9 Aug 2010

Ni dhahiri kwamba baadhi ya vyombo vya habari huko nyumbani vimeshachukua msimamo wa kukipendelea chama tawala CCM.Kwao,habari ni zile zinazoihusu CCM tu,na lazima ziwe habari za kupendeza machoni au/na masikioni.Hatuwezi kuyalaumu magazeti kama Uhuru na Mzalendo,au Redio Uhuru (kama bado ipo) kwa vile vyombo hivyo vya habari vinamilikiwa na CCM.

Lakini haivumiliki kuona TBC,taasisi inayoendeshwa kwa fedha za walipa kodi pasipo kujali itikadi zao za kisiasa,ikielemea upande wa CCM.Awali niliposikia Tido Mhando ameteuliwa kuwa bosi wa taasisi hiyo ya habari nilipata matumaini makubwa hasa kwa vile kabla ya uteuzi huo,Tido alikuwa mtumishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),ambalo kwa hakika ni "mwiba mchungu" kwa serikali.Kwa BBC,cha muhimu ni habari na sio kujikomba kwa chama tawala.Wakati wa uongozi wa chama cha Labour,BBC ilijikuta mara kadhaa ikigongana na serikali huku ikituhumiwa kuwa habari zake zinalenga kuikosoa serikali ya chama kilichokuwa madarakani kwenye takriban kila jambo.

Huko nyumbani tatizo lina sura mbili:KUJIKOMBA na UOGA.Baadhi ya vyombo vya habari vinajikomba kwa watawala kwa sababu wanazojua wao wenyewe.Hili nalihusisha zaidi na legacy ya utawala wa chama kimoja ambapo kiongozi alikuwa mithili ya mungu-mtu.Habari za kiongozi sharti ziwe nzuri,awe amepongezwa au kupongeza,ametunukiwa nishani,ameng'ara katika suala fulani,nk.Lakini madudu yanayofanywa na watawala wetu ni off-limits.Vioja vinavyofanywa na waheshimiwa wetu wanapokutana Dodoma kwenye vikao vya Bunge havipaswi kuripotiwa kwenye vyombo vya habari labda awe ni mwakilishi wa chama cha upinzani.

Tatizo la pili ni hilo la uoga.Sijui uoga huu unatoka wapi.Ingeeleweka kama habari husika zingekuwa za kutunga.Lakini kuna haja gani ya kuwanyima wasomaji/wasikilizaji haki yao ya msingi ya kuhabarishwa matukio mbalimbali yanayowahusu wanasiasa na viongozi wetu kwa vile tu habari hizo "hazitowapendeza" vigogo hao?

Kibaya zaidi ni pale hata habari zisizohusiana na maadili (kufumaniwa,ku-cheat,kutelekeza familia,nk) nazo zinaingia katika mkumbo huo.Na wakati mzuri wa kushuhudia upendeleo huu wa wazi ni katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.Inaelezwa kuwa jamaa wa TBC waliamua kuonyesha sehemu ya juu ya mwili wa Dkt Slaa katika mkutano wake kwenye viwanja vya Jangwani,jijini Dar hapo Jumamosi.Hofu ya TBC ni kwa watazamaji wao kuona idadi ya watu waliojitokeza kwenye shughuli hiyo.Hivi kwa akili yao wanadhani kuficha idadi ya wahudhuriaji itamkwaza Dkt Slaa kufikia mafanikio yake?Na kwanini wawanyime haki walipakodi wa Kitanzania ambao fedha zao ndio zinaendesha TBC?


Kibaya zaidi,ugonjwa huu unaelekea pia kuvikumba vyombo vya habari vya kijamii (social media) hususan blogu.Haina haja ya kutajana majina lakini binafsi nilisikitishwa kwa baadhi ya mabloga wetu kupuuzia tukio hilo muhimu.Wanajijua,na wanafahamu wenyewe kwanini walifanya hivyo.Ofkozi,nafahamu fika kuwa uamuzi wa kuweka au kutoweka habari au/na picha ya tukio ni uamuzi wa blog husika,lakini ni muhimu kwa bloga kutambua kuwa wasomaji wake wana itikadi mbalimbali,na kuminya baadhi ya picha/habari kwa vile tu "zitawakasirisha wakubwa" ni kutowatendea haki wasomaji wetu.

Ni muhimu kuishi katika dunia halisi (realistically) ambapo lolote linawezekana katika siasa.Huyo Slaa mnayemsusia kwenye vyombo vyenu vya habari anaweza kabisa kuwa rais ajaye wa Tanzania.Je akishinda mtaendelea kukwepa habari zake?Kwanini tusijaribu kubalansi kati ya itikadi na maadili ya kazi,kwa upande mmoja,na mapendezeo yetu binafsi na matarajio ya baadhi ya wasomaji wetu?

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube