31 Jul 2014

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA na shushushu mzoefu, John Brennan, akiwa amezungukwa na walinzi wakati akitoa maelezo yake katika 'bunge' la Seneti la nchi hiyo.
Kwa Watanzania wengi, bila shaka mara yetu ya kwanza kufahamu kuhusu mashushushu ilikuwa kupitia vitabu vya Willy Gamba.Unakumbuka 'KIKOMO'? Au 'KIKOSI CHA KISASI?' Au vipi kuhusu 'NJAMA'? Sio siri, kusoma vitabu vya Willy Gamba vya marehemu Aristablus Elvis Musiba kulimfanya kila msomaji atamani kuwa kama Willy Gamba...yaani shushushu. Lakini kwa vile zama za Willy Gamba zilikuwa kipindi ambacho Tanzania ilikuwa kama 'kisiwa' kisichofahamu yanayojiri nje yake, riwaya hizo zilikuwa na mengi yaliyoshabihiana na shushushu wa kimataifa James Bond wa Uingereza.

Lakini baada ya Tanzania kufungua milango yake kwa dunia, wengi walibahatika kumwona James Bond kupitia filamu zake mbalimbali.Lengo la makala hii sio kujadili vitabu hivyo bali kujenga picha halisi, na penine tofauti kati ya ushushushu wa vitabuni au kwenye filamu na uhalisia wa taaluma hiyo. Lakini kabla ya kwenda mbali ni vema pia kukumbushia kuhusu 'Mashushushu wa zama hizi' kwa mfano Jack Bauer wa 'series' ya 24. Wakati Willy Gamba ameendelea kubaki vitabuni tu-kwa maana kwamba hakuna filamu iliyotengenezwa (bado nina fikra za kuyarejesha maisha ya shushushu huyu kwa njia ya filamu), James Bond amekaa 'kizamani' kwa maana ya uwepo wake kwa miaka mingi.Lakini Bauer anaonekana kama 'shushushu wa kizazi kipya' kama ilivyo kwa Nicholas Brody na Carrie wa Homeland, ambao katika filamu zao zina baadhi ya mabo ya kisasa kama matumizi ya mitandao ya kijamii (kwa mfano Facebook na Twitter) na mambo mengine ya 'kwenda na wakati.'

Hata hivyo, japo ushushushu wa kwenye vitabu vya Willy Gamba na filamu za James Bond au series kama 24 na Homeland zinatoa picha ya karibu kabisa na taaluma halisi ya ushushushu, kuna tofauti kubwa kati ya ndadharia na vitendo. Makala hii inazungumzia maisha halisi ya shushushu mstaafu wa shirika la ujasusi la Marekani (CIA), Robert Baer

