26 Sept 2010



Mwaka 2004,jarida maarufu la TIME la nchini Marekani lilimtangaza Rais wa zamani wa nchi hiyo,George W. Bush,kuwa "Mtu wa Mwaka" (Time Person of the Year 2004).Katika mahojiano na jarida hilo,Bush alizungumza mambo mawili ambayo japo sikuwahi kuwa shabiki wake yameendelea kunisaidia katika tafakuri zangu hususan kwenye fani ya uandishi kwa ajili ya jamii.

Jambo la kwanza ni kauli yake kuwa "japo nafahamu kuna watu hawaafikini na mtizamo wangu lakini angalau wanafahamu ninaposimamia kimtizamo".Akifafanua,Bush alisisitiza kwamba kama unaamini katika jambo flani basi inabidi ulisimamie hususan panapojitokeza upinzani au kukusolewa.

Jambo la pili ni imani yake kuwa upinzani au kukosolewa kunaweza kumsaidia mlengwa,kwa maana ya kujitambua yeye ni mtu wa aina gani-kwa mazuri au mabaya.Kadhalika,kwa mujibu wa Rais huyo wa zamani,ukiona unakosolewa au ulichosema/kufanya kinapelekea upinzani basi ujue kwa namna moja au nyingine kimewagusa wanaokupinga au kukukosoa.Kwamba,kama ulichosema au kufanya ni cha kipuuzi,nani atakuwa na muda wa angalau kukikosoa au kukipinga,let alone kukiangalia au kukisikia?

Ni "busara" hizo mbili za Dubya zilizonisukuma kuzungumzia mfumuko wa comments za kashfa na matusi kuhusiana na makala zinazohusu kampeni huko nyumbani.Unajua binadamu akimudu kufikia hatua flani ya maisha,hasa kama amepitia milima na mabonde,basi anakuwa na "ngozi ngumu" (thick-skinned).Binafsi nilitoka katika familia isiyojimudu sana,nikasoma kwa koroboi kwa vile nyumba yetu haikuwa na umeme,O' level na A'level nikategemea zaidi fadhila za ndugu,jamaa na marafiki kwa vile familia haikuwa na uwezo wa kumudu kila mahitaji yangu.Nakumbuka makazi yangu ya muda katika kambi ya JKT ya Ruvu iliyokuwa ikisifika kama kimbilio la watoto wa vigogo.Kwa hakika,adhabu za kijeshi hazikufua dafu kwa adhabu za kisaikolojia tulizokuwa tunapata hohehahe kama mie tuliochanganywa na watoto wa vigogo.

Pamoja na vikwazo na ugumu wote huo,namshukuru Mungu,wazazi wenye upendo,ndugu,jamaa na marafiki walionisaidia kwa hali na mali na kuifanya historia yangu iwe ya fanikio moja baada ya jingine.Haya ni masuala binafsi na nisingependa kuyazungumzia ila nachoweza kuweka bayana ni kuwa sijawahi kufeli tangu shule ya msingi,O'level,A'level,Mlimani (UDSM) na Chuo Kikuu cha Aberdeen ambapo nimefanikiwa kupata shahada mbili huku nikiendelea kuisaka ya tatu (nikiipata,zitakuwa shahada nne kwa ujumla).Naamini kuwa nitaendeleza historia ya kutofeli.Na la muhimu ni kupata shahada husika na si wala imegharimu muda gani.Sasa anapojitokeza  kichwa-panzi (ambaye pengine hata akitakiwa kuhitimu cheti cha chekechea itamlazimu apatiwe msaada wa twisheni) anapokashifu hatua ya kuridhisha kidogo niliyofikia inabidi kumhurumia tu.

Ugumu niliopitia katika maisha umenisaidia sana sio tu kuwa na "ngozi ngumu" bali pia kujifunza namna sahihi ya kuishi.Kuna msemo kuwa ukiweza kusalimika kwenye ugumu ni wazi hutoshindwa kumudu unafuu.Nimejifunza kuheshimu ubinadamu na utu wa mtu.Nimejifunza pia umuhimu wa imani- ya kiroho na kimtizamo-katika kufikia malengo ya maisha.Japo sijafika mahala pa kusema hapa ndio destination (kituo) yangu ya maisha,nimejifunza kuridhika na kidogo ninachopata huku nikijikumbusha kuridhika huko kusinilemaze kufikia malengo ya awali.

Kashfa na matusi (kutokana na msimamo wangu kumsapoti Dokta Wilbroad Slaa kwa nguvu zote) zinatoka kwa watu ambao si vigumu kuwafahamu.Unajua mtu anapoweka comment as anonymous haimaanishi kuwa bloga makini hawezi kujua mahali alipo mtoa comment.Ni rahisi tu kwa ku-track IP address kwa muda comment husika ilipowekwa.Sasa takriban comments zote zenye kashfa na matusi zinatoka maeneo nayoyahusisha na jamaa zangu flani wa zamani.Tatizo la wazembe hawa hawawezi hata kuwezesha IP zao zisitambulike,simply because fungu la fedha linalotolewa kwa madhumuni hayo zinaishia kuwekezwa matumboni mwao kama sio kwenye nyumba ndogo zao.Hawa wanasumbuliwa na ugonjwa wa kutanguliza maslahi ya matumbo yao na kusahau kabisa watu wanaowazunguka (including ndugu zao).Kulipwa mshahara mkubwa na posho nono kila katikati ya mwezi sio kigezo cha kusahau ndugu,jamaa na marafiki wanaoteseka mtaani,kijijini na kwingineko kwa vile tu wewe unayepaswa kuwatumikia ipasavyo unaelekeza nguvu kwa anayewatesa watu hao.

Imani yangu ni kwamba ufisadi ni kama ukimwi.Yaani,hata kama hujaambukizwa ukimwi basi kuna nduguyo,rafikio,jamaa au mtu unayemjua ambaye aidha anateswa na ugonjwa huo au ameshafariki.Ndio maana ya msemo kuwa hata kama ukimwi haujaku-affect bado ugonjwa huo una effect kwenye maisha yako.Katika namna hiyohiyo,hata kama mwajiri wako anakupatia mamilioni kama mshahara na laki kadhaa za "kuiweka nchi salama" haimaanishi ufisadi unaowatesa walalahoi huko mtaani haukugusi.Ukitanua kidogo tu wigo wa wahanga hao wa ufisadi utakutana na nduguzo,jamaa,rafiki na watu wengine ambao kwa namna moja au nyingine wanakugusa.Kwahiyo wakati jamaa zangu hao wanatoa kashfa na matusi kwa vile tu nasimamia kile wanachoona kama kinatishia "usalama" wa ajira zao,wanapaswa kutambua pia kuwa jitihada zangu zinawasaidia wao pia (kwa maana zinalenga kuwasaidia wale ndugu,jamaa,marafiki,nk wa haohao jamaa zangu).

Matusi,kashfa na vitisho haviwezi kubadili msimamo wangu.Tatizo la jamaa zangu wanaofanya hivyo ni lilelile alilogusia Bush kuwa angalau mie najua ninaposimamia na ndio maana naweza kutamka hadharani ninachoamini pasipo kuficha jina langu.Neno sahihi ni kuthubutu (to dare).Tatizo jingine la jamaa zangu hao ni kuguswa na kile nachoamini.Ajikunaye ujue anawashwa.Laiti ningekuwa namsifia Kikwete,au naweka picha tu bila mtizamo wangu binafsi basi jamaa hawa wasingediriki kufanya wafanyacho sasa.Na kwa vile wanawashwa,nami ntaendelea kumwaga dozi.

Anyway,simlalamikii mtu kwa vile safari ya ukombozi ni ngumu.Kuna mzembe mmoja anauliza eti je namsapoti Dkt Slaa kwa kutegemea wadhifa flani huko nyumbani.Laiti angejua undani wa maisha yangu asingehisi hivyo lakini inawezekana anachokonoa ili niropoke (wao na mie tulifundishwa kuwa miongoni mwa njia za kumchonoa mtu ni aidha kuzusha la kuzusha ili mtu aropoke au kumtibua ili aropoke).Kwa kuwa wao wamezowea kulipwa kwa kila wanachofanya,including "asante" za mafisadi wanaowatumikia basi wanadhani kila anayefanya jambo anatarajia malipo.Nachotegemea kwa Dokta Slaa atapoingia Ikulu hapo Novemba ni kuwapatia Watanzania WOTE kile wanachoendelea kunyimwa na utawala dhalimu wa kifisadi wa CCM kwa takriban nusu karne sasa ("WOTE"  hawa wanaotoa kashfa na matusi pamoja na ndugu,jamaa,marafiki etc waliosahauliwa na wenye midomo michafu hawa).

Na kwa vile vichwa panzi hawa hawakuwa na interest na blogu hii hadi nilipoweka bayana msimamo wangu dhidi ya Kikwete na sapoti yangu kwa Dkt Slaa,hawafahamu (au wanafahamu lakini wanazuga tu) kwamba kwa muda mrefu blogu hii imekuwa mstari wa mbele katika kukemea ufisadi.Nisiandikie mate kwa sababu ushahidi unapatikana hapo kwenye "makala za nyuma".Na kwa waliokuwa wakifuatilia safu za "Kulikoni Ugahibuni", "Mtanzania Ughaibuni" na "Raia Mwema Ughaibuni" katika magazeti ya Kulikoni,Mtanzania na Raia Mwema,respectively,wanafahamu vema kuhusu msimamo wangu.Sasa sijui wazembe hawa wanaohusisha posts zangu za kampeni na "matarajio ya kupata chochote" wanataka kusema hata safu hizo (2006-2008) nazo zililenga "kutarajia chochote" !!!

USALAMA WA TAIFA LILILOJAA MASIKINI WANAOKANDAMIZWA NA KUNDI DOGO LA MAFISADI WANAOLINDWA NA TAASISI ZA KUSIMAMIA MASLAHI YA UMMA NI SAWA NA TIME-BOMB.MUDA WA KULI-DEFUSE NI HUU.BADALA YA KASHFA NA MATUSI,TUMIENI FEDHA ZA WALIPAKODI KUUTUMIKIA UMMA NA SIO MAFISADI.

2 comments:

  1. Hapo kaka Chahali ujumbe umefika bila shaka kwa mafisadi wote na walinzi wao.

    Amini hawa watu wanataka kubadilisha mwelekeo wa hii bloga iwe ya kujibu maoni yao ya kitoto na ukitope(kihiyo).

    Kamwe husikubali kuwekeza muda na busara zako Bwana Chahali kuwajibu hawa ndondocha(mafisadi na mashabiki wao) hata kama iwapo ni asasi ya serikali.

    Endelea kutoa dozi kama kawaida, wakati utapofika mwezi Novemba watamani kuingia ardhini kujizika wenyewe kabala mkno wa sheria kuchukua mkondo wake.

    ReplyDelete
  2. Dawa ya wanywanywa hawa ni kuandika zaidi na zaidi tena kwa jazba na nyodo. Mie yamewahi nikuta hayo nikaongeza ukali hadi wakashika adabu na kukubali hawaniwezi. Kwanza licha ya kutokuwa na busara wala elimu, hawana hoja ukiachia mbali kutetea uoza kwa sababu ya uchumia na uchangudoa wao. Hata waliobahatika kusoma nao hawana hoja zaidi ya kuwa Makawambwa au vihiyo wa kawaida ukiachia mbali Wajipendekezaji kama rafiki yangu Silvia Rweyependekeza msemaji wa Kikwekwe kama unasoma kijiwe changu kila ijumaa kwenye gazeti la Tanzania Daima. We need but freethinking mechanism. Watake wasitake mbwa hawezi kumtisha simba wala kuku hawezi kushindana na kanga. Kaka ukipata nafasi tunga hata kitabu wajue mawazo yako yamewekwa kwenye safe ya maisha. Ukiona unashambuliwa sana jua umekomaa. Sie wengine ilifikia hata kiongozi wa mafisadi kuuliza huyu kwanini anafanya hivi badala ya kuhoji uoza wake. Kama sikosei wanataka uwe kama mbwa mwitu waitwao waandishi wa habari waliochuuza taaluma wakachagua kujiuza kama vyangudoa wa Ohio ili wazawadiwe mabaki ya vyeo hasa ukuu wa wilaya ambao umegeuka mradi wa wachumia tumbo na vyangudoa wauza nyuchi. Naona kaka nisiseme mengi. muhimu kaza buti utwange na kupeta na kupetuka.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.