16 Nov 2011

Miraj Kikwete (kushoto)


MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Miraj Jakaya Kikwete, amekitetea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akipinga chama hicho kuhusishwa na vurugu mbalimbali zinazotokea nchini, zikiwemo zile za Wamachinga, zilizotokea jijini Mbeya hivi karibuni.

Mtoto huyo wa Rais alionyesha kukerwa na watu wenye mtazamo wa kukisingizia chama hicho kikuu cha upinzani kwa kukihusisha na vurugu, wakati hali halisi inaonyesha wazi kuwa wananchi wenyewe hawaridhishwi na hali ya mambo ilivyo na hivyo kuamua kuwa mstari wa mbele kupigania haki zao.

Miraj aliweka wazi msimamo wake huo kupitia mtandao wake wa facebook akichangia mjadala mzito uliohoji kwa nini CHADEMA inasingiziwa vurugu Mbeya?

Mtoto huyo wa Rais, aliweka wazi ujumbe wake huo baada ya mchangiaji mmoja, kuchangia kwa jazba akitabiri machafuko kutokea kabla ya 2015.

Mchangiaji huyo alisema yeye si mtabiri, lakini kwa hali ilivyo nchini, tunaelekea kwenye vita na haina hata mpito wa chaguzi mbili mbele kwa maana ya 2015 na 2020.

Mchangiaji mwingine, Gallus Mpepo, ambaye ndiye aliyekuwa akijadiliana na Miraj, alianza kwa kumrushia lawama Mkuu wa Mkoa mpya wa Mbeya, Abbas Kandoro, kwamba kila mkoa anaokwenda, amekuwa ukikumbwa na vurugu za Wamachinga.

Mpepo alisema anashangaa kuona baadhi ya wachangiaji wa mjadala huo, wanahusisha vurugu za Mbeya na maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), licha ya kwamba chanzo chake kiko wazi kwamba wafanyabiashara hao walikuwa wakipinga kuondolewa kwenye maeneo yao ya biashara bila kupewa maeneo mbadala.

Alisema hii inatokana na hali ya kutaka kuficha makosa yaliyofanywa na uongozi wa mkoa huo chini ya Kandoro, kutoongoza kwa busara katika kutatua kero za wananchi.

Katika ujumbe huo, Mpepo alieleza kufurahishwa na ujumbe wa mtoto wa Rais Kikwete na kwamba ameupenda ufafanuzi wake kuhusu mjadala huo.

Akichangia mjadala huo, Miraj ambaye ni nadra kujihusisha na masuala ya siasa, alihoji nani anayedai haki Mbeya kati ya CHADEMA na wananchi hadi kusababisha vurugu hizo.

Mtoto huyo wa Rais Kikwete alisema ni makosa kuihusisha CHADEMA na vurugu hizo kwani CHADEMA si nchi.

“CHADEMA si nchi ni chama na si kwamba wanachama wa CHADEMA ndio pekee wenye shida na matatizo, ni Watanzania wote,” alisema mtoto huyo wa Rais.

Miraj alienda mbali kwa kusema ni fikra potofu kufanya kama vile kuna Tanzania na CHADEMA.

“Maana serikali ndiyo Tanzania na CHADEMA ni chama ndani ya Tanzania, ni chama cha Watanzania kwa ajili ya Watanzania, kama kilivyo Chama cha Mapinduzi (CCM), NCCR-Mageuzi na kadhalika.

“Tofauti ni harakati na sera... tupendane Watanzania, tutafika mbali kwa umoja na mshikamano wetu na wala si kwa kejeli na matusi…, wenye haki tuwasimamie wote na penye haki tusimame sote,” alisema Miraj


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube