4 Oct 2011



Naamini wasomaji wapendwa wa blogu hii mlisoma POST HII niliyomjibu ndugu yangu Omar Ilyas aliyehitimisha kuwa Chadema inahitaji kushindwa ili ishinde

Naam,kwa hakika hicho ndicho kilichojiri jimboni Igunga ambapo licha ya CCM kuwekeza kila aina ya raslimali (halali na za kifisadi) imeibuka na ushindi mdogo tu wa tofauti ya kura takriban 2000.Ni wazi kuwa laiti CUF ingethamini umuhimu wa ushindi kwa vyama vya upinzani-na kumsapoti mgombea wa Chadema- muda huu CCM ingekuwa inahesabu hasara.

Ni rahisi kwa Chadema na wafuasi wake kuvunjika moyo kutokana na kutoibuka washindi katika uchaguzi huo.Lakini kimsingi Chadema imefanya vizuri kuliko ilivyotarajiwa.Unajua,kuna wakati ushiriki tu-na matokeo ya ushiriki huo-ni sawa na ushindi,hususan pale matokeo ya ushiriki huo yanapotoa picha ya kujenga matumaini.

Ni rahisi pia kwa watu kuikebehi Chadema-kama anavyofanya Bwana Nape Nnauye na viongozi wengine kadhaa wa CCM.Ikumbukwe kuwa CCM ililazimika kulamba matapishi yake hadi kufikia hatua ya kushinda uchaguzi huo.Sote tunafahamu kuwa Nnape na wenzie walitupa imani kuwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya uchaguzi,mtuhumiwa wa ufisadi Rostam Aziz,alikuwa gamba.Na hiyo ndio sababu ya msingi ya kufanyika uchaguzi huo baada ya gamba hilo kuamua kuondoka lenyewe.

Lakini wafuatiliaji wa kampeni za uchaguzi huo watakuwa bado na kumbukumbu za Rostam kupandishwa majukwaani kuiombea kura CCM.Well,hilo sio kosa kwani Rostam bado ni mwanachama wa CCM.Lakini ni kituko kisicho na maelezo kumshirikisha kwenye kampeni hizo mtu anayefahamika kama gamba ndani ya chama hicho.Inadaiwa kuwa Rostam alibembelezwa ashiriki kwenye kampeni hizo kutokana na nguvu zake kubwa za kisiasa jimboni Igunga.

Ni wazi kwa mwenendo huu tusitarajie kusikia magamba mengine ie Edward Lowaasa na Andrew Chenge wakijiuzulu nyadhifa zao kwani wanafahamu fika kuwa bado wanahitajika kwenye chama hicho kama ilivyokuwa kwa Rostam.

Sipati tatizo katika kuhitimisha kuwa Chadema ni kama wameshinda kwa vile katika ucgauzi huo walikuwa kama timu ya soka inayopambana na timu pinzani yenye wachezaji 15 (11 wa kawaida,refarii,kamisaa na washika vibendera wawili).CCM ilipewa kila aina ya sapoti kutoka serikalini,tukiweka kando vitisho vilivyotolewa na mawaziri kwa wapiga kura wa Igunga kuhusu "athari za kuwachagua wapinzani."

Lakini hapa tunazungumzia tuliyosoma magazetini na tuliyasikia redioni au kuyaona kwenye runinga.Kuna nguvu za giza ambazo hazikuweza-na kamwe haitowezekana-kuripotiwa.Hawa ni ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa.Ukweli usiofahamika ni kwamba jamaa hawa ni kikwazo kikubwa sana kwa maendeleo ya demokrasia Tanzania kwani wanafanya kila wawezalo-kwa kutumia usiri wao-kuhakikisha CCM inaibuka na ushindi katika chaguzi mbalimbali.

Sasa kama Chadema imeweza kupata kura zote hizo licha ya vikwazo lukuki ilivyokabiliana navyo jimboni Igunga ni dhahri kuwa laiti chama hicho kikishikamana na kudumisha umoja na mshikamano basi 2015 tunaweza kurejea historia iliyojitokeza nchini Zambia hivi karibuni.

Ni muhimu kutoangalia kushindwa kwa Chadema katika uchaguzi huo pasipo kuhusisha jithada (halali na haramu za serikali,taasisi zake na watumishi wake).Kama Chadema imediriki kupata kura takriban 2000 tu pungufu ya mgombea wa CCM basi kitakwimu na kiuhalisi ni kama wameshinda vile.

Of course najua kuna watakaosema najipa matumaini.Well,mimi si mwanachama wa Chadema na sitegemei kuwa mwanachama wa chama hicho au chama kingine chochote kile huko nyumbani.Kwanza sina sifa ya kuwa mwananchama na pili malengo yangu ya kiajira yananizuwia kujihusisha na chama chochote kile cha siasa.

Basi nimalizie kwa kuipongeza Chadema kwa kumudu kutoa upinzani wa dhati licha ya vikwazo vyote ilivyokabiliana navyo.Uchaguzi huu-na kushindwa kwake-iwe changamoto muhimu ya kuwaandaa kukamata nchi hapo mwaka 2015.Mkiamua kiwa kitu kimoja basi ni dhahiri kuwa yaliyotokea Zabia hivi karibuni yatarudia tena mwaka 2015.

Penye nia pana njia

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.