5 Sept 2010

Kuna msemo wa Kiingereza usemao "unchallenged,a lie often assumes a status of truth",yaani uongo usipokabiliwa unaweza kupata hadhi ya ukweli.Msemo huu unaweza kuwa na umuhimu wa kipekee kwa mgombea wa tiketi ya urais kupitia Chadema,Dokta Wilbroad Slaa.Tangu atangazwe kuwa mgombea wa chama hicho,kumekuwa na mashambuli lukuki yanayoelekezwa kwake katika jitihada za kuifanya jamii imwone kuwa mchafu na asiyefaa kumrithi Jakaya Kikwete,mgombea kwa tiketi ya chama tawala CCM.

Ni dhahiri kuwa wanaoeneza sumu hiyo dhidi ya Dkt Slaa wanafanya hivyo kwa malengo makuu mawili.Kwanza,kama nilivyobainisha hapo juu,ni kumfanya aonekane hafai kuwa rais wa Tanzania.Aonekane hafai,kisha akose kura za kutosha kumwingiza Ikulu,na mafisadi waendelee kuvuna wasichopanda katika nchi yetu iliyogeuzwa shamba la bibi.

Lakini la pili ni kupoteza malengo au kwa ufasaha ku-divert attention.Yaani wanachotaka ni Dkt Slaa na Chadema waanze kuhangaika kujibu shutuma,jambo ambalo litawapunguzia muda na focus ya kampeni.Yaani badala ya mgombea huyo kuwashawishi Watanzania atawafanyia nini,mafisadi wanataka aanze jukumu la kujitetea kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake.

Wapo wanaoshauri kuwa dawa ya kudili na tuhuma ni kuzipuuza.Kuna wakati mkakati huo ni mzuri lakini hilo linawezekana katika aina flani ya jamii.Katika jamii yetu ambapo bado asilimia kubwa ya watu wananyimwa uhuru wa kujua ukweli na kuchanganua mambo,uongo usiokanushwa unaweza kabisa kuchukua nafasi ya ukweli.Na ukidhani nachoandika hapa ni hisia zangu tu basi rejea zengwe aliloundiwa Dokta Salim Ahmed Salim alipotangaza dhamira yake ya kugombea urais mwaka 2005.Kikwete na wanamtandao wenzake walimwaga sumu kubwa dhidi ya Dkt Salim hadi wakafanikiwa kumdhibiti.Jitihada zake za kujisafisha hazikuweza kufua dafu kwa character assassination strategy ya wanamtandao.

Ikumbukwe kuwa tunaishi katika jamii iliyolazimika kutegemea umbea na tetesi kubashiri ukweli.Haya ni baadhi ya matokeo ya mfumo dhalimu wa chama kimoja ambapo mambo pekee yaliyopaswa kufahamika kwa umma ni yale yaliyoonekana mazuri kwa watawala.

Kadhalika,kinachotokea kwa Dokta Slaa ni sehemu ya uchafu unaoambatana na fani ya siasa (politics is a dirty game).Huko Marekani,baada ya Barack Obama kuonekana ana nguvu za kumpeleka Ikulu,zilianza kampeni chafu kuhusu imani yake ya dini ikidaiwa alikuwa Muislam (kana kwamba Uislam ni sawa na uhaini nchini humo).Baadaye wakamzushia kuwa sio raia wa Marekani.Timu ya Obama haikukaa kimya bali ilipambana kwa nguvu dhidi ya kampeni hizo chafu na hatimaye Obama akafanikiwa kuingia Ikulu.

Chadema na Dokta Slaa wanaweza kuamua kuwapuuza wanaoeneza sumu kali dhidi yao.Lakini kwa namna hali ilivyo ambapo vyombo vya serikali (vinavyoendeshwa kwa fedha za walipa kodi) kama gazeti la Habari Leo vinapojiunga na kampeni hizo za siasa za maji taka basi ni muhimu kukabiliana nao mapema.

Na kwa kuanzia,nadhani kuna umuhimu wa kulichukulia hatua gazeti la Habari Leo hususan pale lilipoandika "Dokta Slaa padri msomi".Sentensi hiyo ilikuwa na lengo la kumkosesha mgombea huyo kura za wasio Wakatoliki.Ni dhahiri sentensi hiyo ililenga kuendeleza kashfa kuwa Dokta Slaa ni kiongozi wa dini na anataka kuingia Ikulu kuwatumikia Wakatoliki/Wakristo na sio Watanzania wote kwa ujumla.Kulipeleka gazeti hilo kwa Baraza la Habari ni kupoteza muda kwa vile sana sana wataishia kupewa onyo tu.Wanachostahili sio onyo bali adhabu kali ya kuwakumbusha kuwa wanatumia vibaya fedha za walipa kodi kwa maslahi ya watu binafsi.Ni mafisadi kama wale wa Kagoda au Richmond.

Sijui sheri za Tanzania zinasemaje kuhusu super injunctions zinazokataza kuzungumzia maisha ya mtu binafsi.Hapa Uingereza baadhi ya watu maarufu wamekuwa wakizitumia taratibu hizo za kisheria kuwabana vimbelembele wanaoishi kwa kuchokonoa maisha ya wenzao.Naamini Chadema wana wanasheria mahiri wanaoweza kuangalia namna ya kukabiliana na wazushi hawa wanaofadhiliwa na mafisadi.

Blogu hii inatoa wito kwa Dokta Slaa na Chadema kwa ujumla kutokalia kimya uhuni huu ambao pasipo kudhibitiwa unaweza kabisa kuathiri matokeo ya uchaguzi.Hatuhitaji kujiuliza kwanini wamwandame Dkt Slaa pekee na sio wagombea wengine kwani rekodi yake dhidi ya mafisadi ni siri iliyo wazi,na hofu kubwa ya wanaoeneza sumu dhidi yake ni kuwa akiingia Ikulu itawalazimu watafute mahala pa kujificha.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.