26 Nov 2007

MTANZANIA UGHAIBUNI-4

Miongoni mwa matatizo yanayowakabili wageni na wahamiaji katika nchi mbalimbali ni suala la ubaguzi.Ubaguzi wa aina yoyote ni mbaya,uwe wa rangi,dini,jinsia au maumbile.Ubaguzi unaosumbua zaidi barani Ulaya na nchi nyingine za Magharibi ni ubaguzi wa rangi,na waathirika wakubwa ni sie wenye ngozi nyeusi.Na ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi unavuka mipaka ya uenyeji wa huyo anayebaguliwa kwani hata Weusi ambao wamezaliwa katika nchi husika nao hukumbana na vitendo vya ubaguzi kama vile tunavyokumbana navyo sie wageni.

Kuna rafiki yangu mmoja Mwamerika Mweusi aliwahi kuniuliza kuhusu tatizo la ubaguzi kwa hapa Scotland.Nikawa mkweli kwake kwa kumfahamisha kwamba ubaguzi upo japo sio wa wazi sana,na kuna nyakati sio rahisi kubaini kwamba umebaguliwa hadi uchunguze kwa makini.Akanipa “matumaini” kwa kuniambia kuwa nisijali sana hasa kwa vile mie ni mgeni hapa,na kwamba hata yeye huwa anakumbana na ubaguzi huko Marekani,nchi aliyozaliwa na kukulia yeye na vizazi vyake kadhaa vilivyomtangulia.Alikwenda mbali zaidi na kunijulisha kwamba yeye binafsi huwa anakumbana na “ubaguzi wa aina nyingine” pia.Rafiki yangu huyo ni mzaliwa na jimbo la South Carolina liloko kusini mwa Marekani.Kwa maelezo yake mwenyewe,lafidhi ya Wamarekani wenya asili ya kusini mwa nchi hiyo ni tofauti na wale wanaotaka maeneo mengine.Alieleza kuwa kuna wakati huwa anagundua kwamba baadhi ya watu anaoongea nao “wanamsanifu” kutokana na lafidhi yake.Lakini kama hiyo hazitoshi,rafiki yangu huyo ni mfupi (kwa maana halisi ya neno hilo,japo sio “mbilikimo”).Alidai kuwa kuna nyakati huwa anakutana na watu wanaoelekea kufanya ufupi wake kama kichekesho flani.

Kwa hapa barani Ulaya,ubaguzi wa rangi unaweza kuonekana unaongezeka kwa kasi kutokana na kukua kwa siasa za mrengo mkali wa kulia (far-right politics) hasa kuanzia miaka ya 90.Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema kwamba kukua kwa siasa hizo ni matokeo ya kushindwa kwa serikali zilizoundwa na vyama vya mrengo wa kushoto (au kati) kukidhi matarajio ya wanaoongozwa (wananchi).Linapotokea suala la ukosefu wa ajira, “majeruhi” wa kwanza kulaumiwa watakuwa wageni/wahamiaji,kuongezeka kwa uhalifu nako kunahusishwa na wageni hata pale ambapo takwimu za uhalifu hazionyeshi hivyo,na ukosefu wa makazi pia huhusishwa na wingi wa wageni katika miji husika licha ya ukweli kwamba sera nyingi za makazi hutoa kipaumbele kwa wazawa kuliko wageni.Yayumkinika kusema kuwa wageni wamegeuzwa kuwa jalala la lawama kwa takriban kila baya linalotokea katika nchi hizi.

