3 Aug 2011

Chuwit kama kuwadi kubwa lao (master pimp)

Wanaposema siasa ni mchezo mchafu hawaongopi: Bango la  Chuwit wakati wa kampeni za uchaguzi

Pengine ushasikia msemo wa Kiingereza usemao "in the long run it is experience that counts." Kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili ni kwamba uzoefu unalipa.Kadhalika,naamini utakuwa umeshasikia matukio ambapo mwizi mstaafu anatumika kukamata wezi waliopo.Hii ni moja ya mbinu muhimu sana kwa polisi na watumishi wengine wa taasisi za usalama.

Lakini ishu hii imechukua sura mpya huko Thailand baada ya tajiri mstaafu wa biashara za umalaya,Chuwit Kamolvisit,kujiingiza kwenye siasa na hatimaye kufanikiwa kuwa mbunge.Mbunge huyo ambaye anadai angependa zaidi kuitwa kuwadi (pimp)kuliko mwanasiasa ameingia kwa kasi ya kipekee kwenye siasa akidhamiria kupambana na tatizo la rushwa katika nchi hiyo inayosifika kwa utalii wa ngono (sex tourism).

Chuwit alikuwa tajiri anayemiliki massage parlour (sijui neno la Kiswahili ni lipi) na vyombo kadhaa vya habari vinamtaja kama kuwadi kubwa lao (super pimp) mstaafu.Anadai kuwa ili kumudu biashara chafu kama yake ilimlazimu kuwahonga polisi mara kwa mara kwa minajili ya kukwepa mkono mrefu wa sheria (si mrefu kihivyo,anyway).Sasa baada ya kuingia kwenye siasa anataka kutumia uzoefu huo wa kukwepa sheria kwa kutumia rushwa kupambana na rushwa.

Awali,mwanasiasa huyo alichapisha kitabu alichokipa jina lenye utata la Dogstyle Politics (yaani,ashakum si matusi,"Siasa za Chuma Mboga".Katika kitabu hicho,Chuwit anatoa mwanga kuhusu mwenendo wa siasa za nchi hiyo kulingana na uzoefu alioupta wakati wa uchaguzi,Anazilinganisha tabia za wanasiasa na mbwa.Lakini anadai baadhi ya vyama vya siasa vinapaswa kufananishwa na nyoka mwenye sumu kali Cobra,kwani havina itikali wala msimamo na ni hatari zaidi ya mbwa.Katika kitabu hicho,mwanasiasa huyo mwenye vituko ameandika shairi lisemalo, "Kuna tofauti gani kati ya binadamu na mbwa?Hawezi kuongea-mbwa hadanganyi,na mapenzi ya kweli ya mbwa ni kwa mmiliki wake"

Binafsi nadhani watu kama Chuwit wanahitajika sana katika Tanzania yetu iliyogubikwa na ufisadi.Hebu pata picha mtu kama Rostam Aziz aamue kwa dhati kuanzisha vita dhidi ya mafisadi.Kwa mfano aanze na namna mtandao uliomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete ulivyoundwa,fitna walizofanya kusafisha njia ya Ikulu,madili kama ya EPA,Richmond na Dowans yalivyofanikishwa na michezo mingine michafu inayoipa uhai CCM na serikali yake!

Au chukulia mfano Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge aamue "liwalo na liwe" na kumwaga "chenga hadharani" kwa kuufahamisha umma jinsi mikataba ya kijambazi inavyofanikishwa na kurutubisha ufisadi.Au pengine Edward Lowassa baada ya kuona "anazinguliwa" aamue kuwa "bora tufe wote" na kuweka hadharani kila baya analojua linalosababisha Tanzania kuendelea kuwa kichaka cha ufisadi huku maisha ya Mtanzania wa kawaida yakizidi kuwa duni tofauti na danganya toto za Kikwete za "maishabora kwa kila Mtanzania (nadhani alimaanisha 'kwa kila fisadi')

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.