22 Jan 2010


Sadick Mtulya

HATIMAYE Pascal Mnaku, mlinzi wa kampuni ya Ultimate Security aliyepambana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwenye mashine ya kuchukulia fedha (ATM) jijini Dar es Salaam, amefukuzwa kazi na muajiri wake huyo.

Mnaku alijikuta kwenye mpambano mkali na waziri huyo baada ya kumtaka asogee pembeni ya mashine hiyo ya Standard Chartered ili kupisha wateja wengine baada ya Ngeleja kuonekana akitumia muda mwingi kuongea na simu akiwa ndani ya chumba cha mashine hiyo.

Kwa mujibu wa habari tulizozipata kutoka Ultimate na kuthibitishwa na Mnaku, uamuzi wa kumfukuza kazi ulitolewa mara baada ya kikao cha nidhamu cha kampuni hiyo kilichofanyika jana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi jioni kwenye ofisi za Ultimate.

"Ni kweli nimefukuzwa kazi na hivi ninavyoongea na wewe ndio nimetoka katika kikao cha nidhamu na uamuzi uliofikiwa ndio huo,"alisema mlinzi huyo ambaye hakutetereka wakati Waziri Ngeleja alipohoji kama anamfahamu ni nani wakati akitakiwa kutoka kwenye ATM.

"Na hii ni kutokana na kitendo changu cha kumtaka Waziri Ngeleja awapishe wateja wengine kwenye ATM," alilalamika Mnaku.

Jana jioni Mnaku aliliambia Mwananchi kuwa anatakiwa aende kuchukua barua yake ya kutimuliwa kazini Januari 30.

Hata hivyo, mara baada ya gazeti hili kuripoti sakata hilo, Ngeleja alikiri kutokea kwa mtafaruku huo na kujitetea kuwa Mnaku ndiye aliyekuwa chanzo cha mtafaruku huo uliotokea kwenye mashine ya fedha iliyo kwenye jengo la Harbour View (zamani JMall).

Mwananchi iliripoti kuwa waziri huyo alikaribia kuzichapa na mlinzi huyo kwenye baada ya kuombwa asogee pembeni kupisha wateja wengine.
CHANZO: Mwananchi
OMBI LA BLOGU HII KWA WAZIRI NGELEJA NI KUTAMBUA KUWA AJIRA YA MNAKU IMEOTESHWA NYASI KWA "KOSA" LA KUWAJIBIKA KAZINI.NGELEJA ANAPASWA KUFAHAMU KWAMBA UWAZIRI HAUMPI IMMMUNITY YA ADHABU ZA MBELE YA SAFARI YA MAISHA YA KILA BINADAMU.ANAPASWA KUTAMBUA JAPO MISHAHARA YA WALINZI WA MAKAMPUNI BINAFSI NI KIJUNGUJIKO MNO,LAKINI KWA HAKIKA ILIKUWA IKIMSAIDIA MNAKU NA FAMILIA YAKE.KWA KUFUKUZWA KAZI,NI DHAHIRI MNAKU NA FAMILIA YAKE WANAINGIA KATIKA LINDI LA MAISHA YASIYO NA UHAKIKA WA KESHO ITAKUWAJE.
BLOGU HII PIA INATOA WITO KWA TAASISI ZA HAKI ZA BINADAMU PAMOJA NA WANASHERIA WENYE UCHUNGU NA UTAWALA WA SHERIA KUTOA MSAADA KWA NDUGU MNAKU.UMANGIMEZA WA AKINA NGELEJA HAUPASWI KUACHWA UDUMU AU KUHALALISHWA.SHAME ON YOU,YOUR EXCELLENCY!

1 comment:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.