29 May 2012


Mama mpendwa,ilikuwa siku kama yale leo,miaka minne iliyopita,uliondoka hapa duniani wakati tunakuhitaji sana.Japo miaka minne inaweza kuonekana ni muda mrefu kusahau machungu,kwangu mwanao imeshindikana.Kila siku ya Mungu ninaposali kukuombea pumziko na raha ya milele huko ulipo,hujikuta napatwa na uchungu usioelezeka.Kwa kifupi,mama mpendwa,kila siku baada ya kifo chako-siku kama ya leo miaka minne iliyopita,imeendelea kuwa ni hudhuni na majonzi yasiyoelezeka.

Mama mpendwa,ulikuwa ni zaidi ya mama kwangu,kwa mumeo-Baba Mzee Chahali,na kwa wanao wote na ndugu na jamaa.Nakumbuka mwaka 2005 nilipokuja likizo nyumbani,ulirukaruka kwa furaha,ukanikumbatia na kunipakata mwanao,ukaniandalia maji ya kuoga,ukanifanya nijsikie kama mtoto mchanga.Sikujua kuwa furaha ile ya mzazi kumwona mwanae waliopoteana kitambo kidogo sintoipata tena maishani.Inaniuma sana.

Nakumbuka wakati huo ambapo wewe na Baba mlikuwa mnasherehekea miaka 50 ya ndoa yenu,ulinipa mafundisho mengi kuhusu maisha,ndoa,upendo na zaidi ni kumweka mbele Mungu katika kila ninalofanya.Kabla ya kifo chako,nilikuwa nauangalia mkanda niliowarekodi wewe na Baba,na kila nilipofanya hivyo niligundua kuwa nina bahati ya pekee kuwa na wazazi wanaonipenda kiasi hicho.Sikujua kuwa mahojiano yale ndio ulikuwa wosia wako kwangu mwanao.Kwa sasa sina nguvu ya kuangalia video hiyo,kwani kila nikijaribu naishia kububujikwa na machozi.

Nakumbua nilipokwenda chumba cha maiti na kukuona umelazwa kwenye zile friji wanzohifadhia maiti.Nilikugusa mama,nilitaraji muujiza kwamba ungeamka na ndoto ile mbaya ingeisha.Hukuamka hadi leo hii.

Mama,inaniuma sana kwani nilipokuja kukuuza Februari 2008 ulikuwa umeshapoteza fahamu.Ulipokuwa Muhimbili na baadaye St Francis,Ifakara,nilikuwa najaribu kukusemesha.Kama vile ulifahamu mwanao nimekuja kukuuguza,kuna nyakati ulikuwa unatoa tabasamu lako lenye mwanya ulionirithisha.Nikategemea utaamka na kunieleza japo neno moja.Kwa bahati mbaya hadi unafariki hukuweza kuniambia chochote.Inaniuma sana mama.

Inauma zaidi ninapopiga simu nyumbani.Nilizowea kuwa nikimaliza kuongea na Baba anakupa simu wewe tupige stori.Sasa,kila ninapompigia mzee huwa najikuta nataka kumwambia Mzee akupe simu niongee nawe,kisha nakumbuka kuwa hauko nasi.Kila simu ninayopiga nyumbani inanirejeshea kumbukumbu hizo na kuniacha mpweke,mkiwa na mwenye uchungu mkubwa.

Nyakati nyingine baadhi ya watu wangu wa karibu (ninao wengi kutokana na malezi bora uliyonipatia) huwa wananiona kama dhaifu ninapowaeleza uchungu nnilio nao takriban kila siku tangu ufariki.Siwalaum,kwani wanachojitahidi kufanya ni kunishawishi nikubali ukweli kuwa haupo nasi na haiwezekani kukurejesha.Kuna wakati wananichukiza kwani najihisi kama hawaelewi jinsi kifo chako kinavyoniathiri.Lakini baadaye akili hunirejea na kutambua wanachofanya ni kujaribu kunisaidia tu.

Mama mpendwa,sijui nisemeje.Rafiki zako wakubwa,wanao vitinda-mimba,Kulwa na Doto,ndio wananitia uchungu zaidi,kama ilivyo kwa Baba.Watatu hao pamoja na wewe mlikuwa kama marafiki.Nakumbuka siku zile nawapigia simu na kuwasikia mnacheka,mnataniana na kunipa kila aina ya faraja.Kwa sasa imebaki kumbukumbu tu.

Mama mpendwa,siku ya mazishi yako Padre alituambia maneno haya: "Mama Adelina alikuwa mtu wa watu,na kila anayemjua anafahamu hilo.Japo mnaomboleza kifo chake,lakini mnapaswa kupata faraja kuwa kutokana na matendo yake mema,Baba Yake wa Mbinguni Ameamua kumchukua.Sote tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi,na ndio maana amemchukua." Maneno hayo ndio nguvu pekee inayonisaidia kumudu kufanya mambo mengine maishani.

Basi naomba nikuage tena mama kwa kumwomba BWANA AKUPATIE PUMZIKO LA MILELE NA MWANGA WA MILELE AKUANGAZIE,UPUMZIKE KWA AMANI AMEEN.

6 comments:

  1. Tupo pamoja katika kumbukumbu hii ya mama nakuelewa kabisa ni uchungu gani ulionao. Lakini yote ni mapenzi ya Mungu kilichobaki ni kumwombea mama. Yupo nawe wakati wote kiroho.Mama Adelina PUMZIKA KWA AMANI.

    ReplyDelete
  2. inasikitisha, pole ndugu yetu, kifo hakizoeleki, nilimpoteza baba na kaka hakuna siku sijawakumbuka

    ReplyDelete
  3. Poleni sana familia ya Chahali,Mungu aendelee kuwatunza.Raha ya Milele umpe ee Bwana.................

    ReplyDelete
  4. Kaka pole sana kwa kupoteza mama na kwa mapenzi yote unayoyakosa,tarehe kama ya leo mimi na ndugu zangu mama mzazi pia tulipoteza pengo lake mpaka leo ni gumu kuzibika na kila siku inayopita lazima namkumbuka ktk njia moja au nyingine,kama maumivu uliyonayo nayafahamu na inapaswa kuwaombea wapendwa mama zetu wapumzike kwa amani na wapate mwanga wa milele,mpaka tutakapokutana nao tena.

    ReplyDelete
  5. Pole sana Prof Chahali!

    Miss Tambi

    ReplyDelete
  6. Mpiganaji Chahali,mola azidi kukufariji.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.