18 Jan 2011


Kilichonisukuma kuandika post hii ni habari niliyoiona kwenye runinga katika kipindi cha Anderson Cooper 360 (katika kituo cha CNN) kwamba mwanabodi wa taasisi moja ya elimu huko Marekani amekuwa akimshambulia mwanaharakati Dkt Martin Luther Jr,ambaye jana ilikuwa siku ya kumbukumbu yake (Martin Luther King Jr Day).

Mashambulizi hayo dhidi ya Dkt King yalijumuisha madai kama "mwanaharakati huyo hakuwa Dokta"-ikimaanisha si sahihi kuweka kitangulizi hicho kabla ya jina lake,na "alikuwa mkomunisti"- na kwa wahafidhina nchini Marekani,ukomunisti unachukuliwa kama Unazi.

Tukio hilo ni mwendelezo tu wa mashambulizi dhidi ya Dkt King hususan kutoka kwa wanaokumbatia hisia za ubaguzi wa rangi.Lakini kama kuna mtu aliyekuwa "obsessed" zaidi na jitihada za kumuumbua Dkt King basi si mwingine bali Mkrugunzi wa zamani wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) J.Edgar Hoover.Inaelezwa kuwa shushushu huyo alijitahidi kadri alivyoweza kufanikisha azma yake hiyo muflis,ikiwa ni pamoja na kurekodi (bugging) maongezi ya Dk King anayetambulika kama chachu ya mapambano (ya amani) na mafanikio ya Wamarekani Weusi kukubalika katika nchi hiyo (kwa kiasi kikubwa).Hata mafanikio ya  Barack Obama,Mweusi wa kwanza kushika nafasi ya urais wa Marekani yanahusishwa kwa kiasi kikubwa na harakati na changamoto zilizoanzishwa na Dkt King.

Tanzania yetu ya leo inaweza kabisa kulinganishwa na hali ilivyokuwa katika Marekani ya enzi za akina Dkt King ambapo ubaguzi wa rangi ulikuwa umeshamiri vilivyo.Huko nyumbani,na hasa baada ya kifo cha Baba wa Taifa-aliyekuwa muumini mkubwa wa usawa wa binadamu-wengi wa wanasiasa wetu wamekuwa bize kutengeneza mgawanyiko katika jamii kati ya wenye nacho na wasio nacho,vigogo na walalahoi,na katika zama hizi za Kikwete,tumeshuhudia mgawanyiko mkubwa zaidi katika jamii; mafisadi dhidi ya wananchi wa kawaida,na hivi karibuni CCM,Serikali yake na vyombo vyake vya dola dhidi ya wananchi na wapinzani (hususan Chadema) na haki zao.

Lakini pengine la kutisha zaidi ni vuguvugu linalochochewa na CCM ya Kikwete na mafisadi anaowalea la kuwagawanya Watanzania kwa misingi ya imani zao za kidini.Kila mwenye macho na masikio ameona na kusikia kauli mbalimbali za msigishano kati ya viongozi wa CCM na baadhi ya viongozi wa Kanisa kwa upande mmoja,na kwa upande mwingine ni msuguano (unaoelekea kukua) wa kimtizamo kati ya baadhi ya viongozi wa Kanisa na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam.

Kama ambavyo nimerejea kwenye posts na makala zangu kadhaa huko nyuma,suala hili tofauti za kidini kutumika kwa maslahi ya kisiasa linanigusa sana,kitaaluma kama mwanafunzi wa utafiti katika mahusiano ya siasa na dini,na kama raia wa Tanzania-nchi ambayo licha ya kuwa na viungo (recipes) vinavyoweza kupelekea mgogoro wa kijami kwa misingi ya kidini,angalau hali kwa ujumla imekuwa salama (kwa maana ya kutokuwepo vurugu za aina hiyo).

Inapofikia mahala vyombo vya habari vya umma,kama TBC1,Habari Leo na Daily News,vinatumika kusambaza ujumbe wa kuchochea mvurugano katika jamii badala ya kuhamasisha maelewano,ni dhahiri kuwa tunakoelekea si kwema.Vyombo hivi vya habari vinavyoendeshwa kwa fedha za walipakodi pasipo kujali itikadi zao za kisiasa vinaanza kuchukua mwelekeo wa gazeti la Kangura na vituo vya radio vya Radio Rwanda na Radio Télévision Libre des Mille Collines (RTLM) ambavyo vilichangia sana kuhamaisha propaganda za chuki dhidi ya Watutsi zilizopelekea mauaji ya kimari nchini Rwanda kati ya mwaka 1994-95.

                                                                                    



Hivi kama blogu binafsi  ya Ze Utamu ilipigwa kufuli kwa vile tu ilionyesha picha isiyofaa ya Rais Kikwete,kwanini basi vyombo hivyo vya habari vya umma vinaruhusiwa kuchochea chuki miongoni mwa Watanzania ambapo madhara yake ni makubwa zaidi ya namna picha za Ze Utamu zingeweza kumdhalilisha Kikwete?Hapa sio kama naitetea blogu hiyo bali ninachojaribu kupigia mstari ni ukweli kuwa amani ya Watanzania inayowekwa rehani na TBC1,Habari Leo na Daily News ina umuhimu na thamani kubwa pengine zaidi hadhi ya Kikwete pekee.Ikumbukwe kuwa wakati jitihada za Serikali kuitia kufuli Ze Utamu zilipelekea picha hizo kutoonekana tena,sumu inayomwagwa na vyombo hivyo vya habari vya umma ikishasambaa hakutakuwa na namna ya kuizuwia.

Nirejee kwa Dkt King na funzo linaloweza kusaidia katika harakati za mapambano dhidi ya udhalimu wa Kikwete na CCM yake inayoendeshwa kishkaji.Pamoja na jitihada na nguvu kubwa iliyotumika kumdhibiti,na hatimaye kuuawa,mbegu alizopanda mwanaharakati huyo zimefanikiwa kuzalisha watu kama Obama,Oprah,Condoleeza Rice,Collin Powell,nk ambao kwa hakika wasingeweza kujichomoza katika mfumo wa kibaguzi uliowabagua Weusi katika kila nyanja ya maisha nchini Marekani.

Kama ambavyo Dk King aliandamwa na FBI na J.Edgar Hoover ndivyo wazalendo kama Dkt Wilbroad Slaa walivyojikuta wakiandamwa na taasisi za serikali katika kila wanalofanya,huku baadhi ya waendaji wa taasisi hizo wakidiriki hata kuvunja "miiko" waliyojiwekea ili waweze kumshamshambulia Dkt Slaa (rejea kauli ya Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka).Na kama ambavyo wabaguzi wa rangi wanavyoendelea kubomoa misingi iliyowekwa na Dkt King,ndivyo Kikwete akisaidiwa na mafisadi anaowalea-plus vyombo vyao vya habari-wanavyofanya kila wawezalo kudhoofisha harakati za kuwakomboa Watanzania kutoka katika himaya ya ufisadi,ukiukwaji haki za binadamu na umasikini wa kupindukia.

Usihadaike na kauli za watu kama Lowassa wanajifanya kutahadharisha kuwa mjadala wa Katiba mpya usiwe chanzo cha kuhaarisha amani kwani yayumkinika kuamini kuwa wale wote wanaohusishwa na ufisadi wasingependelea kuona tunakuwa na Katiba mpya inayompa mamlaka mwananchi wa kawaida kuwa mwenye nchi halisi badala ya hali ilivyo sasa ambapo nchi yetu imekuwa kama kampuni binafsi ya mafisadi,wakiipelekesha watakavyo na sheria zikibaki sheria tu isipokuwa katika kukandamiza maandamano ya amani na kuminya haki za binadamu.


Licha ya kuuawa kwake,wengi wa Wamarekani Weusi sasa wanafaidi matunda ya harakati za Dkt Martin Luther King Jr.Vikwazo na upinzani wa kila hali dhidi ya harakati hizo hakukumvunja moyo Dkt King,na hata kifo chake hakiwazuia washirika na watangulizi wake kuendeleza harakati hizo za kudai usawa wa binadamu.Damu ya mashujaa iliyomwagika huko Arusha kutokana na unyama waliofanyiwa na polisi wa Kikwete na IGP Mwema isipotee bure bali iwe chemuchemu ya kudumu kuhakikisha kuwa hatimaye udhalimu na ufisadi wa CCM na serikali yake unakomeshwa completely.

Kama Dkt Martin Luther King Jr aliweza,na Nelson Mandela akaweza pia-bila kusahau kuwa nasi pia tuliweza kumwondoa mkoloni na kumfurumisha nduli Idi Amin-basi kwa hakika harakati hizi za sasa zinaweza pia kufanikisha ndoto na malengo yetu ya kuwa na Tanzania tunayostahili kuwa nayo,na sio hii ya sasa inayoendeshwa kwa remote control na mafisadi huku wakiwatuza majambazi wa Dowans kwa mabilioni na "kuwazawadia" waandamaji wa amani risasi za kuwaua na kuwajeruhi.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.