21 Apr 2009

Shule ya Sekondari ya kutwa ya Marambo yenye wanafunzi 253 ya kidato cha Kwanza hadi cha Nne , iliyopo Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi ina mwalimu mmoja. Mkuu wa shule hiyo, Saidi Mbutuka ndiye pekee aliye shuleni hapo anayelazimika kushika nyadhifa zote.

Mbutuka aliliambia gazeti hili kuwa hali hiyo inatishia mustakabali wa elimu kwa wanafunzi shuleni hapo kwa kukosa elimu inayostahili. ''Mimi ndiye mkuu wa shule, ndiye mwalimu wa zamu, mwalimu wa taaluma, kila siku za kazi natakiwa kuingia katika madarasa yote manne, kwa siku ninakuwa na vipindi zaidi ya 10'', alisema.

Aliongeza, ''kwa hali hiyo hata kama ningekuwa mwalimu mzuri, kuna kila sababu ya kutilia mashaka na ubora wa elimu, mimi ni mwalimu wa masomo ya Sanaa, lakini nalazimika kufundisha Sayansi,'' alisema Mbutuka.

Alifafanua kuwa tatizo hilo limejitokeza mwaka huu baada ya walimu wanne waliokuwa shuleni hapo kwenda kusoma. 'Tunao wanafunzi wa kidato cha Nne ambao wanahitaji wafanye mtihani wa kuhitimu elimu yao, hivi tujiulize nini watavuna wanafunzi hawa kwa kufundishwa na mwalimu mmoja ambaye pia ndiyo nguzo kwa wanafunzi wa vidato vingine,'' alihoji.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, akiondoka kwenda mjini hulazimika kuwatawanya wanafunzi au kuwaacha chini ya uangalizi wa wanafunzi wenzao ambao ni viongozi.
Mbutuka alibainisha kuwa pamoja na tatizo hilo shule hiyo inakabiliwa na tatizo sugu la mdondoko wa wanafunzi unaotokana na wanafunzi hao kukimbilia katika machimbo ya madini ya Miruwi, Nachianji na Mituguru yaliyopo jirani na shule hiyo.

Alisema mwaka 2006, wanafunzi 53 waliripoti shuleni hapo hata hivyo waliobakia ni 31, wakati mwaka 2007 wanafunzi walioripoti walikuwa 111 waliopo 73. Mwaka 2008 wanafunzi 80 waliripoti na waliopo ni 50. Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Wilaya ya Nachingwea, Bakari Mussa, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa halmashauri inashindwa kuwahamishia walimu shuleni hapo kutoka shule zingine ili kupunguza ukubwa wa tatizo kutokana na kukosa fedha za uhamisho.

''Kuna waraka wa serikali unaomtaka mwajiri kutomhamisha mtumishi yeyote bila kumlipa stahiki zake, kwa sababu halmashauri haina pesa tunashindwa namna ya kuiisaidia shule hiyo, lakini uwapo wa tatizo hilo sote tunautambua'' alisema Mussa.

CHANZO:Habarileo


HALAFU 2010 CCM WATAKUJA KUTUIMBIA MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA ELIMU,NA KUDAI WAPEWE TENA MUDA WA KUIPELEKA NCHI YETU WANAKUJUA WAO.MIAKA ZAIDI YA 40 BAADA YA UHURU BADO TUNAKUWA NA SHULE YENYE MWALIMU MMOJA?WATETEZI WATASEMA SIE MASIKINI.MASIKINI GANI ANAYEWALIPA WABUNGE ZAIDI YA 300 SHS MILIONI 7 KWA MWEZI?MASIKINI GANI ALIEIBIWA BILIONI 40 NA KAGODA LAKINI ANAMWONEA AIBU HATA KUMTAJA HADHARANI?

1 comment:

  1. Ama kweli hizi ni mbinde za elimu nchini Bongo.


    Hapo ukiwauliza wanakupa majibu rahisi eti nhe, bajeti ni finyu...

    Hawa hawa wanaosingizia ufinyu wa bajeti, wanaweza kupendekeza kila jimbo liwe na wabunge wawili, na kila mbunge awe na msaidizi, na msaidizi awe na msaidizi wa msaidizi...


    Kama shule inaweza kuwa na mwalimu mmoja na ikawezekana, basi na tuwe na mbunge mmoja kwa mkoa mzima!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.