Kwenye filamu ya hivi karibuni ya James Bond, SKYFALL, 'kubwa la maadui' ni gaidi la mtandaoni (cyberterrorist),Raoul Silva, shushushu wa Kiingereza aliyeasi na mwenye dhamira ya kusababisha 'kiama' kwa ulimwengu wa komputa (digital universe).Ukiangalia filamu hiyo unapata picha ya jinsi janga hilo linavyoweza kuwa na madhara makubwa. 
Lakini kitu pekee cha karibu kati ya ushushushu wa kwenye filamu na ushushushu halisia ni ukaribu na ukweli wa tishio la ugaidi wa kompyuta. Yaani, iwe ni kwenye filamu au katika dunia halisi, kilichomo kwenye filamu hiyo kitakuwa janga kubwa laiti kikitokea. 
Usinielewe vibaya, mie ni shabiki wa filamu za James Bond.Huenda kuziangalia kwa sababu zilezile ambazo kila mwendaji filamu anazo: wanawake warembo, sehemu nzuri za kuvutia, na 'kimuhemuhe' kinachoambatana na stori zinazobeba filamu za Bond.
Lakini kama shushushu mstaafu, kinachonivutia zaidi katika filamu za Bond ni kila mara mema kushinda maovu.Katika filamu zote za Bond, kubwa la maadui huangamia na dunia ya watu wema husalimika. 
Lakini katika ushushushu halisia, mambo hayaendi 'kiuzuri' kama iavyooneshwa katika filamu za Bond, na kwa hakika kuna 'mbinde' kadhaa. 
Tofauti na busara za muda mrefu mrefu kuwa adui wa adui yetu ni rafiki yetu, kwenye ushushushu halisia hali yaweza kuwa tofauti. Wakati flani, kwenye miaka ya 1980,nilipewa kabrasha la viongozi flani wa upinzani nchini Libya, miongoni mwa wengi waliokuwa wakifanya shughuli zao jijini Khartoum,nchini Sudan. Awali, nilkuwa na upeo mdogo tu kuhusu wasifu wa wapinzani wa kingozi wa Libya wa wakati huo,Kanali Muamar Gahddafi. Kitu pekee nilichokuwa na uhakika nao ni kwamba Rais wa Marekani wakati huo,Ronald Reagan, alikuwa anataka Gaddafi aangamie. 
Usiku mmoja, nilishtushwa na sauti za vitako vya bunduki vilivyokuwa vikibamiza mlango wa chumba changu.Watoa habari wangu wawili wa Kilibya walikuwa wakihangaika kulinda maisha yao dhidi ya wauaji wa Ghaddafi na walitegemea mie ndio niwapatie ulinzi.Tulfanya maongezi takriban usiku mzima kuhusu Libya, historia ya nchi hiyo na Allah. Ulipotimu muda salama kwa wao kuondoka, nilikuja kubaini kuwa watu tuliowaamini kuwa wangetusaidia kumwondoa Ghaddafi ni Waislam wenye msimamo mkali ambao lengo lao kuu ni kuifanya Libya kuwa taifa la msimamo mkali wa Kiislam. 
Wakati flani,katika kumfuatilia mtoa habari 'mpotevu,' mwajiri wangu (CIA) alinituma Monaco. Matatizo yalianza hata kabla sijapanda ndege. CIA walikataa kuninulia suti ya tuxedo (ili kuendana na mazingira ya casino za huko) na mhasibu wetu alikataa kunipa fedha za kuchezea kamari.Nilipofika,na kuingia kwenye casino hiyo, walinzi walinihoji kirefu, na mwishowe operesheni hiyo haikufanikiwa kwani sikuweza kumpa mtoa habari niliyekuwa nikimsaka. Kwa hakika nilitambua urahisi alionao James Bond kwenye filamu ni mgumu katik halisi halisi. 
Mtu yeyote aliyepitia chuo cha mafunzo ya mashushushu wa CIA Langley atakwambia maisha ya shushushu yanahitaji uvumilivu mkubwa. Ni muda mrefu wa kuwa peke yako katika kijichumba kidogo, kupitia mafaili kwa undani, mafaili ambayo watu kibao wameshayapitia, matarajio yakiwa wewe utagundua kitu ambacho wenzio hawakukiona. Au kugandishwa kwenye kibanda cha simu kwa muda mrefu ukisubiri labda mtoa habari atakupigia simu. Au kufanya dua kwa matumaini kwamba operesheni yako ijayo sio katika eneo la kutishia uhai.  
Hata hivyo, pamoja na yote hayo sio kusema kwamba katika ushushushu hakuna matukio kama tunayoyaona katika filamu za James Bond.Mashushushu walimwinda Osama bin Laden na hatimaye kufanikiwa kumuua watakueleza kwamba mara kadhaa walikuwa kama wanaishi kwenye filamu ya James Bond. 
Hata hivyo, ukweli unabaki kuwa maadui wanaowindwa na mashushushu huwa wanajificha katika mazingira ambayo kwa hakika ni vigumu mno kuwagundua. 
Kama ilivyo kwa CIA, maafisa wa shirika la ujasusi la Uingereza MI6 pia wanatumia mjuda mwingi maofisini badala ya unachokiona kwenye filamu za James Bond au Jack Bauer wakifanya mambo ya miujiza kama kuruka kutoka kwenye ndege na kusalimika. Na kama walivyo wenzao wa CIA, kwa muda mwingi mashushushu wa MI6  ni watu wa kupekua mafaili ofisini kuliko watu wa action kwenye mapambano ya 'kuchemsha damu' kama inavyoonyeshwa kwenye filamu za kipelelezi. 
Katika zama tunazoishi sasa, mashushushu wengi ni watu wa kupekua data na kujaribu 'kuhujumu' kompyuta. Hawa ndio watu waliomudu kuhujumu mfumo wa kompyuta wa kijasusi na nyuklia wa Iran unaofahamika kama Stuxnet. Huenda kabla ya kufanikisha operesheni hiyo, mashushushu hao walikaa kwenye kompyuta zao miezi kadhaa kusaka mafanikio walioyapata.
Angalau filamu nyingine ya kishushushu kutoka Hollywood, Argo, inatoa picha ya karibu ya maisha halisi  ya shushushu- kukaa ofisini muda mrefu kurudia 'somo' lileile hadi 'siku ya siku ya balaa' inapowadia. Operesheni za 'hatari' hutmia muda mwingi wa maandalizi ofisini kuliko katika 'uwanja wa mapambano' au 'eneo la tukio,' tofauti na inavyoonyeshwa katika filamu nyingi za aina hiyo. 
Lakini japo mwisho wa filamu hiyo ya 'Argo' ni mtamu ambapo 'mateka' wote waliokolewa, hali haikuwa hivyo kiuhalisia kwani si mateka wote waliookolewa na mwishowe Marekani iliishia kuumbuka badala ya kuonekana shujaa anayeonyeshwa katika filamu ya Argo.

