8 Nov 2008


SERIKALI kwa mara nyingine imeingilia kati na kuamua kulipa mishahara ya wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), baada ya mwekezaji wake kushindwa kulipa mishahara ya mwezi uliopita.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitangaza uamuzi huo bungeni jana, alipokuwa akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mamuya (CCM), aliyetaka kujua mpango wa serikali katika kuhakikisha mwekezaji huyo anaiendesha kampuni hiyo kwa ufanisi na kama alikuwa akijua kuwa hadi jana wafanyakazi wa kampuni hiyo walikuwa hawajalipwa mishahara yao ya mwezi uliopita.

“Serikali imelichukua tena tatizo hilo na tunalifanyia kazi. Ninaahidi kuanzia sasa wafanyakazi hawa hawatakosa tena mishahara, tutajaribu kuona kama hiyo nyongeza tutaweza kuilipa,” alisema Pinda.

Agosti, mwaka huu, tatizo la wafanyakazi kukosa mishahara lilipotokea kwa mara ya kwanza, Waziri Mkuu ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuokoa jahazi na hadi jana na juzi alikuwa akihaha kuhakikisha wafanyakazi hao wanalipwa mishahara yao ya Oktoba.

“Hadi juzi nilikuwa nahangaikia suala hili, ahadi ya serikali ilimalizika Agosti na tulitarajia uongozi wa TRL ungeendelea kulipa viwango vipya vya mishahara kuanzia Oktoba kama tulivyokubaliana, lakini kwa bahati mbaya wameshindwa na tunalazimika tena kulipia mishahara ya wafanyakazi hao hadi Novemba,” alisema Pinda.

Hii ni mara ya tatu kwa serikali kulazimika kuiokoa kampuni hiyo, baada ya uongozi wake kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi.

Miezi mitano tangu mwekezaji alipolichukua shirika hilo wakati huo likiitwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), serikali iliingia mfukoni na kutoa fedha za walipa kodi zaidi ya sh bilioni tatu kuikopesha TRL kwa ajili ya kulipa mishahara ya wafanyakazi.

Septemba, mwaka huu, TRL ilikwama tena kulipia viwango vipya vya mishahara na serikali iliamua kulipa mishahara ya mwezi huo kwa ahadi kwamba kuanzia Oktoba mwekezaji angeweza kuendelea kulipa wafanyakazi wake bila matatizo.

Kampuni hiyo imeshindwa tena kulipa mishahara ya mwezi uliopita. Serikali kwa mara ya tatu sasa inajikuta ikilazimika kuingia tena mfukoni kuokoa jahazi.

Juzi wafanyakazi wa TRL walitangaza kuanza mgomo baridi, huku wakisubiri hatua zinazochukuliwa na mwekezaji kuikoa kampuni hiyo. Mbali na sula la TRL, Waziri Pinda pia alizungumzia suala la kuvuja kwa mitihani aliposema serikali inaliangalia kwa umakini Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kwani ndipo penye tatizo.

Serikali inajitahidi kuangalia namna bora ya kulisimamia kwani ni aibu kwa taifa kukaa na kuulizana maswali juu ya uvujaji wa mitihani. Amewataka wazazi na wanafunzi wanaotafuta mitihani kuacha kuendekeza tabia hiyo ya aibu.

“Natoa rai kwa wazazi kuwa tusikubali na tuwe wa kwanza kutoa taarifa tunapoona watoto wana mitihani ya kununua,” alisema Pinda.

Jibu hilo la Waziri Pinda lilitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya (CUF), aliyetaka kujua mpango wa serikali katika kukabiliana na tatizo la kuvuja kwa mitihani na uchapishaji wa vyeti feki vinavyosambazwa mashuleni na kusababisha kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

Akizungumzia hali ya kiuendeshaji ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Pinda alikiri kwamba kwa sasa kampuni hiyo iko taabani, hali iliyosababisha serikali ilazimike kufanya mazungumzo na shirika moja nchini China, lengo likiwa ni kuinusuru ATCL katika hali hiyo mbaya.

Akijibu swali la Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, aliyeitaka serikali ichukue jukumu la kununua vitabu vya kiada kwa shule za msingi na sekondari na kuvisambaza badala ya jukumu la sasa la kutumia wakandarasi, Waziri Pinda alisema utaratibu wa sasa ni kwamba serikali inatoa fedha kwa halmashauri, nazo zinatumia wakandarasi ambao wengine si waaminifu.

“Wakandarasi mara nyingine hununua vitabu vya mitaani vinavyokuwa katika kiwango cha chini, hivyo tumekubaliana na wizara tutafute utaratibu mzuri wa upatikanaji wa vitabu,” alisema.


CHANZO: Tanzania Daima

KUMWOKOA MWEKEZAJI KILA ANAPOKWAMA SIO UFUMBUZI,BALI UAHIRISHAJI WA UFUMBUZI,WA TATIZO.NI MUHIMU KUJIULIZA HUYU MWEKEZAJI ATAENDELEA KUOKOLEWA HADI LINI,AND WHAT'D HAPPEN IF HATOOKOLEWA!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.