29 Oct 2008

Wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam, wameamua kufunga mageti ya chuo hicho kuzuia uongozi wa chuo kuingia na kutoka baada ya Menejimenti kutotimiza ahadi ya kuongea nao, kutokana na mgogoro wa kufeli kwa wanafunzi wengi katika mitihani yao. 

Akipitisha azimio la kufunga mageti hayo, Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Ali Mayay, aliwatangazia wanafunzi kuwa magari ya walimu yaliyoko ndani hayatatoka na yaliyoko nje hayataruhusiwa kuingia hadi uongozi wa chuo uzungumze na wanafunzi. 

Makamu Mkuu wa Chuo aliyetajwa kwa jina la A. Ahamed, ndiye aliyeahidi kukutana na wanafunzi hao saa nane mchana, lakini hakutokea hali iliyowakasirisha wanafunzi hao na kuanza kufanya fujo. Awali, wanafunzi hao ambao wamegoma kuingia madarasani, walidai kuwa kiini cha wanafunzi wengi kufelishwa ni mgogoro uliopo baina ya Mkuu wa Chuo na walimu wa CBE. 

Matokeo ya wanafunzi ambayo yametoka hivi karibuni yanaonyesha kuwa matokeo ni mabaya, hali iliyowashtua wanafunzi wanaotaka kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa chuo hicho sababu ya wanafunzi kufeli kiasi hicho. Matokeo hayo ya mitihani yamekuwa mabaya kwa wanafunzi wa jioni waliofanya mitihani ya semista ya tatu pamoja na matokeo ya wanafunzi wanaosoma asubuhi ambao walifanya mitihani ya marudio. 

“Sisi tunaamini kuwa mgogoro uliopo baina ya Mkuu wa Chuo na walimu ndio chanzo cha wanafunzi kufelishwa kiasi hiki na sisi tangu Ijumaa tumeamua kutoingia madarasani hadi tupate maelezo kutoka kwa uongozi wa chuo,” alisema Makamu Rais wa Serikali ya Wanafunzi (Cobeso), Godrey Misso. Alisema hawaingii madarasani hadi watakapopata maelekezo kutoka kwa uongozi wa chuo. 

“Waliahidi kuongea na sisi jana (Jumatatu), lakini ikashindikana, wameahidi leo (jana) tunawasubiri,” alisema. Alisema haijawahi kutokea katika historia ya chuo hicho wanafunzi kufeli kiasi hicho. “Haiwezekani katika darasa la watu 400 wafaulu watu sita, ina maana wanafunzi wengine hawana akili?…hiki ndicho tunachopinga,” alisema. Baadhi ya walimu waliozungumza na gazeti hili, walikiri kuwa Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Wilclif Lugoe tangu ajiunge na chuo hicho miezi 10 iliyopita, amefanya marekebisho ya mfumo wa uendeshaji ambayo yanawaathiri walimu kimapato.

CHANZO: HabariLeo

1 comment:

  1. Hi there I was looking through your blog and I like it, so I would like you to come and visit my blog here in San Diego.

    I want you to come by and enjoy the different labels and music videos I have with the many artistic elements I use in my art blog.

    See you soon :)

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.