11 Mar 2011


Hivi kwanini watawala wetu wanaogopa sana maandamano?Wakati mchecheto ulioikumba Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na CCM yake (kutokana na maandamano ya amani ya Chadema) haujaisha,gazeti la Mwananchi linaripoti kuwa askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wamezuia maandamano ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam

Soma habari kamili hapa chini:

KIKOSI cha Kutuliza Ghasia cha Jeshi la Polisi (FFU) jana kilitawanya maandamano ya wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam waliokuwa wakielekea Ikulu kupinga ongezeko jipya la nauli za daladala.

Kundi la kwanza la wanafunzi hao lilijikusanya katika Viwanja vya Mnazi Mmoja majira ya mchana na kuanza maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la kumfikishia ujumbe Rais Jakaya Kikwete wa kutoridhishwa na ongezeko hilo la nauli. Kundi jingine la wanafunzi lilianzia maandamano hayo katika Uwanja wa Karume.

Mwandishi wa habari hii alipofika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja aliwakuta wanafunzi hao wakijipanga kuanza maandamano hayo huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali. Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: ‘Kama ni maji ya pilipili, hayawezi kuwa suluhisho la migomo.’

Baadhi ya wanafunzi walisema wameamua kupinga nauli hiyo mpya kwa maandamano ili kuishinikiza serikali iifute wakitaka kurejeshwa kwa ile ya zamani ya Sh100 ili kuwapunguzia mzigo wazazi wao kuwasomesha.
“Sisi wengine kwa siku tunapanda magari matatu hadi kufika shule na hapo bado hujala. Sasa kwa hali hii kweli tutasoma?" Alihoji mmoja wa wanafunzi hao.

Mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Habib Juma alisema nauli ya Sh150 kwa mwanafunzi ni kubwa mno kuimudu akisema kipato cha wazazi wengi ni duni na baadhi yao wanashindwa hata kutoa michango mbalimbali ya shule.

Hata hivyo, jitihada za wanafunzi hao kufikisha ujumbe wao Ikulu ziligonga mwamba baada ya kudhibitiwa na FFU muda mfupi tu baada ya kuingia barabarani.Askari hao waliokuwa na pikipiki walitanda barabarani na kuwatawanya wanafunzi hao na baadaye waliwashikilia wanafunzi wawili wa kiume baada ya wenzao kukimbia. Wanafunzi hao walipakiwa kwenye gari la polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi.

Nauli hizo mpya za daladala zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), wiki iliyopita zilianza kutumika rasmi jana.Ofisa Mfawidhi wa Sumatra katika Kanda ya Dar es Salaam, Conrad Shio alisema nauli hizo zimegawanywa katika makundi matatu kwamba wanafunzi watatozwa Sh150 kwa safari, kundi la pili ni njia zenye nauli moja ya Sh300 na la tatu ni la njia zenye nauli zaidi ya moja na kwamba nauli hizo zimeongezeka kwa Sh50 katika nauli za awali, katika kila safari moja.

Shio alitoa mfano akisema kwa njia ambayo abiria wake walikuwa wanatozwa nauli ya Sh250 kwa safari, sasa watatozwa Sh300.Alisema katika Kanda ya Mashariki nauli ya juu zaidi itakuwa Sh1,700 kwa safari kati ya Kigamboni na Pembamnazi, eneo ambalo awali nauli yake ilikuwa Sh1,300.

Sumatra imeongeza nauli hizo baada ya kupokea maombi ya wamiliki wa mabasi mwishoni mwa mwaka jana wakilalamikia kupanda kwa gharama za uendeshaji.

ANGALIZO: Ubabe huzaa ubabe.Kama watawala wetu wanadiriki kutumia ubabe hadi kwa wanafunzi wa shule za msingi na serikali,basi tukae tukijua kuwa tulipo na tuendako si salama.Maandamano ni haki ya msingi ya kila mwananchi alimradi hayahatarishi amani.Hivi kuna ugumu gani kwa askari kutoa escort kwa waandamanaji hadi watapowasilisha ujumbe wao kunakohusika na kisha kuwasihi warejee makwao kwa amani?

Hizi ni dalili za wazi za udikteta kwa kisingizio cha kulinda amani na utulivu.

1 comment:

  1. Ukiritimba usiokuwa na mipaka, lakini yote haya yanatokea kwasababu ya serikali kukosa kujiamini na kutokuwa na dira na mwelekeo sahihi. Mwisho wa siku wanaishia kujihami kwa kutumia misuli badala ya kutatua kero za waandamanaji kwa njia ya majadiliano.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube