadi ya nyumba ndogo.Wakati mwingine unaweza kusema kuwa kwa baadhi ya watu umasikini au kipato cha kawaida ni sawa na neema kwao kwani wakazifuma inakuwa shida.Utadhani ni kosa la jinai kwa mtu kuwa na mafedha bila kuwa na mwanamke zaidi ya mmoja.

Ndio maana majambazi wa uchumi wetu huwa hawadumu sana baada ya kustaafu au kustaafishwa.Wanakuwa na majukumu mengi-sio ya kibiashara au kidini-kuhakikisha nyumba ndogo zao hazikati kamba na pengine kuhudumia timu za watoto wa nje walipatikana wakati wanafilisi nchi yetu.Na sio kwa vibosile tu,hata kwa vijana ambao katika mahesabu yasiyotabirika kimaisha wanalala masikini na kuamka matajiri.Utakuta,kwa mfano,msanii ambaye anatoka familia masikini kabisa anafanikiwa kujitoa katika umasikini kwa kipaji cha muziki.Akipata malipo ya kazi yake ya sanaa anataka dunia imtambue.Basi warembo watabadilishwa mara nyingi zaidi ya anavyobadili nguo zake.

Huu mtindo wa kuwekeza kwenye ngono utawamaliza wengi.Ukimwi upo na hakuna dalili za tiba hivi karibuni.Kujidanganya kwamba kuna zana au hizo dawa za kurefusha maisha ni upuuzi.Sawa,dawa zipo lakini ukichanganya na maisha mabovu ya anasa na kuendeleza ngono kutumia dawa hizo ni sawa na kujaribu kubadili ladha ya bahari kwa kijiko kimoja cha sukari.
Hasemwi mtu mmoja hapa.Wanaosemwa ni wazinzi wote na wale ambao pamoja na nafasi zao muhimu katika jamii wanashindwa kusimama imara kuendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi kwa vile wao wenyewe wanaendekeza ngono kupindukia.

Habari njema ni kwamba kwa wale ambao bado hawajaanza rasmi kujikinga na kushiriki kuudhibiti Ukimwi muda bado upo japo unakwisha kwa mwendo wa shaa.Kwa waliooa au kuolewa ni vema wakatambua kuwa wana jukumu kubwa la kuwatunza wenza wao kwa kuwa waaminifu,na kutambua kuwa vifo vyao vitaacha wajane na yatima.Kwa wale wanaoendekeza kuwekeza kipato chao kwenye ngono nawashauri watambue kuwa kuna mabenki na sehemu kadhaa za kutumbukiza fedha hizo na matokeo yake hayatakuwa homa za mara kwa mara bali kupata riba na kujiendeleza kimaisha.Na kwa mashetani wanaowatumia waathirika wa Ukimwi kwa ajili ya kujinufaisha wao wenyewe,nawaomba wafahamu kuwa hawana tofauti na wale wanaoambukiza ugonjwa huo kwa makusudi.Fedha wanazopewa na wafadhili zinahitajika sana kutufikisha walipofika wenzetu wa Uganda.Bila dhamira ya dhati,Ukimwi utaendelea kuliathiri Taifa letu.

Alamsiki.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.