13 Nov 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-26

Asalam aleykum,

Hapa ni shwari japokuwa usafiri wa anga umekuwa ni kama adhabu vile tangu zipatikane taarifa kwamba kuna kundi la watu lililokuwa linapanga kulipua ndege kadhaa.Huwezi kuzilaumu taasisi zinazohusika na usafiri na usalama kwa kuchukua hatua ambazo kwa namna flani ni kama bughudha kwa wasafiri kwa vile pindi wakizembea kidogo tu basi kuna hatari ya watu kupoteza maisha yao.Wachambuzi wa mambo wanasema wakati magaidi wanahitaji kosa moja tu kutimiza azma yao vyombo vya usalama vinahitaji kila sekunde kuwa makini kuwazuia magaidi kutekeleza azma yao.

Ni kutokana na kuongezeka kwa matishio ya mashambulizi ya kigaidi shirika la ujasusi la Uingereza (MI6) lililazimika hivi karibuni kuvunja mwiko wake na kutangaza hadharani nafasi za kazi za ushushushu.MI6 ilikiri kwamba inahitaji nguvukazi zaidi ili kuweza kumudu kwa ufanisi zaidi majukumu iliyonayo ya kuilinda nchi hii.Kabla ya hapo shirika hilo lilikuwa na njia zake za siri za kuajiri watumishi wake.Pamoja na MI6 ambayo kimsingi kazi yake kubwa ni kuzuia matishio ya kutoka nje ya nchi,patna wake MI5,shirika la ushushushu wa ndani,kwa pamoja wameanza kujitokeza hadharani zaidi ili kupata sapoti ya wananchi ambao kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani huyaangalia mashirika kama hayo kwa wasiwasi na uoga.Sababu kuu ni kwamba wengi hawajui umuhimu wa taasisi hizo muhimu kwa ustawi wa taifa lolote lile.Hali ni tofauti kidogo nchini Marekani ambapo mashirika mawili makuu (wana mlolongo wa taasisi za kishushushu) yaani FBI na CIA yamekuwa wazi kwa kiasi flani ukilinganisha na katika nchi nyingine.

Huko nyumbani,hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua Bwana Rashid Othman kuwa Mkuu mpya wa Idara ya Usalama wa Taifa.Kwa baadhi ya sie tuliopo Uingereza tunamfahamu Mheshimiwa huyo kwa vile alikuwa mwambata kwenye Ubalozi wetu wa London,na Watanzania wengi hapa wameupokea uteuzi wake kwa furaha kwa vile alikuwa mchapakazi na mtu wa karibu kwa wengi.Kingine kilichowagusa wengi ni kauli yake kwamba atakuwa anakutana na waandishi wa habari kubadilishana nao mawazo sambamba na mkwara aliowachimbia majambazi.Baadhi ya vyombo vya habari viliporipoti uteuzi na kuapishwa kwa Bwana Othman vilionyesha kukunwa na dhamira ya kiongozi huyo na taasisi yake kuwa karibu zaidi na wananchi katika harakati za kukabiliana na maovu katika nchi yetu.
Wengi wetu tumekuwa na hisia potofu sana kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa.Siku za nyuma wapo waliokuwa wanaamini kuwa maofisa usalama ni watu waliokuwa wakuenda baa kuhesabu visoda vya bia kuwatambua watu wanaotanua (wanaotumia fedha pengine zaidi ya kawaida).Wapo pia wale waliokuwa wanadai kuwa mashushushu ni wanyonya damu (sijui hiyo damu ilikuwa inapelekwa Muhimbili au wapi).Baadhi ya wanaozijua ofisi za taasisi hiyo wamekuwa wanaogopa hata kuziangalia utadhani wakifanya hivyo watapigwa risasi.Kwa kifupi,japokuwa taasisi hiyo ni ya Kitanzania na watumishi wake ni Watanzania wenzetu imekuwa ikichukuliwa kama imetoka nje ya dunia.

Kiutamaduni,taasisi za usalama zinafanya kazi zake kwa siri.Na ni kwa usiri wa aina hiyo ndio unasikia MI6 na wenzake wanaweza kuokoa maisha ya watu waliokuwa wanapanga kulipua ndege pamoja na matukio mengine ambayo laiti yangetokea basi mamia na pengine maelfu ya watu wangepoteza maisha yao.Wapo wanaosema kwamba wakati wa mapambano dhidi ya ukaburu huko bondeni (Afrika Kusini),makaburu walitaka sana kuihujumu Tanzania hasa kutokana na mchango wake katika mapambano hayo lakini Idara ya Usalama wa Taifa ilisimama kidete kukabiliana nao hadi mwisho.Inasemekana pia kwamba japo wengi tunaamini kwamba Watanzania ni watu wa amani kwa asili,mchango wa taasisi hiyo katika kuiweka nchi yetu kuwa kisiwa cha amani ni mkubwa sana.Wachambuzi wa mambo ya usalama wa kimataifa wanabainisha kuwa utulivu katika nchi ni kigezo muhimu cha ufanisi wa idara yake ya usalama wa taifa.

Itakuwa tunawaonea tukiwalaumu wale wanaodhani mashushushu ni wanyonya damu au wale wanaoogopa kuzitazama ofisi au magari ya idara hiyo utadhani wakifanya hivyo watapigwa na radi.Wanapatwa na hisia hizo kwa vile hawajui kinachofanywa na taasisi hiyo.Hatuwezi pia kuilamu idara hiyo kwa kuwaacha watu waiogope kwa vile kazi ya kubadilisha mawazo ya watu inaweza kuchukua karne nzima na pengine bila mafanikio.Hata huko Marekani ambako taasisi kama CIA na FBI ziko wazi kiasi haimaanishi kuwa watu hawana mawazo ya ajabuajabu dhidi ya taasisi hizo.La muhimu hapa sio nani alaumiwe au kuwa na uoga ni kosa au dhambi.La muhimu ni mahusiano bora kati ya taasisi hiyo na wananchi.Wengi wetu tunawaogopa polisi lakini tunapopata matatizo tunakwenda kwenye vituo vya polisi.Pengine badala ya kuendelea na uoga wananchi wanapaswa kuzisaidia taasisi zinazowalinda.Kinachohitajika ni utaratibu tu wa namna mchango wa wananchi wa kawaida unaweza kuwasilishwa.
Yayumkinika kusema kwamba wananchi wengi wana imani kubwa na taasisi hiyo nyeti.Nasema hivyo kwa sababu pindi Rais Kikwete alipotangaza kuwa vita dhidi ya rushwa na ujambazi itaijumuisha pia Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba watu wanaweza kupeleka majina ya watuhumiwa kwenye ofisi za taasisi hiyo wananchi wengi walipata imani kuwa sasa mafaniko yanaweza kupatikana hata kama itachukua muda kidogo.Kama alivyosema Bwana Othman baada ya kuapishwa,wananchi wa kawaida wana mchango mkubwa katika ustawi na usalama wa nchi yetu hasa kwa vile wale wanaotunyima usingizi (majambazi),wanaogeuza ndugu zetu kuwa mazezeta na nusu-wafu (wauza unga),wanaokwamisha maendeleo yetu na kuminya haki zetu (wabadhirifu na wala rushwa) ni watu tunaoishi nao.Ni dhahiri basi kwamba ushirikiano kati ya wananchi na taasisi za usalama ni wa manufaa makubwa kwa kila mmoja wetu.

Alamsiki.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.