9 Nov 2008


UTATA umegubika mchakato wa zabuni nyeti ya matengenezo ya mfumo wa usalama ndani ya Benki Kuu Tanzania (BoT), ambayo imetolewa kwa Kampuni ya Siemens ya Afrika Kusini.

Kuibuka kwa utata huo kumekuja wakati Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu akiwa katika mipango ya kuisafisha benki hiyo na tuhuma mbalimbali, ikiwemo ya ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Nyaraka ambazo gazeti hili inazo, zinaonyesha utata huo umeibuka kutokana na malalamiko kutoka kwa Kampuni ya ESS ya Afrika Kusini, ambayo haijaridhishwa na taratibu za mchakato zilivyofanyika.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, ESS inaonekana kulalamikia hatua ambayo imeita kuwa ni kuwepo mawasiliano kabla, kati ya watendaji wa Siemens na baadhi ya watu ndani ya Bodi ya Zabuni ya BoT.

Mawasiliano hayo yalinaswa katika barua pepe kati ya mwakilishi wa Simens nchini Julai 29,2008, akifahamisha viongozi wake kufanya mawasiliano na mtu mmoja muhimu ndani ya BoT.

Sehemu ya barua hiyo inasomeka, " Nimeweza kuzungumza na mtu mmoja wa kuaminika ndani ya BoT, na amesema zipo zabuni mbili tofauti, ila sisi tutapatiwa moja tu ya utengenezaji mfumo wa usalama."

Barua hiyo, iliandikwa Julai wakati mshindi wa zabuni alipatikana Oktoba 28, ambapo ESS kama mmoja wa washiriki, alifahamishwa.

Utata mwingine katika zabuni hiyo unatokana na kile kinachoelezwa kwamba, Siemens ilishiriki katika uwekaji mfumo huo katika ujenzi wa jengo la ghorofa 18 maarufu kama Twin Towers na lile la Gulioni Zanzibar, ambayo yanachunguzwa.

"Sasa ikitokea ukaguzi wa Twin Towers umeonyesha kulitumika mabilioni bila kuangalia Value for money (thamani ya pesa kwa kitu), itakuaje?" kilihoji chanzo kimoja.

Siemens katika mkataba huo wa miaka miwili iliomba zabuni kwa sh 3.4 bilioni, hata hivyo, makampuni mengine kwa mujibu wa nyaraka za BoT yako juu zaidi.

Hata hivyo, akizungumzia utata huo ofisini kwake jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Gavana Ndulu, alisema hadi sasa ana imani kwamba, mchakato wa zabuni hiyo ulifuata taratibu husika.

Kwa mujibu wa Profesa Ndulu iwapo atabaini kuna tatizo lolote ikiwemo ukiukwaji wa mkataba huo hatasita kuisitisha.

Profesa Ndulu alisema dai la kwamba Siemens ilijenga Twin Towers ni kweli, lakini akabainisha kuwa hata kampuni nyingine ambayo ni pamoja na ESS na Group 5, pia zilishiriki katika ujenzi huo na pia ziliomba zabuni hiyo.

Profesa Ndulu alisema kabla ya kushirikisha kampuni hizo tatu ambazo zote zilishiriki katika uwekaji wa mfumo wa usalama kwa ngazi tofauti, ilibidi bodi itafute mwongozo kutoka Mamlaka ya Zabuni (PPRA), ambayo ilithibitisha hakuna tatizo.

Mwananchi Jumapili ilifanikiwa kuona nakala ya baraka za PPRA kwa BoT, ikieleza kuwa hakuna matatizo kwa makampuni hayo kushiriki ili mradi vigezo vizingatiwe.

"Najibu moja baada ya jingine, unanijua sifichi kitu na sipendi kupindisha mambo, kuhusu Siemens kushiriki katika Twin Towers, ni kweli, lakini hata ESS na Group 5 walishiriki kwa ngazi tofauti, Group 5 ndiyo wanaojenga jengo hilo, lakini pia wameshiriki," alisema Profesa Ndulu na kuongeza;

"Kama ni kigezo hicho, tusingeruhusu hata ESS na Group 5, kampuni hizi mbili na Siemens zote zimeshiriki katika Twin Towers, ndiyo maana kabla ya zabuni tukaenda PPRA kupata ufafanuzi, wakaruhusu," alisema.

Akifafanua kuwepo mawasiliano kati ya watu ndani ya bodi na Siemens, alisema hadi sasa hajaona tatizo kwani ni kweli zabuni zilikuwa mbili, lakini BoT ikaamua yenyewe kuchukua kazi moja ya kushughulikia uendeshaji wa mambo mbalimbali na kuacha hilo la ukaratabati mfumo wa usalama.

"Ni kweli, zabuni zilikuwa mbili, tulipoona wenyewe tunayo idara ya kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo usafi na ununuzi wa vifaa, tukaamua tuipunguzie gharama kwa benki kwa kuipa zabuni kampuni moja, lakini pia si kwamba tunamwachia peke yake, wapo vijana wetu mahiri wanashirikiana nao," alifafanua.

Profesa Ndulu alisema hajaona tatizo katika hatua hiyo kwani zabuni ilitangazwa Juni na mawasiliano yamefanyika Julai, huo ni utaratibu wa kawaida kwa sababu kuna vitu ambavyo kampuni zote zinapaswa kuelezwa baada ya zabuni kufunguliwa.

"Sasa kusema kwamba zabuni ambayo itatolewa kwa ajili ya kugombaniwa ni ya usalama si uendeshaji, si tatizo ndicho tulichoeleza kwa kampuni zote," alifafanua.

Profesa Ndulu alisema ingawa haingii wala kuruhusiwa kuingilia mambo ya zabuni, lakini amekuwa akiuliza na kupatiwa taarifa za mara kwa mara kwa lengo la kuangalia utaratibu wa kutekelezwa kwa kuzingatia taratibu za kisheria.

"Mimi sitaki watu wapindishe mambo hata kidogo, nitasimamia sheria na kanuni, ndiyo maana huwa wakati mwingine nataka ufafanuzi wa mambo mbalimbali," alisisitiza Gavana Ndulu.

BoT katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 imekuwa na matatizo mbalimbali, ambayo hata hivyo, chini ya uongozi wa Profesa Ndulu amekuwa akijaribu kuisafisha na tuhuma hizo.

Baadhi ya mambo aliyoahidi kuyashughulikia ni kuchunguza mchakato wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo jijini Dar es Salaam na lililoko Zanzibar, kupitia ajira za watumishi wa BoT ambaye ametekeleza kwa kiasi kikubwa.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.