24 Feb 2011


Maandamano ya kupinga tawala dhalimu,ambayo yamesambaa maeneo kadhaa ya Afrika Kaskazini,yanaanza kuonyesha dalili za kusambaa sehemu nyingine za bara la Afrika hadi Cameroon,Gabon,Zimbabwe na Mauritania.


Nchini Cameroon,kulikuwa na mpango wakufanya maandamano jana kwa lengo la kumwondoa madarakani Rais Paul Biya,kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani.Biya amekuwa madarakani kwa miaka 28.Kiongozi wa upinzani,Kah Walla,aliieleza CNN kwamba kundi lake linataka kuona chaguzi huru na za haki.

Mwandishi wa gazeti la New York Times la Marekani,Nick Kristof, aliandika kwenye Twitter kwamba:

Mapambano ya kudai demokrasia yanasambaa maeneo mapya barani Afrika: Cameroon,Gabon,Zimbabwe,Mauritania.
Naye Msemaji wa Serikali ya Marekani P.J Crowley alitwiti

Wanaharakati wakutana Zimbabwe kujadili yaliyojiri Misri na Tunisia na wameishia kukamatwa.Mugabe hajaelewa somo
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari inaripoti kwamba Eritrea,Guinea ya Ikweta na Zimbabwe wamedhibiti kabisa maendeleo ya mapambano ya kung’oa tawala dhalimu huko Mashariki ya Kati na Afrika Magharibi.

Habari zaidi kutoka CNN zinaeleza kuwa wanaharakati na viongozi kadhaa wa vya vyama vya wafanyakazi nchini Zimbabwe walizingirwa na polisi wiki iliyopita na sasa wanakabiliwa na hukumu ya kifo baada ya waendesha mashtaka wa serikali ya nchi hiyo kuwasomea mashtaka ya kupanga maandamano ya kuung’oa madarakani utawala wa Rais Robert Mugabe.

Katika kesi hiyo iliyoendeshwa jana,washtakiwa 46 wanakabiliwa na shtaka la uhaini .Walikamatwa Jumapili iliyopita baada ya mamlaka kudai kuwa walikutwa wakiangalia mikanda yenye kuonyesha maandamano yaliyopelekea kung’olewa madarakani aliyekuwa Rais wa Tunisia Zine El Abidine Ben Ali na mwenzie wa Misri Hosni Mubarak.

Mtandao wa habari wa Afrol unaripoti kufanyika kwa maandamano ya nchini nzima huko Cameroon kushinikiza Rais Biya aondoke madarakani ,japokuwa maandamano hayo yalidhibitiwas kirahisi na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Miji mikubwa ya Younde na Douala ilitawaliwa na askari wa kutuliza ghasia huku magari yakisimamishwa na kupekuliwa na mikusanyiko ya watu ikidhibitiwa.Kadhalika,mashuhuda wameeleza kuwa polisi walinyang’anya kamera na simu za mikononi.
Wachambuzi wa mambo wanadai kuwa licha ya maandamano hayo kutofanikiwa kufikia matarajio ya wengi,bado kuna uwezekano wa yaliyojiri sehemu kama Tunisia na Misri kujitokeza nchini Cameroon hivi karibuni.Kilio cha wananchi wengi wa taifa hilo ni rushwa na hali ngumu ya maisha.Harakati za kudai mabadiliko nchini humo zinachochewa zaidi na Wakameruni wanaoishi nje ya nchi hiyo.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.