5 Oct 2013



Mnamo tarehe 9 Desemba 1961, Tanganyika ilipata Uhuru chini ya Waingereza waliokuwa waangalizi wetu tu, 

Ni nyakati hizo ambapo mataifa ya Afrika yalikuwa kwenye vuguvugu la kupata uhuru wao kamili yakiongozwa na Nchi ya Gold Coast iliyojinyakulia uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo tarehe 6 Machi 1957, na ikawa taifa la kwanza la Afrika Kusini mwa Sahara (Sub-Saharan Africa) kufanya hivyo japokuwa Gold Coast/Ghana haikuweza kutangaza uhuru wake kamili kutoka kwa Uingereza hadi tarehe 1 Julai 1960 ambapo pia nchi ilianza kujulikana kama Jamhuri ya Ghana.

Nchi ya Gold Coast ilianzishwa na Waigereza, "Gold Coast" ni nchi ya Ghana ya leo, Neno Ghana lina maana ya Shujaa Mfalme na lilikuwa ni jina la heshima walilopewa wafalme wa Himaya ya Ghana nyakati za kale za Afrika Magharibi.

Tangu Tanganyika ipate uhuru 09/12/1961 hadi kifo chake chenye utata 1964, ilitumia KATIBA ya chama cha Ukombozi cha TANU iliyoandikwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na mahuisho mengi yaliyopita kama yale ya 1962, 1965, 1977, 1992 bado asili ya katiba hii tuliyonayo leo ni ya MKONO wa Julius Nyerere,

Marekebisho makubwa ya Katiba yalikuwa ni mwaka 1977, lakini asili ya KATIBA ile ya Mkono wa Nyerere imeendelea kuishi na kulitendea haki Taifa na wajihi wake!

Nchi ya Gold Coast ilipopata uhuru chini ya Kwame Nkrumah licha ya kubadili jina la nchi na kuitwa Ghana, bado iliendelea kutumia asili ya katiba ya Chama cha The Convention People's Party (CPP) 

Labda kwa wale wasiojua niwafahamishe kuwa Katiba ya Tanganyika African National Union (TANU) ilinakiliwa kutoka chama rafiki cha The Convention People's Party (CPP)

Ni mashirikiano mema katika makutano ya fikra za kisiasa kati ya vijana wawili wasomi na imara ambao bara la Afrika halijapata kuwa nao kwa karne hivi sasa, si wengine ni Julius Nyerere na Kwame Nkrumah walipobadilishara fikra na kuzaa matunda ya Afrika na dunia tuyatafunayo sasa,

Nimekuwa na mtazamo hasi kabisa juu ya uhuru wa Afrika kwa mda mrefu sana hasa kwa matukio niyaonayo na niyasikiao toka Afrika,

Miaka ya 1955-1975 ni kipindi ambacho Afrika ilijitoa toka mikononi mwa mkoloni, mimi huwa naamini ni kipindi ambacho Afrika haikuwa na sifa za kuwa tayari kujitawala kwa maana ya kujipatia/kupewa UHURU,

1. Afrika haikuwa na Wasomi wakuongoza nchi

2. Waafrika walikuwa kwenye lindi la kutopea kwenye ujinga, hawakuwa tayari kwa kuupokea uhuru huo,

Mfano Tanganyika ilipata Uhuru ikiwa na wasomi wachache wenye ngazi ya shahada ya Uzamili (Masters) ambae ni Julius Nyerere, na Shahada ya Uzamivu (PHd) ni mmoja tu ambaye ni Dr Vedasto Kyaruzi, 

Na hata wale waasisi waliokuwemo kwenye harakati za kupigania Uhuru ndani ya TANU hawakuwa wasomi wa ngazi za juu zaidi ya Julius Nyerere,

Wazee hawa ni Julius Kambarage Nyerere, Ali Sykes, Lameck Makaranga, Gosbert Milinga, Gelmandus Pacha, Joseph Kimalando, Japhet Kirilo, Abubakar Ilanga, Saadan Kandoro, Suleiman Kitwara, Kisunguta Kabara, Tewa Said Tewa, Dosa Aziz, Patrick Kunambi, Joseph Kasela-Bantu, John Rupia, Abdul Wahid Sykes.

Nchi ya Gold Coast/Ghana ilipopata uhuru haikuwa na wasomi wengi wa Shahada, Stashada na Shahada ya Uzamivu na uzamili, 

Msomi wa ngazi ya juu alikuwa mmoja tu mwenye shahada ya Uzamili (Master of Science) ndugu Kwame Nkrumah 

Japokuwa usomi wa ngazi ya juu kwa watawala sio tiketi ya uwezo wa kutawala katika nchi, Hili huwa naamini ni kosa la Afrika la 1960-1975 kudai Uhuru na kupewa MAPEMA huku Waafrika hawakuwa tayari kujitawala wenyewe,

Hatua hii hunifanya niamini kuwa Afrika haikuwa imepevuka kujitawala kwa ngazi ya karne ile ya 20, huwa naamini kuwa miaka 1975-1985 ndicho kipindi ambacho Afrika ingekuwa kwenye mapito sahihi ya kujitawala, nikipindi ambacho binadamu wa Afrika angekuwa amepevuka,

Sasa ni karne ya 21, kosa lile la Karne ya 20 linajirudia katika muundo uleule kasoro nadharia tu, nalo ni upatikanaji wa Katiba mpya ya Tanzania,

Hali hii ya uhitaji wa katiba mpya kwa Watanzani ni jambo la kupongezwa na kujivunia kwa kila mtanzania, kwakuwa imedhihirika kuwa sasa Taifa limekuwa kifikra, na zaidi idadi ya wasomi katika nchi imeongezeka maradufu,


Lakini jambo la hatari na lisilokubalika nikuwa Taifa limeaminishwa kuwa Katiba Mpya itapatikana kabla ya 2015, huu ni ulaghai na wendawazimu wa wazi kabisa,

Katiba ya Watanzania haiwezi kupatikana kwa miaka mitano ama mmoja huu uliosalia, Katiba inayohitaji maridhiano, katiba inayopita kwenye misigano ya kitaifa, katiba inayohitaji elimu kwa Watanzania kwanza kamwe haiwezi kupatikana kabla ya 2015, kitakachopatikana kabla ya 2015 kitaitwa katiba ya kisiasa sio katiba ya Watanzania, 

Ninachokiamini nikuwa Watanzania tujipe muda, turuhusu fikra na mijadala huru iendelee juu ya upatikanaji wa Katiba mpya, turuhusu majibizano ya hoja ya endelee, tuyturuhusu Watanzania wote wake kwa waume, Wazee kwa vijana wote watoe ya moyoni bila kuogopa mawazo yao,

Katiba bora ya kiraia yenye matakwa halisi ya Wananchi inaweza kuchukua hata miaka 10 mchakato wake mpaka kuipata, hivyo katiba hii ambayo mchakato wake unaendelea SIO lazima isimamie Uchaguzi wa 2015 kama wanasiasa wanavyotusukuma tuamini hivyo,

Nionavyo muhimu katika kipindi hiki nikuwa, Watanzania, wanaharakati na Wanasiasa waendele kusimamia mchakato uendelee lakini upande wa pili wageuzi fikra zao, uanzishwe mchakato wa marekebisho ya Katiba hii iliyopo ili tuingie nayo kwenye uchaguzi 2015.Kinyume na hapo ni kuwalaghai Watanzania kuwa katika itapatika kabla 2015, 

Ikumbukwe kuwa Jakaya Kikwete ambae sasa ndiye rais wa Tanzania, katika historia ya siasa zake DUNIANI, hajawahi kuhitaji katiba mpya ya Tanzania wala kuizungumzia tu, hata serikali ya Chama chama Mapinduzi ambacho yeye ndiye Mwenyekiti hakijawahi kuhitaji Katiba Mpya ya Tanzania, na zaidi serikali ya Chama cha Mapinduzi iliyodumu kwa miaka 50 sasa haijawahi kuhitaji katiba Mpya ya Tanzania,

Vyama vya upinzani na Wanaharakati wa Tanzania ndio walioasisi mapambano ya kudai Katiba mpya, tena vikipita katika mapito magumu sana yenye kuhatarisha uhai wao,

Ni baada ya uchaguzi mkuu 2010 ndipo mbinyo wakudai katiba mpya ukiongozwa na chama kikuu cha upinzani nchini huku ccm na wahafidhina wake wakipinga katukatu kuwa Taifa halihitaji Katiba mpya,

Lakini KUFUMBA na KUFUMBUA Jakaya Kikwete alilitangazia Taifa kuwa linaanza mchakato wa Katiba, akitumia neno KUHUISHA katiba.

Tafakari Chukua Hatua, Busara ni mwanzo wa kukaribisha Hekima yenye nguvu za maliza tofauti katika nchi na kupata katiba ya kiraia yenye mkono wa Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.