Sote tuliinjoi kusoma stori za Willy Gamba au kuburudika na stori za James Bond, Jack Bauer au Carrie na Nicholas Brody ambazo kwa kiasi flani zinarahisisha operesheni za kishushushu kwa minajili ya ileile ya 'stering hauwawi.' Hata hivyo, kwenye uhalisi wa operesheni za kishushushu ni vigumu mno kubashiri matokeo, na hata kama mambo yakionekana kwenda sawia kama ilivyapangwa, surprise ni jambo la kawaida. 

Na wakati mwingine ugumu wa operesheni unachangiwa na funzo muhimu kwa mashushushu kwamba 'ukiona kila kitu kinakwenda sawia basi ujue kuna hatari huko mbeleni.' Katika mafunzo ya taaluma hiyo, inakumbushwa mara kwa mara kwamba kamwe usiamini unachokiona bali jaribu kwenda ndani zaidi na kutafuta kisichoonekana.

Nimalizie makala hii na stori moja ya kusisimua (hainihusu): jamaa flani alikuwa ajifanikiwa kujipenyeza kwenye genge flani la wauza noti bandia katika mtaa mmoja maarufu jijini Dar. Kwa umahiri wake alifanikiwa kuaminika mno hadi akaweza kuwa karibu na bosi wa genge hilo. Kwa vile mashushushu ndio wanaowataarifu polisi kabla ya kuvamia makundi kama hayo, siku ya tukio kulijitokeza mgogoro wa kimawasiliano kati ya mashushushu na polisi, na matokeo yake polisi walivamia genge hilo wakati yule jamaa akiwa kazini-kaka shushushu na kama membe wa lile genge. Naomba uelewe kuwa katika matukio ya aina hiyo kuna uwezekano wa kupoteza maisha kwa vile polisi wanadhani wote waliomo katika genge husika ni wahalifu halisi bila kujua kuwa kuna mashushushu wapo kazini pia. 

Katika dakika ya kuamua kifo au kubaki hai, jamaa huyo alipatwa na mtihani wa aidha ajitambulishe kwa polisi na kuwasihi wawasiliane na viongozi wa operesheni hiyo (na kwa kufanya hivyo angekuwa anaweka roho yake rehani kwani genge lingebaini kuwa yeye ndo aliwachoma) au 'afe kizungu na tai shingoni' kwa kuendelea kujifanya mhalifu na kuomba dua zake pilisi wasimtoe roho...

No, hiyo sio hadithi ya kutunga. Ni tukio la kweli kabisa, na japo nisingependa kueleza hatma yake kwa undani (jamaa huyo alisalimika na yupo hai hadi leo licha ya baadhi ya wahalifu 'wenzie kuuawa au kujeruhiwa kwa risasi za polisi katika tukio hilo) nadhani tukio hilo laweza kukuonyesha jisni ushushushu wa vitendo unavyoambatana na hatari ambazo pengine kwenye vitabu vya Willy Gamba au filamu za James Bond, 24 au Homeland zinajengwa katika amzingira ya 'stering hauwawi.'

Endelea kutembelea blogu hii kwa ajili ya kupata habari na matukio mbalimbali yanayohusiana na taaluma ya intelijensia, hasa kwa kubonyeza hapo juu ya blogu kwenye maneno INTELIJENSIA
0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube