TAARIFA KWA UMMA
UBAGUZI UNAOFANYWA NA SERIKALI KWA
VIONGOZI WETU NGAZI YA CHINI
Ndugu wanahabari
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kupitia Kurugenzi ya Kampeni na Uchaguzi inapenda kutoa taarifa kwa
umma na kukemea ubaguzi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali dhidi ya
viongozi wa vyama vya siasa, hususan wale wa chama kikuu cha upinzani na chama
mbadala, CHADEMA.
Chama kupitia Kurugenzi ya Kampeni
na Uchaguzi kimepata taarifa kutoka ngazi ya chini ya uongozi, yaani misingi na
matawi kwamba mabalozi wa nyumba kumi wa CHADEMA wamekuwa wakibaguliwa katika
utendaji kazi wao wa kila siku na watendaji wa serikali, huku watumishi hao wakiendelea
kutoa ushirikiano kwa mabalozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu wanahabari kupitia kwenu,
tunaomba umma wa Watanzania ufahamu mambo mawili muhimu hapa;
Kwanza; balozi wa nyumba kumi wa
chama cha siasa si sehemu ya uongozi wa kiserikali. Suala hili limewahi
kusisitizwa na serikali yenyewe kwa kutoa kauli bungeni. Ngazi rasmi ya uongozi
wa kiserikali inaanzia serikali za mitaa/kitongoji.
Lakini pia suala hili la ngazi za
uongozi wa kiserikali na kuwa mabalozi si sehemu ya uongozi huo linaoneshwa pia
katika katiba yetu ya sasa (pamoja na ubovu wake uliotusukuma tudai iandikwe
upya).
Pili; Sheria ya Vyama vya Siasa ya
Mwaka 1992, inavitambua vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwa vyote
viko sawa mbele ya sheria. Halikadhalika
kutokana na sheria hiyo, katiba za vyama vyote vya siasa ni sawa, hasa
baada ya kuwasilishwa na kupitishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na
kupitishwa.
Kwa mantiki ya masuala hayo mwili
hapo juu, Kurugenzi ya Kampeni na Uchaguzi, inatumia fursa hii kutoa tamko kwa
umma kuwa mabalozi wa CHADEMA na CCM, wana haki sawa mbele ya sheria, kwa
sababu wanatokana na vyama vilivyo sawa mbele ya sheria, halikadhalika katiba
za vyama hivyo ziko sawa mbele ya sheria.
Mabalozi wa CHADEMA wanapatikana kwa
mujibu wa Katiba Mpya ya Chama ya Mwaka 2006, Sura ya Saba, ambayo inazungumzia
ngazi, uongozi na majukumu ya vikao.
Tofauti pekee ya mabalozi wa CHADEMA
na CCM ni kwamba mabalozi wa CHADEMA wanavaa magwanda wale wa CCM wanavaa
magamba. Lakini pia wanatofauti ya tabia;
Mabalozi wetu wanasimamia ukweli,
wakati wale wa CCM wanasimamia uongo, mabalozi wa CHADEMA wanasimamia uadilifu,
wale wa CCM wanasimamia ufisadi, wakati mabalozi wetu wanasimamia na kutumikia
wananchi, wale wa CCM wanatumikia maslahi ya chama chao na yao binafsi.
Pamoja na kazi zingine, baadhi ya
majukumu ya balozi wa CHADEMA ni pamoja na kuwa mwakilishi wa chama na
wanachama. Ana wajibu wa kuwatambua wanachama wenzake, wananchi wote na pia
anaufahamu wa kutosha wa masuala mbalimbali katika eneo lake la nyumba kumi.
Tunasema hivyo kwa sababu wakati mwingine
kutokana na kukosa mtandao mpana mpaka chini katika kaya za watu na wakati
mwingine ukubwa wa maeneo ya kitongoji/mtaa unakuwa kikwazo, mamlaka za
serikali katika kutekeleza majukumu mbalimbali zinashindwa kumtambua kila mwananchi, hivyo zinalazimika
kuhitaji mtu/watu wa kusaidia kazi hiyo katika nafasi za uongozi walizoaminiwa
katika maeneo madogo ambayo ni rahisi watu kutambuana. Hapo ndiyo dhana ya kuwa
na kiongozi wa kaya kadhaa kwa jina la balozi unatokea.
Mabalozi wetu CHADEMA kwa sababu
wanatokana na taasisi inayotambulika kisheria, makini na imara wanafanya kazi
kwa barua na mhuri wa chama.
Kupitia tamko hili, Kurugenzi ya
Kampeni na Uchaguzi ya CHADEMA, inawataka watendaji wa ngazi zote wa serikali
kuacha mara moja tabia ya kuwabagua mabalozi wa CHADEMA kwani wanatokana na
watu, wanatambua na wanaweza kutimiza wajibu wanaopaswa kufanya.
Chama pia kinatumia fursa hii kutoa
mwito kwa mabalozi wote wa CHADEMA nchi nzima ambao wanakutana na vikwazo vya
watendaji wa serikali katika kutimiza majukumu yao mbalimbali ya kila siku,
watoe taarifa rasmi kwa ngazi za juu zao, ili ngazi hizo husika nazo
ziwasilishe kunakohusika, kwa ajili ya chama kuchukua hatua zaidi.
Imetolewa
leo Juni 24, 2012 Dar es Salaam na
Msafiri
Abdulrahaman Mtemelwa
Mkurugenzi
wa Kampeni na Uchaguzi CHADEMA
0 comments:
Post a Comment