Kwa haraka haraka,kuna takriban vyama vya siasa 11 ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vichochezi vikubwa vya ubaguzi wa rangi barani Ulaya.Vyama hivyo ni pamoja na BNP (British National Party) cha Uingereza,ambacho japo hakijawa na mafanikio makubwa ya kisiasa,kinaendelea na jitihada za kukusanya wafuasi.Vyama vingine ni Freedom Party (FPO) cha Austria ambacho kina wafuasi wengi kusini mwa nchi hiyo,Flemish Block (VB) cha Ubelgiji chenye viti 15 katika bunge dogo la nchi hiyo,na huko Denmark ni chama cha DPP (Danish People’s Party) ambacho pamoja na mambo mengine kimekuwa kikiishinikiza serikali ya mseto ya nchi hiyo kupunguza misaada kwa nchi masikini.Pamoja na kutopata matokeo mazuri kwenye uchaguzi uliopita nchini Ufaransa,Jean-Marie Le Pen na chama chake cha National Front (FN) ameendelea kuwa miongoni mwa vielelezo rahisi vya namna siasa za mrengo mkali wa kulia zinavyoshamiri barani Ulaya.Le Pen aliwashangaza wapenzi wengi wa soka duniani wakati wa michuano iliyopita ya kombe la dunia pale alipodai kuwa ni vema timu ya taifa ya soka ya nchi hiyo ikatolewa mapema kwani haiwakilishi Ufaransa kwa vile imejaa wachezaji weusi.Vyama vingine “hatari” ni pamoja na LPF cha Uholanzi,Progress Party cha Norway,Popular Party cha Ureno,na Swiss People’s Party (SVP) chenye uwakilishi mkubwa zaidi bungeni na ambacho kimetamka bayana kuwa watu weusi wanapaswa kutimuliwa nchini humo eti kwa vile “wao ndio chanzo cha uhalifu”.Huko Ujerumani,vyama vya Republican Party (REP),German People’s Union (DVU),na National Democratic Party (NPD) vimekuwa kama mwendelezo wa siasa za ki-Nazi ambapo wanachama wake wanasifika zaidi kwa uhuni,vurugu na chuki yao ya wazi dhidi ya wageni na wahamiaji.Lakini matatizo nchini Ujerumani hayaishii kwenye vyama hivyo vya ki-Nazi pekee kwani kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Foxnews cha Marekani,asilimia 25 ya Wajerumani wote (wengi wao wakiwa wenye umri wa miaka 60 na zaidi) wana mtizamo chanya (positive view) kuhusu sera za kibaguzi za ki-Nazi,na wanauona unyama wa Hitler ulikuwa sahihi.

Kama ilivyo nchini Ujerumani ambako vyama vya mrengo mkali wa kulia vinaelekea kurithi siasa za kinyama za ki-Nazi,nchini Italia nako vyama “hatari” vya National Alliance na Northern League vina sera za ajabu kabisa ikiwa ni pamoja na wazo lao la kuanzishwa kwa kikosi cha askari wa majini (coast guard) kitachokuwa na jukumu la kuwapiga risasi wageni wote wanaoingiza nchini humo kwa kuzamia.Pia vyama hivyo vyenye mrengo wa kifashisti vinapinga kwa nguvu Muungano wa nchi za Ulaya (EU) huku madai yao yakiwa eti EU inaongozwa na wanaopenda kufanya ngono na watoto (pedophiles).Angalau kidogo nchini Uholanzi,chama cha Pim Fortuyn’s List (PFL),licha ya msimamo wake mkali dhidi ya wahamiaji na wageni,kimekuwa na viongozi wanaotoka katika makundi ya kijamii ambayo kimsingi ni “maadui wa asili” wa siasa za mrengo wa kulia,kwa mfano watu weusi,mashoga,nk.Mwanzilishi wa chama hicho,Pim Fortuyn alikuwa shoga asiyejificha (openly gay) na naibu wake Joao Varela alikuwa Mholanzi mhamiaji Mweusi.Fortuyn ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi alianzisha PFL baada ya kutimuliwa kwenye chama kingine cha mrengo wa kulia nchini humo cha Liveable Netherlands kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya wageni na wahamiaji.

Hivyo ndivyo siasa za ubaguzi zinavyoshika kasi huku ughaibuni.Ninapoichambua hali hii najikuta nashindwa kujizuia kujadili “sekeseke” linalotengenezwa huko nyumbani kuhusu suala la uanzishwaji wa mahakama ya Kadhi.Nikiwa kama mwanafunzi ninayefanya utafiti ambao kwa namna flani unahusu mahusiano kati ya siasa na dini kwa huko nyumbani,naomba kusema kuwa pamoja na mazuri yote ambayo jamii inanufaika kutokana na dini,kuna tatizo moja la msingi ambalo pia linaweza kusababishwa na dini ambalo ni ubaguzi.Pengine ni vema kukumbusha pia kwamba kukua kwa siasa za ubaguzi katika nchi mbalimbali kumeambatana na baadhi ya “wazawa” kuwaangalia waumini wa dini nyingine,hususan zile za wageni na wahamiaji,kuwa “hazifai”.Tunaweza kukubaliana kuhusu kitu kimoja kwamba mara nyingi msingi wa imani wa dini moja ni kuwa dini hiyo iko bora zaidi ya dini nyingine,au pengine Mungu wa dini hiyo ndio Mungu halisi kuliko wa dini nyingine.

Mjadala kuhusu suala la mahakama ya kadhi unapaswa kufanywa kwa umakini sana hasa kwa vile ni suala nyeti na linalogusa hisia za kidini.Nadhani kuna mambo mawili matatu yanayopaswa kufanyiwa kazi mapema.Kwa upande mmoja ni kwa mamlaka husika kulishughulikia suala hili kwa uwazi na kwa kuzingatia maslahi ya pande zote husika.Nadhani badala ya kukaa kimya au kuendeleza ahadi kwamba “suala hili linashughulikiwa na litapatiwa ufumbuzi hivi karibuni” ni vema maamuzi kuhusu suala hilo yakatolewa mapema ili pamoja na mambo mengine kuzuia uwezekano wa kuzuka chokochoko za hapa na pale kutoka kwa makundi mbalimbali katika jamii.Kama maamuzi hayo yanaweza kutolewa na watengeneza sera pekee basi na yafanywe mapema lakini kwa umakini,na kama maamuzi yatapaswa kutolewa kwa njia ya maoni ya wananchi basi na iitishwe kura ya maoni mapema kadri iwezekanavyo.Kwa upande mwingine ni subira inayohitajika miongoni mwa makundi mbalimbali katika jamii.Izingatiwe kwamba katika masuala yanayogusa imani ya mtu,kauli zinazoonekana za kawaida tu lakini zenye maana tofauti kwa waumini wa dini tofauti na ya mtoa kauli hizo,zinaweza kupelekea uvunjifu wa amani na hata kuitumbukiza nchi kwenye machafuko ya kidini.Ni jukumu letu sote kukubushana kwamba wakati inachukua miongo kadhaa,kama sio karne,kujenga amani,kuipoteza ni suala la wiki chache tu,kama sio siku kadhaa.Tusiruhusu tofauti zetu za mitazamo ziwe chanzo cha kutupiana makonde,na kwa hakika tunaweza kabisa kupingana ki-hoja pasipo kutishiana amani.

IFUATAYO NI MAKALA NYINGINE

KULIKONI UGHAIBUNI-86


Asalam aleykum,

Moja ya mambo nayopendelea kufanya pindi muda unaporuhusu ni kuangalia runinga.Lakini naweza kusema kwa kujiamini kabisa kwamba mahaba yangu kwa runinga yamekuwa ni sawa na mithili ya kuingia darasani kwani ni nadra kwangu kupitisha siku nzima pasipo kujifunza kitu kipya kwenye runinga.Hiyo haimaanishi kwamba kila kipindi nachoangalia kina jambo jipya au la maana,bali najitahidi kuwa makini katika uchaguzi wa kile nachoangalia.Halafu nimejenga desturi ya kuangalia runinga huku laptop yangu ikiwa pembeni.Hiyo huwa inanirahisishia kufanya “reference” ya kitu nachokiona kwenye runinga lakini pengine hakijafafanuliwa vizuri.Inapotokea hivyo basi huwa naingiza neno husika kwenye mtambo wa kusaka habari kwenye mtandao ujulikanao kama “Google” au nakimbilia kwenye tovuti nyingine maarufu kwa maelezo ya watu na vitu ijulikanayo kama “Wikipedia”.

Kitu kimoja nilichojifunza kuhusu vipindi vya televisheni hapa Uingereza ni namna mashindano ya kupata watazamaji yalivyo juu.Kutokana na mashindano hayo,vituo vya televisheni hujitahidi kuja na ubunifu wa kila namna,wa maana na wa kipuuzi.Na miongoni mwa ubunifu huo ni hivi vipindi vinavyojulikana kama “reality tv” ambavyo kwa tafsiri isiyo rasmi ni vipindi vinavyoonyesha maisha katika uhalisi wake.Sintoingia kwa undani sana kuelezea maana ya vipindi vya namna hiyo kwani nilishawahi kuviongelea katika makala yangu moja huko nyuma.Ila kwa kukumbushia tu,katika makala hiyo nilizungumzia mbinde iliyojitokeza kwenye kipindi cha “celebrity big brother”,yaani “Big Brother” kama hiyo aloshinda Richard lakini wahusika wake wanakuwa “watu wenye majina” (celebrities).Hiyo ni “version” (aina) tofauti ya “Big Brother” ya kawaida ambayo kwa mwaka huu iliweka historia ya kupata mshindi Mweusi,Brian,Mwingereza mwenye asili ya Nigeria.Katika “Celebrity Big Brother” iliyopita kulizuka migogoro wa ubaguzi wa rangi dhidi ya stta wa filamu za Kihindi,Shilpa Shetty,ambapo washiriki watatu wakiongozwa na mshindi wa zamani wa “Big Brother” (ya kawaida) Jade Goody,walitoa matamshi kadhaa yaliyoashiria ubaguzi wa rangi.Zilipigwa kelele nyingi sana na nusura mashindano hayo yavunjike kabla ya muda wake,lakini yalifanikiwa kumalizika salama ambapo Shilpa aliibuka mshindi.Sokomoko hilo lilifika hadi bungeni na wakati flani Gordon Brown (Waziri Mkuu wa sasa) akiwa ziarani nchini India alilazimika “kuwaomba radhi” Wahindi kwamba yaliyomkuta Shilpa katika jumba la “Big Brother” sio taswira halisi ya jamii ya Waingereza.

Sokomoko la ubaguzi wa rangi katika kipindi hicho lilipelekea baadhi ya watu kuhoji umuhimu wa vipindi vya namna hiyo na faida yake kwa jamii.Lakini pia lilizua swali moja la msingi,je panapojitokeza vipindi vya kipuuzi namna hiyo wa kulaumiwa ni nani?Waandaaji au watazamaji?Kwamba kama waandaaji watakuwa makini basi ni dhahiri hakutakuwa na upuuzi katika vipindi wanavyoandaa.Lakini pia iwapo kipindi kitaonekana cha kipuuzi basi watazamaji wanaweza kukisusia hivyo kuwalazimisha waandaaji kukirekebisha au kukiondoa kabisa hewani.Ikumbukwe kwamba kwa nchi za Magharibi,vyombo vya habari vinahangaika sana kupata “ratings” nzuri,yaani idadi kubwa ya watazamaji au wasomaji.Wapo wanaodhani kuwa “ratings” zimekuwa zikichochea sana vyombo vya habari kukurupuka na habari zenye utata au za kusababisha mgongano kwani sote twafahamu kuwa “mbwa kung’ata mtu sio habari lakini mtu kung’ata mbwa ni zaidi ya habari”.Yaani kwa kifupi,utata “unalipa sana” kwenye habari.

Nije kwenye “Big Brother” ya akina Richard.Binafsi sikuwa nafuatilia kwa karibu japo ilipokuwa inaelekea ukiongoni nilijikuta natamani Mtanzania mwenzetu Richard ashinde.Lakini tukiwa wakweli na waadilifu,tunaweza kweli kujibu kwa uhakika nini cha msingi tulichojifunza kutokana na mashindano hayo?Hivi kuna lolote la maana la kujifunza pale mshiriki mmoja anapolewa chakari na kuishia kufanya tendo la ndoa huku anafahamu bayana kuwa kamera zinarekodi tukio hilo laivu?Naamini kuna wenzangu wengi tu ambao “Big Brother” kwao ina umuhimu mdogo kuliko hata vichekesho vya kikundi cha “Ze Comedy” ambavyo kwa kiasi flani vinafikisha ujumbe muhimu katika namna ya kuvunja mbavu.Sina tatizo na ushindi wa Richard,ila tatizo langu ni mantiki nzima ya “Big Brother”.

Lakini kama nilivyosema awali kuwa “mtu akimng’ata mbwa inakuwa zaidi ya habari”.Pengine laiti “Big Brother” ikiondoa “manjonjo” ya ngono za hadharani na uchafu mwingine inaweza kupoteza umaarufu na si ajabu ikafutiliwa mbali baada ya muda mfupi.Nadhani vimbwanga vinavofanyika kwenye jumba hilo vinachangia sana kuongeza umaarufu wa kipindi hicho.Kwa bahati mbaya,vimbwanga hivyo havina umuhimu wowote,sio kwa washiriki pekee bali hata kwa watazamaji.Pia nadhani ngono ndani ya jumba la “Big Brother” inaweza kufunua unafiki wa namna flani wa wenye majukumu ya kulinda maadili ya jamii yetu.Nilisoma mahala flani habari kwamba video ya wimbo “Simama Tucheze” wa Q-Chief imepigwa stop kuonyeshwa katika vituo vya runinga kwa vile imejaa vitendo vya ngono.Japo siungi mkono video zenye kuonyesha vitendo vya ngono lakini kinachonifanya niwatolee mimacho “askari wetu wa maadili” ni namna wanavyoweza kufumbia macho matendo ya ngono kwenye jumba la “Big Brother” lakini wanadiriki kumkalia kooni Q-Chief.Na si hapo tu,kama msomaji mpendwa utakuwa msikilizaji wa vipindi vya miziki (hususan vile vya mchana) nadhani utakuwa umeshasikia baadhi ya tungo za muziki wa kufokafoka (hasa wa Marekani) ambazo “hazijachujwa” na hivyo kujumuisha maneno yasiyofaa katika maadili ya jamii yetu.Kwa kawaida na kwa kuzingatia ujumbe uliomo,nyimbo za kufokafoka hutolewa katika “versions” mbalimbali lakini nazozungumzia hapa ni “radio version” (ambapo “maneno machafu” huwa yamefutwa,yamehaririwa-edited-au yameminywa) na “dirty version” (ambapo kila neno linasikika bila kujali “makali” yake).Inawezekana watangazaji wanaopiga “dirty versions” radioni huwa hawajui kinachoongelewa katika nyimbo hizo au wanajua lakini hawajali kwa vile “askari wa maadili” hawana muda wa kufuatilia.

Kabla ya kuandika makala hii nilisoma Sera ya Taifa ya Utamaduni ambayo inaharamisha waziwazi burudani zinazoendana kinyume na maadili ya jamii yetu.Lakini nadhani ufuatiliaji ni mdogo kwani hata video za baadhi ya nyimbo za wakongomani (Wazaire) ni “chafu” mno kuzionyesha kwenye runinga.Na kama unadhani hiyo ni ndogo basi nenda kajionee “ubunifu” wa bendi zetu katika suala zima la unenguaji.Amin nakuambia,namna baadhi ya wanenguaji wanavyocheza ni mithili ya kuangalia filamu ya “X”.Ukilogwa kwenda na mama mkwe kwenye shughuli kama hizo basi unaweza kujikuta unamtaka radhi kwa namna wanenguaji “wanavyojituma”.

“Askari wa maadili” wanakabiliwa na changamoto nyingine kubwa ya kudhibiti watazamaji wenye umri mdogo kwenye shughuli “za watu wazima”.Kwa hapa Uingereza,ili kijana aweze kuingia kwenye ukumbi wa disko ni lazima awe na kitambulisho kinachoonyesha kuwa umri wake unamruhusu kuingia humo.Na hilo ni hata kwenye kununua pombe na sigara.Sheria iko wazi na inasomeka kwenye kila duka kwamba ili mteja anayeonekana kuwa na umri mdogo aweze kuuziwa bidhaa anapaswa kuthibitisha umri wake.Lakini kwa huko nyumbani ni suala la kawaida kumwona mtoto mdogo kabisa akiwa na “michupa kadhaa ya bia” akielekea grosari au baa kwenda kununua bia.Hivi lile zoezi la kuanzisha vitambulisho vya taifa limefikia wapi?Je vitambulisho hivyo vitaonyesha umri wa mwenye kitambulisho?Nadhani mpango huo utakapokamilika basi inaweza kuwa rahisi kwa “askari wa maadili” kuanza kudhibiti watoto na vijana wenye umri mdogo wasiruhusiwe kuingia sehemu zinazoweza “kuwazibua akili” au kuwabana kununua bidhaa kama bia au sigara.

Pengine kabla sijamalizia makala hii utakuwa unajiuliza tangu lini jeshi la polisi limekuwa na kitengo cha “askari wa maadili”.Well, “askari wa maadili” ni pamoja na mamlaka zinahusika na kuhakikisha maadili ya jamii hayavunjwi,kuupuuzwa au kupindwa.Wahusika wengine ni wazazi,kaka,dada,mabaunsa wanaoruhusu watu kuingia disko,wauza maduka na baa,bila kusahau mimi na wewe.

Alamsiki


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube