12 Nov 2008


VIONGOZI wa Nchi za Maziwa Makuu wamesema ipo haja ya kupeleka majeshi kwa ajili ya kurejesha amani eneo la Kivu lililopo Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako kwa sasa hali ya usalama si shwari kutokana na mapigano yanayoendelea. 

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe ambaye alisema uamuzi huo ulitolewa na viongozi wa nchi hizo na kuungwa mkono na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. 

Alisema hatua hiyo inatokana na hali ya siasa ilivyo Kaskazini Mashariki mwa DRC kuwa mbaya kufuatia mashambulizi yaliyoanzishwa na kundi la waasin wanaoongozwa na Bw. Laurent Nkunda. 

"Mashambulizi hayo yamesababisha athari kubwa kwa wananchi, kiasi cha watu wengi kukimbia makazi yao hivi karibuni. Pamoja na kuwepo makubaliano mengi ya awali, Laurent Nkunda na kundi lake bado hawaheshimu makubaliano hayo," alisema Bw.Membe. 

Alisisitiza kuwa kwa hali ilivyo sasa nchini DRC viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja huo, Rais Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na viongozi wengine kadhaa wamekuwa wamekifanya mikutano ya dharura ili kuona jinsi gani wanaweza kumaliza mapigano yanayoendelea na kurejesha amani. 

Pia alisema maamuzi mengine yaliyotolewa na viongozi hao ni SADC kupeleka haraka wataalamu wa jeshi kusaidia kuangalia mipaka ya DRC na nchi jirani. 

Vile vile SADC iwe na ujumbe katika timu ya upatanishi iliyoanzishwa na wakuu wa nchi za Maziwa Makuu ambapo Rais Mstaafu wa Naijeria, Jenerali Olesegun Obassanjo na Rais Mstaafu wa Tanzania, Bw. Benjamin Mkapa wa Tanzania wamechaguliwa kuwa wajumbe wa timu hiyo. 

Alipoulizwa kuna tofauti gani kati ya Bw. Nkunda na aliyekuwa muasi wa Komoro, Kanali Mohamed Bakar, Bw. Membe alisema hawana tofauti kwa sababu wote ni waasi. 

"Hakuna tofauti kati ya hawa wawili kwani Kanali Bakari aliiasi Serikali yake Nkunda naye ni muasi ndio maana tunamtaka asitishe mapigano na tunakoelekea akiendelea kukaidi kuna hatari ya AU kupeleka majeshi ya kumdhibiti," aliongeza. 

Kuhusu hali ya kiasa nchini Zimbabwe, Bw.Membe alisema bado juhudi za kutafuta suluhu kuhusiana na muskabali wa nchi hiyo unaendelea.

CHANZO: Majira

NI WAKATI WA VITENDO ZAIDI KULIKO MANENO.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.