28 Jul 2014

Rais Jakaya Kikwete akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Rashid Othman 
Wakati idadi kubwa ya Watanzania inapinga vikali taasisi za intelijensia kuwafanyia ushushushu viongozi wa siasa na raia wa kawaida, Tanzania inashika nafasi ya pili duniani-nyuma ya Italia-kwa kudaka mawasiliano ya wananchi wake kwa siri.

Asilimia 71 ya Watanzania waliohojiwa katika utafiti uliofanywa na taasisi ya Pew Research Centre ya Marekani walipinga vitendo vya serikali kuingilia mawasiliano ya simu na email ya viongozi wa kisiasa. Asilimia 25 waliafiki vitendo hivyo.

Utafiti huo ulionyesha kuwa Watanzania wanaongoza barani Afrika katika upinzani wao dhidi ya uvamizi wa faragha yao unaofanywa na taasisi za intelijensia.

Hata hivyo vitendo vya kishushushu kufanya ufuatiliaji kwa kuingilia au kunasa mawasiliano vimeshamiri mno nchini Tanzania kiasi kwamba nchi hiyo inashika nafasi ya pili duniani nyuma ya Italia katika vitendo hivyo.

Mwezi uliopita, kampuni ya kimataifa ya simu za mkononi ya Vodafone, ilitoa taarifa inayoonyesha kuwa kampuni yake tanzu ya Vodacom Tanzania ilitoa mawasiliano 98,765 ya wateja wake kwa mashushushu.

Katika ripoti hiyo, Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya pili duniani - katika nchi 29 ambapo Vodafone inatoa huduma - nyuma ya Italia kwa kufuatilia, kuingilia au kunasa mawasiliano ya simu. Italia inashika nafasi ya kwanza kwa mawasiliano 605,601 yaliyoombwa na taasisi za usalama.

Vodafone ilibainisha uwepo wa nyenzo za siri zinazowawezesha mashushushu kusikiliza mawasiliano ya wateja wa kampuni hiyo.

Kampuni hiyo imevunja ukimya kuhusu vitendo vya serikali kuwafuatilia raia wake kwa ushushushu katika mitandao ya simu na intaneti.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Tanzania, utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 49 ya Wakenya wanaafiki mashushushu kunasa mawasiliano ya simu na email ilhali asilimia 44 hawaafiki.

Utafiti huo unaonyesha kuwa Kenya inaongoza miongoni mwa nchi za Afrika kuhusu ridhaa kwa serikali/mashushushu kuwapeleleza raia.

Chanzo: imetafsiriwa kutoka gazeti la The Citizen (Tanzania)0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.