15 Mar 2011


Kuna kila dalili kuwa chama tawala CCM sasa kinajiendesha kwa mtindo wa bora liende.Asubuhi utasikia huyu karopoka hili,mchana utamsikia mwingine karopoka lile,alimradi ni vurugu mechi kila siku.

UVCCM hawana mamlaka kutung'oa-Chiligati
*Makamba asema hayo ni maoni ya vijana
*Lowassa ahoji nani asiyeona uchumi ulivyo?

Na John Daniel
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Maponduzi (NEC) Itikadi na Uenezi, Bw. John Chiligati amesema licha ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kuwa na haki ya kutoa maoni, lakini hawana mamlaka ya kuiondoa sekretarieti madarakani.

Wakati Bw. Chiligati akitoa kauli hiyo, wajumbe wenzake wa sekretarieti waliotakiwa kuachia ngazi kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa 'kumsaidia' mwenyekiti wametofautina kuhusu kauli hiyo huku wakishindwa kuzungumzia kwa uwazi wito huo wa vijana.

Jana gazeti hili liliwakaririwa vuoa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ukiitaka sekretarieti ya chama hicho kujizulu kabla umoja huo haujachukua hatua za kuwaondoa kwa kuwa imeshindwa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo wa mkoani Pwani, Bw. Abdallah Ulega wakati akifungua Baraza la Umoja wa Vijana Mkoa humo, huku akisisitiza kuwa sekretaeti hiyo haifai kwa kuwa ilisababisha chama hicho kushinda kwa taabu katika uchaguzi mkuu uliopita, na kuwa ndiyo imekuwa ikitoa siri kwa chama cha upinzani cha CHADEMA.

Secreterieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba, inajumuisha Manaibu Katibu Wakuu Bara, Kapteni George Mkuchika na Salehe Ramadhani Ferouz (Zanzibar), Katibu wa Itikadi na Uenenezi, Kapteni John Chiligati, Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha, Bw. Amos Makala na Katibu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe.

Akizungumza na Majira jana Bw. Chiligati alisema kimsingi vijana hao wametumia uhuru wao ndani ya chama kutoa maoni yao na kwamba haoni sababu ya hatua hiyo kusumbua vichwa vya watu kwa kuwa ni jambo la kawaida kikatiba.

"Ni haki yao kutoa maoni, sioni cha ajabu hapo, vijana wana haki ya kuzungumza na kutoa maoni yao kwa uhuru kabisa.

"Lakini Secretarieti inachaguliwa na NEC na tunawajibika kwa NEC kupitia Kamati Kuu, hao waliotuchagua ndio wana mamlaka ya kutuondoa, lakini hilo haliwakatazi vijana kutoa maoni," alisema Bw. Chiligati.

Alipoulizwa changamoto waliyopata na iwapo wanajiandaa kuwasilisha mapendekezo yao kwenye vikao vya juu kutokana na wito wa UVCCM hakuwa tayari kutoa majibu ya moja kwa moja badala yake alisisitiza kuwa hayo ni maoni ya vijana.

"Nimesema hayo ni maoni ya vijana na wana haki ya kuyatoa," alisistiza Bw. Chiligati bila kufafanua.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba alisema licha ya kuheshimu uhuru wa kutoa maoni lakini haamini kama yaliyoandikwa katika vyombo vya habari ndiyo yaliyozungumzwa na UVCCM mkoa wa Pwani.

"Hayo ndio maoni ya vijana, wamekaa kwenye baraza lao na wakaona hivyo. Hayo ndio maoni yao mimi sina cha kusema," alisema Bw. Makamba.

Alipotakiwa kujibu iwapo katiba, kanuni na taratibu za CCM zinatoa nafasi kwa umoja huo kuondoa secretarieti iwapo imeshindwa kutimiza wajibu wake alisema;

"Ni maoni yao, lakini pia sina hakika kama yaliyoandikwa yako sawa sawa," alisema Bw. Makamba bila kutoa ufafanuzi wa kina.

Alipoulizwa hatua atakazochukua kama Mtendaji Mkuu wa CCM kuhusu wito huo wa UVCCM alisema yeye hawezi kujitetea kupitia magazeti na kusisitiza kuwa hayo ni maoni ya vijana.

"Siwezi kufanya kazi ya kujitetea kwenye magazeti, wao ni vijana wa CCM, wamekaa kwenye baraza lao wakasema, sasa unataka nisema nini? alihoji Bw. Makamba na kuongeza, "Nasema hivyo ndivyo walivyoona. wajumbe wengine wa sekretarieti hiyo hawakupatikana kutoa maoni yao kwa simu zao zilikuwa zinaita bila majibu.

Mbali na sekretarieti, vijana hao waliwashambulia mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye wakisema kauli zao za kukikosoa chama hazina lengo zuri bali ni njia tu ya kutafuta urais 2015

Akizungumzia suala hilo, Bw. Lowassa ambaye pia alionywa na vijana hao kutoa maoni nje ya vikao wakati anayo nafasi ya kukutana na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Rais Jakaya Kikwete, alisema maoni yake kuhusu uchumi hayana sababu ya kusubiri vikao.

"Nilikuwa vijijini kwenye ziara sijasoma magazeti, lakini wewe nikikuuliza hali ya uchumi utasema kuwa ni nzuri?Nani asiyejua kuwa kuna hali ngumu ya uchumi! Hata bei ya nyanya imependa hilo nalo tusubiri vikao? alihoji Bw. Lowassa.

Alisema kama mtu anataka kuwania urais mwaka 2015 hawezi kuanza kampeni kwa sasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kutoa nafasi ya kushughulikiwa na kuchafuliwa na maadui. Bw. Sumaye hakupatikana jana kwenye simu yake.

Majira ilipomtafuta Makamu Mwenyekiti Taifa wa CCM, Bw. Pius Msekwa ili kuzungumzia wito huo wa UVCCM, alisema hawezi kusema lolote kwa kuwa hayo ni maoni ya vijana na kila mmoja anayo haki ya kutoa maoni yake.

"Hayo ni maoni ya vijana, sasa unataka nitoe maoni gani?" alihoji Bw. Msekwa. 

CHANZO: Majira

3 comments:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.