7 Sept 2011

Ndugu zangu,Ndani ya siku tatu za kupiga kura kwenye Pima-Maji ya Mjengwa.blogspot.com watu 165 wameshatumbukiza kura zao. Matokeo mpaka dakika hii ni Joseph Kashindye wa CHADEMA anayeongoza kwa kura 116 akiwa amejinyakulia asilimia 70 ya kura zote. Anayefutia ni Dr. Peter Kafumu wa CCM mwenye kura 39 sawa na asilimia 23 ya kura zote. Wa tatu ni Leopard  Mahona wa CUF mwenye kura 10 sawa na asilimia 6 ya kura zote.

Tafsiri yangu;
Huu utakuwa mpambano mgumu mpaka dakika ya mwisho. Kwamba leo Jumanne wagombea wa vyama saba vya upinzani wamerudisha fomu si habari njema kwa CHADEMA. Tayari katika hatua hii ya kura za maoni za Watanzania wa mtandaoni tunaona CUF kwa namna moja au nyingine imepunguza kura za CHADEMA kwa asimilia 6. 

Laiti CUF na vyama vingine vya upinzani vingeiachia CHADEMA ipambane na CCM na huku vyama hivyo vikiipa sapoti CHADEMA, basi, CCM wangekuwa na kibarua kigumu zaidi kulibakisha jimbo la Igunga mikononi mwake. 

Na kama mgombea wa CHADEMA atabaki kwenye asilimia 60 au 70 ya ushindi siku tatu kabla ya uchaguzi, basi, Peter Kafumu wa CCM anaweza kabisa kuapishwa kuwa Mbunge wa Igunga kwenye Bunge la Kumi na Moja mwezi Novemba. Kwanini? CCM ni mabingwa wa ' kuokoteza' kura kwenye siku za mwisho za kampeni, kwa mbinu zote. Hivyo basi, kumfanya mgombea wao aibuke kidedea.

Na Siku tatu zijazo zitatoa picha zaidi juu ya hali ilivyo kwenye uwanja wa mapambano ya kisiasa kule Igunga.  CHADEMA watazindua rasmi kampeni zao, alikadhalika CCM na CUF. Hotuba za uzinduzi na mwitikio wa Wana Igunga kwa kila chama kitapozindua kampeni zake unaweza kutusaidia kutafsiri mwelekeo.

Naingiwa na hofu. Kwanini?
Kuwa Igunga inaweza pia kuwa kwenye hatari ya vurugu za kisiasa kama zilizotokea Tarime. Ni kwa vile CCM, CHADEMA na CUF vyote vimeikamia Igunga. Na itangulizwe busara na maslahi ya taifa.
Msomaji unakumbushwa. Nini tena?
Kuwa Pima-Maji ya Mjengwablog juu ya kinyang'anyiro cha Igunga bado inaendelea. Itumie blogu yako ya jamii shirikishwa ili utoe maoni yako.  Zimebaki siku tatu za kupiga kura kabla kituo cha kupigia kura kufungwa. Piga kura yako sasa  hapo juu kulia. Na kisha angalia matokeo. Kumbuka, kompyuta moja, kura moja. Ndio, hii ni Pima-Maji isiyochakachulika!
Maggid,
Dodoma.0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube