28 Oct 2009


SERIKALI imeshutumiwa kwa kuibua hoja ya 'posho mbili' kwa wabunge ili kuzima kashfa ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development (LLC) iliyobuni mkataba wa kifisadi kati yake na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Shutuma hizo zinakuja baada ya vyombo vya habari mbalimbali kutangaza jana msuguano uliojitokeza kati ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta aliyetoa hoja kusitishwa kwa wabunge kuhojiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusisitiza kuwa zoezi hilo litaendelea kwa sababu ni agizo kutoka katika Ofisi ya Rais, Ikulu.

Takukuru imekuwa ikiwahoji baadhi ya wabunge, wengi wao wakitajwa kuwa ni miongoni mwa wanaojipambanua katika kupiga vita ufisadi, kwa madai ya kupokea posho mara mbili, kufuatia malalamiko ya baadhi ya idara na taasisi kuwa kamati za Bunge zinadai posho mara mbili.

Sambamba na hoja ya 'posho mbili' za wabunge kwa kazi moja, kuendelea kujadiliwa katika nyanja mbalimbali za kijamii, pia mjadala mkali umekuwa ukiendelea katika mtandao maarufu wa 'wanajamii'.

Mchangiaji mmoja, Richard Mabala alisema anashangaa kuona serikali imeamua kuchagua kupambana na baadhi ya wabunge wakati suala la 'posho mbili' ni utamaduni wa miaka mingi bungeni.

"Mwaka juzi nilipotumwa kazi na wafadhili kuonana na kamati moja ya Bunge, vivyo hivyo walitengewa vijisenti vyao, wakiwemo mawaziri na mawaziri wastaafu ndani ya Bunge, mashirika ya jamii na wafadhili," ameandika.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa hiyo ya Richmond, juzi alizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kusema kuwa kitendo hicho cha Takukuru ni cha kisasi na kuwa kamwe hatokubali kuhojiwa.

Jana Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Juma Haji Duni alisema serikali inaogopa matokeo ya sakata la Richmond na inataka kutumia suala la wabunge kupokea posho mara mbili kama njia ya kutokea, baada ya kukwama kutekeleza maazimio ya Bunge kwa zaidi ya miezi sita sasa.

"Waziri Mkuu Mizengo Pinda na serikali yake anaogopa Richmond, anakazania wabunge wahojiwe kwa kuwa anaona hapo ndio mahali pa kutokea, wanajaribu kukwepa hoja ya msingi," alisema.

Alisema ikiwa serikali ina sura mbili moja ikiwa ya ufisadi na ndio sababu inachelea kuchukua hatua za wazi zilizopendekezwa na kamati ya Bunge kuhusu watendaji wake.

"Kama serikali ina sura mbili, moja ya kifisadi; ingekuwa makini ingewachukulia hatua wote kama ilivyopendekezwa na Bunge. Sasa inashangaza kwa kushupalia posho za wabunge na kuwahoji ikitafuta pa kutokea," alisema Duni na kuongeza:

"Kama serikali ipo makini kwa nini haijasema wazi ni nani waliorejesha fedha za EPA? Si kweli kama posho za wabunge ndiyo suala kubwa kwa sasa. Serikali iache unafiki kwani, kama posho si wabunge pekee hata watendaji wa serikali wanakula mara mbili."

Alisema, Pinda anajipapatua, huo ni unafiki wa serikali kutaka kufunika hoja ya Richmond na kwamba, kama wana umakini mbona waliorejesha fedha za EPA hawatajwi mpaka leo. Kama Takukuru wapo 'serious' (makini) kwa nini hawakulisemea hilo mwanzo wanasubiri wakati huu wa mkutano wa Bunge."

Aliongeza kuwa lililo mbele ni Bunge kuachiwa lifanye kazi yake na wabunge wafanye kazi yao na iwapo serikali kupitia Takukuru inahitaji kuwahoji basi isubiri kumalizika kwa mkutano wa Bunge.

Kauli hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF iliungwa mkono na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF) aliyesema kuwa ingawa hana tatizo na Takukuru kutekeleza wajibu wake, lakini hofu yake ni wakati gani inatekeleza wajibu huo na kama Bunge ambalo pia lina kanuni zinazoweza kufanyia kazi madai hayo limeshindwa kufanya hivyo.

"Ingawa sheria za nchi hazikatazi mtu kuhojiwa wakati wowote, lakini kila jambo lina wakati wake. Kama Takukuru imefanya hivyo ili kudhoofisha nguvu za wabunge kutetea maslahi ya taifa, basi wajue hakuna mtu yeyote anayeweza kulizuia Bunge kufanya kazi yake," alisema Hamad na kuongeza:

"Bunge lisizuiwe kufanya kazi yake. Hata kama litawavuruga wachache bado tutasimamia haki kwani waliobaki pia ni nguvu ya umma, kwa kuwa ni wawakilishi wa wananchi na wana nguvu na uwezo ule ule".

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewasihi wabunge wenzake kukubali kuhojiwa na Takukuru kama njia pekee ya kujisafisha mbele ya umma kuhusu tuhuma za kulipwa posho mara mbili kwa kazi moja.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake bungeni mjini Dodoma jana, alihadharisha kuwa endapo umakini na busara haitatumika katika suala hilo, kashfa hiyo inaweza kuliondolea Bunge heshima ambayo chombo hicho kimejijengea kwa wananchi.

“Sisi wabunge tunapopinga kuhojiwa na chombo cha dola tunatoa taswira mbaya kwa jamii…tunaweza kuharibu hii sifa tuonekane kuna mambo tunayafanya halafu tunajificha na kinga ya Bunge…kinga inatulinda kutoa maoni na michango yetu ndani ya Bunge tusishtakiwe,”alisema Zitto.

