18 Jan 2013

*Serikali yadaiwa kuchakachua bei halisi ya ujenzi
*Gharama za mradi huo zimeongezwa maradufu
*Zitto Kabwe adai kuwa viongozi wamehongwa KASHFA mpya ya ufisadi wa mamilioni ya Dola za Kimarekani zilizokusudiwa kutumika katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, imeanza kutokota serikalini, Rai limedokezwa.


Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka vyanzo vyake mbalimbali serikalini, zimeeleza kuwa kufichuliwa kwa ufisadi huo, ni jitihada za kuwaunga mkono wananchi wa Mtwara, ambao kwa takribani wiki mbili sasa, wamekuwa katika mgogoro na Serikali wakishinikiza uvunaji wa gesi hiyo uwanufaishe wao kwanza, badala ya kuipeleka jijini Dar es Salaam, jambo ambalo Serikali imekuwa ikiliita ni usaliti na uhaini.Maofisa kadhaa walioko Wizara ya Nishati na Madini waliozungumza na Rai kuhusiana na sakata hilo, wameeleza kuwa, baadhi ya viongozi wa Serikali, waliosimamia upatikanaji wa mkopo wa Dola za Kimarekani bilioni 1.2 kutoka Benki ya Exim ya China, na wale walioandaa gharama za ujenzi wa bomba hilo, walishtushwa na hatua ya wananchi wa Mtwara kuandamana kupinga mpango wa ujenzi huo, kutokana na hofu ya kubainika kwa ufisadi mkubwa ulioughubika mradi huo.Wamesema kutokana na hofu hiyo, viongozi mbalimbali wanaoguswa na walio katika hatari ya kuguswa na sakata hilo, walianzisha uchunguzi, ili kubaini iwapo maandamano hayo yalikuwa na shinikizo la wanasiasa waliobaini kuwapo kwa ufisadi kwenye mradi huo.Ili kuzima jitihada za aina yoyote za kuukwamisha, walilazimika kutumia maneno makali na yenye vitisho kwa waandamanaji na kuwatuhumu wanasiasa waliokuwa wakiunga mkono hatua ya wananchi wa Mtwara.Kwa mujibu wa taarifa hizo, gharama zilizoongezwa katika ujenzi wa bomba hilo ni Dola za Kimarekani milioni 532, kiasi kinachoelezwa kuwa kinaweza kulingana na gharama halisi ya ujenzi kwa mradi mzima.Baadhi ya wahandisi waliobobea katika fani hiyo, wamelieleza Rai kuwa gharama halisi ya ujenzi wa bomba hilo ambalo litatandazwa urefu wa kilomita 532 kutoka Mtwara hadi eneo la Kinyerezi, Dar es Salaam, ni Dola za Kimarekani milioni 638, hivyo kiasi kilichokopwa na Serikali kwa ajili ya kazi hiyo ni kikubwa zaidi.Wamefafanua kuwa, gharama za kimataifa za ujenzi wa mabomba ya aina hiyo kwa kilomita moja, ni Dola za Kimarekani milioni 1.2 na kwamba kiasi hicho hutumika kwenye maeneo magumu kiujenzi yakiwemo maeneo ya milima na kweenye miamba.Kiasi hicho kinazidi karibu maradufu ya kile kinachotumika hapa nchini, ambapo kilomita moja inajengwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 2.2. Kwa gharama hiyo, kukamilika kwa ujenzi wa kilimota 532, kutagharimu kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 1,170,400,000.Mchanganuo wa gharama za bei za kimataifa zinazotumika sehemu mbalimbali kwa ujenzi wa njia za mabomba na gharama inayotumika Tanzania uliofanywa na watalaamu wa uhandisi waliozungumza na Rai, unaonyesha kuwa zaidi za Dola za Kimarekani milioni 500 zimeongezwa, jambo linaloashiria kuwapo kwa ufisadi katika mradi mzima.Akizungumza na Rai kuhusu sakata hilo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, amesema analifahamu kwa undani suala hilo na kwamba kinachoitesa sasa Serikali, ni kubainika kwa ufisadi mwingine ilioufanya ambao utawaumiza Watanzania kwa kiwango kikubwa.Zitto amesema anazo taarifa za kutolewa rushwa kubwa kwa baadhi ya viongozi wa Tanzania na wale wa China, ambao walihusika kuidhinisha na kupokea mkopo wa Dola za Kimarekani bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa bombahilo, madai ambayo ameanza kuyachunguza kutokana na historia ya China kuonyesha kuwa imekuwa ikijihusisha na vitendo vya rushwa katika kupata zabuni kubwa kubwa katika mataifa mbalimbali duniani.“Kuna ufisadi wa kutisha katika mradi huu, ukiangalia fedha zilizotolewa, gharama halisi ya ujenzi wa bomba la gesi na gharama inayotumiwa kujenga hili la hapa nchini, utabaini kuwepo kwa ufisadi. Tunapaswa kujiuliza uhalali wa gharama hizi. “Ni kweli Serikali imekopa dola bilioni 1.2 kutoka Benki ya Exim ya China kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo. Gharama za kimataifa za ujenzi wa kilomita moja ni dola milioni 1.2, lakini sisi tunajenga kilomita moja kwa dola milioni 2.2, mara mbili ya gharama za kimataifa. “Kwanini? Watanzania wanapaswa kujiuliza hili, kwanini gharama hizi? Sasa kwa sababu ya hofu ya kugundulika kwa ufisadi huu, Serikali inapoona wananchi wanadai haki yao ya msingi, kwa sababu ya hofu ya kubainika kwa ufisadi, ilioufanya inahamanika kwa sababu madudu yake yatabainika.“Taarifa nilizonazo zinaeleza kuwa kuna dola milioni 220 zilitumika kuhonga viongozi, ili mkopo upatikane na gharama za ujenzi ziwe juu. Sasa China inasifika kwa rushwa kwenye miradi mikubwa, kwa sababu hiyo tu, utaona kuna kila sababu ya suala hili kuchunguzwa vizuri. Wabunge wanapaswa kuhoji hili,” alisema Zitto.Zitto ameeleza zaidi kuwa, mazingira ya utoaji wa mkopo huo yamejaa utata, kwa sababu Benki ya Exim haijautoa serikalini, bali imeelekeza fedha zote kwa kampuni iliyopewa zabuni ya ujenzi, hivyo Watanzania hawataambulia chochote katika mkopo huo.Amesema maeneo mengine yenye utata katika utekelezaji wa mradi huo, ni namna mzabuni alivyopatikana bila kufuata taratibu za utoaji zabuni, na kwamba hata mkataba wa ujenzi uliosainiwa na Wizara ya Fedha na Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC) kwa upande wa Tanzania na Benki ya Exim kwa upande wa China, umeghubikwa na usiri, ambapo kabla na baada ya kusainiwa, Bunge limekuwa likifichwa kufahamu chochote kilicho katika mkataba huo.Akieleza kushangazwa na jinsi mkopo huo ulivyopatikana, amesema imekuwa kawaida kwa China inapotoa mkopo, kuweka sharti kwa mkopaji na kutoa kitu kitakachoinusha na kutoa mfano wa nchi ya Angola, ambayo ilipewa mkopo kwa sharti la kupatiwa visima vya gesi, hivyo ni lazima Serikali ya Tanzania imetoa sehemu ya maliasili zake kwa mkopo huo, ambazo amesisitiza kuwa ni lazima zitajwe ili Watanzania wafahamu.Jitihada za Rai kumpata Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhusu suala hilo, hazikuweza kufanikiwa, baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa kwa muda mrefu.Kuibuka kwa madai ya kuwapo ufisadi katika mradi wa ujenzi wa bomba la gesi, kunazidi kuyapa nguvu madai ya wananchi wa Mtwara ya kutaka rasilimali hiyo isitumike vibaya, bali iwanufaishe wananchi, tofauti na ilivyopata kutokea katika maeneo ya madini ambako kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuwa madini yamekuwa yakiwanufaisha zaidi vionghozi wachache na wawekezaji badala ya wananchi.

CHANZO: Rai

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube