24 Nov 2010


Mwandishi Wetu
Novemba 24, 2010
Polisi Uingereza wamchunguza mwanawe
Washitushwa na uhamishwaji wa Sh.bil. moja
MTOTO wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa anayeitwa Frederick Lowassa anachunguzwa na Kitengo Maalumu cha Polisi wa Kimataifa wa Uingereza wanaofuatilia utata wa uhamishaji fedha kutoka Tanzania, Raia Mwema limedokezwa.

Fedha hizo zinahusishwa na ununuzi wa nyumba yenye thamani ya pauni za Uingereza 475,000 (takriban Shilingi bilioni moja) katikati ya Jiji la London, .

Hata hivyo, watu walio karibu na Frederick wameelezea kwamba kijana huyo hakuwahi kununua nyumba; bali aliwahi kutaka kupanga kwa ajili ya kuishi akiwa masomoni nchini Uingereza na fedha nyingine alizituma kwa ndugu yake aishie nchini humo.

Nyumba ambayo inatajwa katika maelezo ya awali iko mtaa wa Leinster Gardens, jijini London.

Hata hivyo, hakuna ofisa yeyote wa Serikali ya Tanzania aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo, pamoja na kuwapo taarifa kwamba tayari vyombo vya dola vya Tanzania vimekwisha kuhusishwa katika uchunguzi huo.

Maofisa wa Polisi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID) wanaohusika na uchunguzi wa fedha haramu, wamekwepa kuzungumzia suala hilo na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, hakuweza kupatikana, na alielezwa kuwa nje ya nchi kikazi.

Ofisa wa CID aliyeelezwa kuongoza kitengo kinachochunguza makosa ya uhalifu wa fedha na nyaraka, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Samson Kasala, alikanusha kufahamu chochote kuhusiana na suala hilo, kabla ya kukata simu alipohojiwa na Raia Mwema kuhusu taarifa hizo.

Taarifa zinaeleza kwamba Kitengo cha Ufuatiliaji wa Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit-FIU) kilichopo chini ya Wizara ya Fedha nchini, kilipokea taarifa kutoka Polisi wa Kimataifa wa London, Uingereza, wakitaka taarifa muhimu kuhusiana na Frederick, kabla ya kitengo hicho kuomba msaada wa polisi.

Hata hivyo, Kamishna wa FIU, Herman Kessy, hakuweza kupatikana wiki iliyopita akielezwa kuwapo nchini Afrika Kusini kikazi, lakini hata aliporejea wiki hii Raia Mwema ilikosa ushirikiano kutoka kitengo hicho Jumatatu wiki hii.

FIU imeanzishwa chini ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (Anti-Money Laundering Act-2006) kwa kuundiwa kanuni mwaka 2007, lakini hadi sasa kitengo hicho kimekuwa kikiendeshwa na maofisa watano tu, Kamishna Kessy, mchambuzi mmoja, mtaalamu wa mawasiliano na wasaidizi wawili wasio wataalamu, kitengo kilichopaswa kuendeshwa na watu wengi zaidi kutokana na unyeti wake.

Habari zinaeleza kwamba hata ofisa wa Polisi aliyewahi kuhamishiwa FIU kwa kazi maalumu alijikuta akitengwa na kutopangiwa kazi na maofisa hao ambao wengi wanatoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baada ya kuwa ‘wameaminiwa’ sana na uongozi wa juu wa serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo bado zinafanyiwa kazi, Frederick ambaye baba yake alijiuzulu Waziri Mkuu kwa kuhusishwa na kashfa ya ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyokabidhiwa kwa kampuni tata ya Richmond Development LLC, anadaiwa kufanya mawasiliano kupitia kampuni ya uwakala iliyotajwa kwa jina la ‘Mishcon’.

Nyaraka alizowasilisha, zilidai kuwapo ubia kati ya mtuhumiwa huyo na kampuni tatu ikiwamo Integrated Property Investment(T) Ltd na Barare Ltd Company.

Mkataba huo unaonyesha kuwa Frederick Lowassa ana hisa kwenye kampuni hizo, na kwamba fedha za ununuzi wa nyumba hizo zinatokana na fedha za malipo ya hisa anazopata kutokana na kampuni hizo.

Hata hivyo, mkataba huo unaonyesha kusainiwa Machi 25 mwaka 2009 siku moja baada ya Frederick Lowassa kusaini mkataba kati yake na kampuni ya Mishcon kama wakala wake katika ununuzi wa jengo hilo.

Pia aliwasilisha nyaraka zinazoihusisha kampuni ya Alphatel kama moja ya kampuni ambayo pia yeye ni mkurugenzi wake ambayo pia ni chanzo chake kingine cha fedha anazotumia kununua jengo hilo.

Taarifa zimedokeza kuwa ununuzi huo ulikwama baada ya kushindwa kutoa malipo hayo kwa mujibu wa mkataba kati yake na wakala wa ununuzi wa nyumba hiyo (kampuni ya Mishcon) ambao ulimtaka awe amekamilisha kulipa fedha hizo kabla ya Aprili 14, mwaka 2009.

Hata hivyo, siku chache baadaye ndani ya mwezi huo wa Aprili, Frederick aliipelekea Mishcon kiasi cha pauni za Uingereza 199,940 zikitokea kwenye kampuni ya ununuzi fedha ya Wall Street Exchange.

Aidha kiasi cha pauni 100,000 kiliingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo hiyo ya Mishcon kwa fedha taslimu katika mikupuo 12 tofauti zikitokea kwenye matawi tofauti ya benki ya NatWest Bank plc iliyoko Kaskazini mwa Jiji la London.

Raia Mwema limeelezwa kuwa mazingira ya kuingizwa fedha hizo kwenye akaunti ya wakala huyo ( Mishcon) ndiyo yameifanya Taasisi ya SCD 6 Economics and Specialist Proceeds of Corruption Unit ya Uingereza inayosimamia uchunguzi wa sakata hilo kuwa na mashaka makubwa kuhusu uhalali wa fedha hizo.

Kutokana na mazingira hayo, SCD 6 Economic and Specialist Crime Proceeds of Corruption Unit yenye ofisi zake Victoria Block, New Scotland Yard, London, ililazimika kuwasiliana na FIU ikitaka maelezo ya awali kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi kuhusu fedha hizo.

Raia Mwema iliwasiliana na Fred ambaye alikana kununua nyumba Uingereza lakini alikiri kuwahi kutuma fedha huko. Aliliambia Raia Mwema pia kwamba hajawahi kuhojiwa na yeyote kuhusu suala hilo, na pia kwamba hana taarifa kuwa polisi wa Uingereza wanampeleleza.

Hata hivyo kwa upande mwingine, gazeti hili limebaini kuwa, maelezo ya awali ambayo yalitakiwa kutoka Tanzania na makachero hao wa Uingereza, ni pamoja na kutaka kufahamu kama kweli Frederick Edward Lowassa amezaliwa Agosti 26, 1977, Mwanza Tanzania na anamiliki hati ya kusafiria yenye namba AB 109402 iliyotolewa Tanzania na kwamba anwani yake nchini Uingereza ni 71 Hendrix Drive, Milton Keynes, MK8 0DY.

Pia makachero hao waliitaka Serikali ya Tanzania kutoa ufafanuzi wakitaka kujua kama Frederick Lowassa ni mbia katika kampuni za Alphatel Partnership (Tanzania) Barare Ltd na Intergrated Tanzania Limited, kampuni ambazo zimefahamika kumilikiwa na familia ya Lowassa.

Asasi hiyo ya Uingereza pia imeomba kujua kama FIU wana taarifa zozote za uhalifu dhidi ya Frederick Lowassa na kama baba yake Edward Lowassa anachunguzwa kwa tuhuma yoyote ya rushwa na mamlaka za uchunguzi wa rushwa nchini Tanzania kuhusu fedha haramu.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na vyombo vya dola, ulielezwa na taarifa hizo kwamba Frederick Lowassa si mbia katika kampuni hizo na kwamba Barare Ltd wenye hisa ni Edward Ngoyai Lowassa mwenye hisa 500 na Regina Mumba Lowassa mwenye hisa 500 huku wakurugenzi wakiwa ni hao hao.

Ofisa wa Uingereza anayesimamia uchunguzi huo, George Simpson, ameliambia Raia Mwema kupitia barua pepe kwamba kanuni za uchunguzi kuhusiana na kesi zenye mguso wa kisiasa huwazuia kukanusha au kuthibitisha kuhusu uchunguzi unaoendelea hadi pale wanapofikia hatua ya kukamata mtuhumiwa ama anapofikishwa mahakamani.

CHANZO: Raia Mwema

1 comment:

  1. MUDA UMEFIKA MPAKA UMEPITILIZA! HATA KAMA KUNA UOGA, KUNYENYEKEA SO CALLED WAKUBWA, NA UGONJWA WA FIKRA TANZANIA,LAKINI YANA MWISHO, HAO WATOTO WA WAKUBWA WANAISHI MAISHA YA JUU WAKIDHANI OOH DADDY PROVIDE! WAKATI DADDY NI MWIZI?! HII NI JASHO LA MNYONGE AMBAYE HANA SAUTI HAPO, MAISHA YAKE KILA SIKU NI'JAMANI NISAIDIENI'!! NI AIBU SAANA KWA KIONGOZI KUJILIMBIKIZIA MAHELA YA WATU, NA KUJIFAIDISHA YEYE NA FAMILIA YAKE! KWA MTU YEYOTE MWENYE KUAMINI MUNGU NI DHAMBI KUBWA, VIONGOZI WETU WAMETAPAKAA DAMU HATIA INAYOENDELEA KUMWAGIKA! LAKINI HUKUMU YAJA, HAWAWEZI KUKIMBIA, KILA SEHEMU WATAMULIKWA, WAO NA VIZAZI VYAO, TUMECHOKA NA SHIDA, NI KUWAVUMBUA TU, MAANA NI PESA ZETU HIZI, MALI YA WATANZANIA, NCHI MASIKINI KWA JINA WAKATI NI TAJIRI KWA WACHACHE!!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.