Katika mtazamo tofauti Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema anayachukulia mabishano hayo sawa na ya vibaka wawili wanaogombana kila mmoja akitaka kumuwahi mwenzake.

“Takukuru ni questionable (wanatuhumiwa) na wabunge nao pia ni ‘questionable’. Sasa imekuwa ni sawa na vibaka wawili ambao wanapambana na sasa inategemea ni kibaka yupi atamuwahi mwenzake.” alisema Mbatia.

Alifafanua kuwa katika mazingira ya sasa wabunge, wanatuhuma na wanapaswa kuchunguzwa na suala la Richmond nalo linapaswa kuchukua nafasi yake, hivyo Takukuru wasizuiwe kufanya kazi zao kama Bunge nalo lisivyotakiwa kuingiliwa.

Naye Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ambaye pia ni kijana aliyeinukia kwa kasi kisiasa nchini katika miaka ya karibuni, Nape Nnauye, alisema anatilia shaka uhalali wa Takukuru kutekeleza kazi yao wakati huu wa Mkutano wa Bunge, hasa ikizingatiwa hoja nzito zinazotarajiwa kujadiliwa.

"Mazingira ya sasa tuna sakata la Richmond na bado halijaisha na mmoja wa wanaotuhumiwa ni Mkurugenzi wa Takukuru. Hata kama operesheni yao ni 'genuine' (halali) tunaweza tukafikiri ni kuzuia wabunge wasitekeleze wajibu wao," alisema Nnauye.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Malya alielezea kitendo hicho cha Takukuru kuwa ni cha kuwadhalilisha wabunge na kuongeza kama ni suala la kutolewa posho mara mbili kwa wabunge, Bunge kupitia kamati yake ya maadili lingeweza kujadili na kutoa ripoti.

"Tunaamini wabunge wetu wamekuwa wakijadili kwa uwazi mambo yote kwa maslahi ya umma. Suala hilo pia wangeweza kulifanyia kazi. Kitendo cha Takukuru kwenda kuwafuatilia mimi naona ni cha kuwashushia hadhi," alionya Usu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk Edward Hosea, ametia ngumu akitaka uchunguzi dhidi ya wabunge uendelee akisema : "Hakuna mtu aliye juu ya sheria."

Kauli hiyo ya kwanza ya Dk Hosea tangu kuanza uchunguzi huo ambao sasa umefikia hatua ya juu zaidi, inakuja kipindi ambacho tayari kumeibuka msuguano kati ya mihimili miwili ya dola, ambayo ni Bunge na Serikali.

"No one is above the Law..., no matter who are you (Hakuna aliye juu ya sheria, bila kujali wewe ni nani)," alisema Hosea na kuongeza:

"Sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na katiba, kwa hiyo hatuangalii nani ni nani zaidi ya sheria na katiba".

Mapema mwaka huu Dk Hosea alionya wabunge kwamba, wakianza mchezo wa kuumbuana hawatasalimika, kwani kumekuwa na taarifa na ushahidi wa kutosha kuhusu ufisadi wao wa kuchukua posho mara mbili.

Akionyesha kutimiza azma hiyo, Hosea alisema hapendi malumbano na wanasiasa kwani yeye si mwanasiasa mwenye jukwaa kama Bunge, ila atasimamia sheria.

"Wanaweza kusema mambo mengi, mimi si mwanasiasa sipendi malumbano na wanasiasa, wao wana audience (hadhara) mimi sina, wana Bunge na wanaweza kukaa bungeni na kuzungumza chochote," alifafanua Hosea na kusisitiza:

"Lakini kwa kifupi ni kwamba, msimamo wa Takukuru uko wazi, ni kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na katiba basi, hakuna jambo jingine".

Alipoulizwa endapo uchunguzi huo una msukumo na nguvu za aina yoyote nje ya sheria na utendaji kazi wa kawaida wa Takukuru, alijibu: "Nasisitiza, sipendi malumbano na wanasiasa, wanaweza kusema mengi, lakini tunasimamia sheria tu".

Msuguano huo unaondelea kati ya mihimili hiyo miwili ya dola, pamoja na mambo mengine unaweza kuliingiza Bunge la Tanzania katika kashfa mbaya ya matumizi mabaya ya fedha za umma kama ilivyokuwa kwa Bunge la Uingereza.

Tayari hadi sasa, wabunge wengi wakiwa ni kutoka Kamati ya Nishati na Madini wakiongozwa na Shellukindo mwenyewe, wamekwishahojiwa kutokana na tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa habari ambazo gazeti hili imezipata, karibu wajumbe wote 21 kutoka Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma wamekwishaitwa kuhojiwa huku mwenyekiti wao Zitto akiwa njiani.

Baadhi ya wabunge kama James Lembeli wa Kahama na Dk Mwakyembe, walikwishaitwa kuhojiwa lakini hadi sasa hawajafanyiwa hivyo, huku mbunge huyo wa Kyela akiweka bayana kwamba, hayuko tayari kuhojiwa na Takukuru vinginevyo apelekwe mahakamani.

Baadhi ya wananchi waliliambia gazeti hili kwamba, hawaoni sababu ya wabunge kulalamikia kitendo cha Takukuru.

"Mjadala wa bunge hauwezi kuzuia mambo mengine yasifanyike... kama wabunge watashindwa kwa sababu tu ya kuhojiwa basi kazi yao watakuwa hawaijui. Na pengine hili litakuwa ni changamoto kwao," alisema Hamis Athuman.

Imeandaliwa na Exuper Kachenje, Leon Bahati na Ramadhan Semtawa

SOURCE: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube