4 Jul 2010

Kwanza naomba samahani kwa kupotea kwa zaidi ya wiki sasa.Afya iliyumba kidogo.Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wote walionitumia meseji za kunitakia afya njema.Bwana Amesikiliza sala na dua zenu.

Jana,katika pitapita zangu mtandaoni nilikutana na habari kwamba Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,Juma Mwapachu,amewashukia wasomi wa vyuo vikuu kwa kuwapotosha wananchi kuhusiana na serikali kujiunga na soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililofunguliwa majuzi.

Kwa mujibu wa habari hiyo,Balozi Mwapachu alitoa kauli hiyo kufuatia ya baadhi ya wasomi kudai kuwa soko hilo linaweza kuwaathiri watanzania katika ushindani wa ajira.Akizungumza jana kwenye ufunguzi wa maonyesho ya 34 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Balozi Mwapachu alisema wasomi hao ambao wamesomea uchumi, wameshindwa kusema ukweli kuhusiana na kujiunga na soko hilo, na kusababisha wananchi kuingia uoga.

Alisema wasomi walipaswa kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi kuhusu jumuiya hiyo na faida zake badala ya kuwapotosha wananchi kuhusu suala hilo na kusababisha baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuhofia.

Alisema kabla ya kufungua milango hiyo aliweza kuzunguka katika kila nchi kwa ajili ya kuzungumza na wadau mbalimbali kuhusu suala hilo, lakini wananchi wamekuwa waoga na kusababisha kutoa maoni mbalimbali ya kupotosha.

"Niwashaangaa sana wasomi tena wamesomea uchumi, lakini wamekuwa wa mbele kuwapotosha wananchi kuhusu soko la pamoja la jumuiya ya Afrika Mashariki, hii imesababisha wanachi washindwe kujiamini na kufikiri kuwa wanaweza kukosa ajira,"alisema Mwapachu.

Alisema watanzania wengi wanawaogopa wakenya kwa madai kuwa wanaweza kushindwa kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira.

Nadhani kwa mtu mwenye uelewa mkubwa kama Balozi Mwapachu kutoa kauli hizo ni jambo la kusikitisha sana na ni uthibitisho mwingine wa namna maslahi binafsi na ya kisiasa yanavyowekwa mbele ya maslahi ya taifa,sambamba na kupuuza ushauri wa kitaalam.

Yayumkinika kuamini kuwa kwa wadhifa wake kama Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo,ni lazima Mwapachu aipigie debe ili iendelee kuwepo kwani kinyume chake ni kuwa hatakuwa na ajira.Hata hivyo,laiti Mwapachu angeangalia mantiki ya hoja za wasomi (ambazo kwa hakika ziko shared na hata "wasio wasomi") badala ya kuwashambulia kama kundi la kijamii (yaani kujadili hoja badala ya kumjadili mtoa hoja)angeweza kabisa kufahamu kwanini wanaonyesha wasiwasi wao.

Hivi kama kabla ya ujio wa soko la pamoja la Jumuiya hiyo tayari wageni (licha ya hao wanaotoka Kenya na nchi nyingine za Jumuiya) tayari soko la ajira na bidhaa limetawaliwa kwa kiasi kikubwa na wageni,kwanini basi tusihofu kuwa "kuhalalisha" huko kutapelekea hali kuwa mbaya zaidi kwa Watanzania?

Na wakati Mwapachu anatoa porojo zake kuhusu mafanikio ya soko la pamoja,mbona hatuambii yeye na viongozi wenzie wa Kitanzania wameshafanya jitihada zipi kuhamasisha Watanzania kumudu ushindani uliopo na ujao?Siafikiani na mawazo potofu ya Mwapachu kuwa tatizo la Watanzania ni uoga.Na hata kama tatizo lingekuwa ni uoga basi bado hoja ingekuwa iwapo uoga huo ni halali au potofu kwani uoga kama uoga sio dhambi au kosa kama unajengwa kutokana na mantiki.Tatizo la msingi linalowakabili Watanzania kukabiliana na changamoto za mfumuko wa nguvu za nje katika soko la ndani la ajira na bidhaa ni complex sana,na makala hii fupi haiwezi kujadili yote bali itaangalia kwa ufupi.

Kwa upande wa biashara,kuna tatizo sugu la urasimu ambalo kwa kiasi kikubwa linachangiwa na ufisadi.Urasimu kuanzia kwenye utaratibu wa kuandikisha biashara hadi kwenye masuala ya kodi.Sijawahi kufanya biashara lakini nina marafiki kadhaa wanaojaribu kumudu maisha yao kwa kujihusisha na biashara.Kwa kifupi,ajira ya Mtanzania kwa kutegemea biashara ni suala gumu sana.Katika mazingira ya kawaida sio rahisi kwa biashara kudumu kwa angalau miezi kadhaa kama mhusika hatokuwa tayari kutoa chochote kitu kwa wahusika.Yayumkinika kusema kuwa ili biashara halali ishamiri vema ni lazima ikaribishe illegality ya namna flani,yaani uharamu wa biashara ili kuwa halali.

Na wakati Watanzania wengi tu wangependa kujishughulisha na biashara zao kihalali ili wamudu maisha yao,wanakumbana na ushindani kutoka kwa wenzao "wanaobebwa" na vigogo.Hivi mfanyabiashara anayelipa mlolongo wa kodi huku anauza bidhaa za ndani atamudu vipi kupambana na mfanyabiashara anayeagiza vitu kutoka nje (huku vingine vikiwa feki) lakini anavilipia kodi pungufu au halipi kodi kabisa?Ni dhahiri biashara ya huyo "anayebebwa" itashamiri zaidi kuliko ya huyo mnyonge anayejikongoja peke yake.

Lakini pia kuna suala la utamaduni wa kuthamini baidhaa za nje kuliko za ndani.Baadhi ya wachambuzi wanaeleza kuwa miongoni mwa madhara ya utandawazi ni kuibuka kwa mapambano kati ya vitu vya nje dhidi ya vya ndani au vya asili.Hapa simaanishi kuwa kila element ya utandawazi ni mbaya.Sasa kama serikali yetu inaagiza kila kitu kutoka nje kwa ajili ya matumizi yake huku ikiwaacha mafundi seremala wetu "wakidodewa" na samani zao,na hiyo ni kabla ya ufunguzi wa soko hilo,sasa kwanini wasomi wasihofu kuwa soko hilo linaweza kuwa habari mbaya zaidi kwa Watanzania wengi?

Tukija kwenye ajira,hali ndio mbaya zaidi.Wakati Watanzania wamekuwa mahiri zaidi kupeleka watoto wao Kenya na Uganda,wenzetu hao wamekuwa wakileta nguvu kazi yao ya ziada kuchukua nafasi mbalimbali za kazi.Na kama ilivyo kwenye suala la bidhaa,waajiri wetu nao wanaelekea kuwa na ugonjwa uleule wa kuthamini zaidi wageni kuliko wazawa.Mwapachu alipaswa kutueleza ni Watanzania wangapi wana ajira nchini Kenya,Uganda au Rwanda kulinganisha na raia wa nchi hizo waliokamata ajira hapo nyumbani kabla ya ujio wa soko la pamoja.Najua hawezi kusema hilo sio kwa vile hana takwimu (na inawezekana kabisa akawa hana) bali anafahamu kuwa kwa kweka hilo bayana atalazimika kuungana na hofu walionayo wasomi na Watanzania wengine.

Kilichoua Jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki ni kuweka siasa mbele ya maslahi ya nchi.sambamba na kupuuza ushauri wa wataalamu.Na akina Mwapachu ambao walikuwa watu wazima muda huo wanataka kurejea makosa hayohayo.Wanajifanya vipofu wa ukweli kwamba ni vigumu kuwa na ushirikiano wa maana palipo na viwango tofauti vya maendeleo kati ya nchi husika.Tunafahamu vema uchumi wa Kenya,Uganda na Rwanda unavyofanya vema zaidi ya uchumi wetu.Sasa kama tunafahamu hilo kwanini basi tusihofu kuwa soko hili jipya linaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi?Au Mwapachu na wenzake wanadhani kuwa ukigusana na tajiri nawe unapata utajiri?They are completely wrong.Mahusiano ya mwenye uwezo wa kiuchumi na mwenye uwezo duni mara nyingi huishia kumnufaisha zaidi mwenye uwezo kwani nguvu ya uchumi inapelekea kuwa na nguvu kwenye maeneo mengine pia.

Akina Mwapachu wanapaswa kufuatilia kwa karibu mambo yanayoyumbisha jumuiya ya Ulaya ambapo nchi kama Uingereza zimeendelea kuwa na msimamo wa kujihusisha kwa kiasi flani tu na sio kwa asilimia 100 kwa vile wanatambua kuwa kuna nchi zenye uchumi duni zinazotarajia ushirikiano huo uwanufaishe wao zaidi at the expense of wale wanaojimudu.

Mwisho,ili Tanzania ijikomboe kutoka uchumi unaomilikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 na wageni ni lazima siasa iwekwe kando,ushauri wa kitaalamu uzingatiwe,na kubwa zaidi,maslahi ya taifa yawekwe mbele ya maslahi binafsi.Vinginevyo,soko la pamoja la Afrika Mashariki litaishia kuwa soko la bidhaa na ajira kwa Wakenya,Waganda,Wanyarwanda na Warundi na sie "tukiishia kunufaika" kwa uwepo wa akina Mwapachu kama viongozi wa jumuiya ilhali uchumi wetu ukizidi kuelekea shimoni.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.