20 Aug 2014

"Hao Chadema ni watu hatari kabisa. Eti ndio 'government-in-waiting' (chama kinachotarajia kushinda uchaguzi na kuunda serikali)." Haya ni maneno ya msomi mmoja, mtu ambaye kwa hakika ana uelewa mkubwa wa masuala mbalimbali hususan yanayoihusu Tanzania yetu. 

Hii ndio Tanzania, na hawa ndo watu wake. Ni vigumu mno kutofautisha kati ya msomi na mbumbumbu yanapokuja masuala yanayohitaji kuuhangaisha ubongo. Wanasiasa matapeli wameshatambua udhaifu huo mapema, na wanautumia ipasavyo.

Hivi kweli mtu mwenye akili nzuri anaweza japo kupoteza muda wake kusikia porojo kuwa 'Chadema ni chama cha kigaidi, na ndicho kilichopanga mauaji ya kinyama ya mwandishi Daudi Mwangosi'? Ndio, kuna wanaoichukia Chadema kwa sababu 'ni chama cha Kikristo.' Kuna wanaoichukia kwa vile 'ni chama cha Wachagga.' Kunawanayoiona Chadema ni ya kitapeli kwa vile 'Mwenyekiti wake Freeman Mbowe alikuwa mpigisha disko (DJ) huko nyuma.' Na kuna wanaoitazama Chadema kama kundi la wazushi kwa vile Katibu wake Mkuu, Dkt Willbrod Slaa 'aliacha upadri na kuingia kwenye siasa.'

Lakini Chadema imejitengenezea maadui kadhaa kutokana na matatizo yake na mwanachama wake machachari Zitto Kabwe. Huyu ni mtu mwenye ushawishi mkubwa, hususan miongoni mwa vijana. Ana marafiki wengi, hususan mtandaoni. Matatizo kati yake na Chadema, ambayo binafsi ninayatafsiri kama 'kutanguliza hisia mbele ya akili' (puitting emotions in front of common sense) yanachukuliwa na marafiki zake kama moja ya sababu kuu za kuichukia Chadema.

Pengine ni vema nikatanabaisha kuwa si lazima kila mtu aipende Chadema, kama ambavyo hakuna anayelazimishwa kuichukia CCM au kuipenda CUF. Ndio demokrasia, kupenda au kuchukia kitu. Lakini kupenda au kuchukia huko kuna kuwa na maana kama kutatokana na sababu za msingi. Siasa si mtu japo ni kwa ajili ya watu. Ni vigumu mtu kuchukua nafasi ya taasisi hata awe na umaarufu kiasi gani. 

Tuweke kando sababu 'za muhimu' za kuichukia Chadema. Majuzi zimeibuka mbinu chafu za kukichafua TENA chama hicho. Nasema 'tena' kwa sababu hii si mara ya kwanza. Mengi yashatokea huko nyuma, na makala hii haitoshi kuyaorodhesha yote. Lakini tuhuma kubwa dhidi ya Chadema ni ugaidi. Alipokufa aliyekuwa Makamu wake wa Mwenyekiti Chacha Wangwe, ambaye nae kama Zitto alikuwa na matatizo na viongozi wenzie, chama hicho kilituhumiwa kumuua kwa kisingizio cha ajali. Angalau uzushi huo ungeweza kuaminiwa na mzembe yeyote yule wa kufikiri kwani sote twafahamu kuwa wakati mwingine njia mwafaka ya kudili na adui yako ni kummaliza. Lakini Wangwe alikuwa adui wa nani? Majibi ya haraka yatakuwa 'Mbowe' kama sio 'Slaa.'

Ni hivi, Chadema bado ni chama kichanga kiumri. Na katika jithada zake za kujijenga lazima kitahusishwa na majina ya viongozi wake wachache badala ya chama kizima. Hata CCM na ukongwe wake bado ina majina flani ambayo ni kama chama, watu kama Kingunge au Lowassa. Kwahiyo si jambo la ajabu, baya au hata zuri la Chadema likahusishwa na majina flani ya viongozi wake maarufu. Na kwa namna flani huo ni mtihani ambao Chadema wanalazimika kuushinda: kujenga taswira ya chama badala ya majina ya viongozi wachache.

Kifo cha Wangwe kitaendelea kuiandama Chadema kwa muda mrefu, pengine hadi CCM itakapopoteza nguvu zake, kwa sababu chama hicho tawala kimeishiwa kabisa na mbinu za kupambana na Upinzani isipokuwa kujenga picha ya uadui kati ya Upinzani na wananchi.

Ni hivi, huhitaji kuwa msomi, mjuzi wa siasa au mwenye ubongo 'mkubwa' kama wa Albert Einstein, kutambua kuwa tuhuma za hivi karibuni dhidi ya Chadema zinahusiana moja kwa moja na uhuni unaoendelea huko Dodoma kwa jina la Bunge la Katiba. Ni mkakati fyongo unaolenga sio tu kuifarakanisha Chadema na washirika wenzie huko UKAWA bali pia kuipotezea uhalali wake kwa wananchi.

Hebu kwa minajili tu ya mjadala huu, tupumzishe ubongo na kuamini kuwa kweli Chadema walimuua marehemu Mwangosi. Kwanini suala hili lilifichika hadi muda huu? Mchange (Habib) hakuhama Chadema leo, na amekuwa akiishutumu Chadema tangu aondoke/atimuliwe katika chama hicho. Kipi kilmkwama kooni hadi akashindwa kuituhumu Chadema kwa mauji ya Mwangosi wakati huo? Kwanini iwe sasa?

Laiti tukitumia ubongo wetu ipasavyo tutaweza kirahisi tu kujumlisha moja na moja na kupata mbili: jithada za kuichafua Chadema muda huu hazihusiani na 'uhalifu uliozoeleka katika chama hicho' bali ni suala k
la Katiba mpya. CCM inataka kulazimisha upatikanaji wa Katiba mpya kwa njia za kihuni, lakini imefika mahala na kutambua kuwa japo yaweza kutumia ubabe wake kupitisha Katiba hiyo, lakini inaweza kukosa uhalali. Sasa njia nyepesi ni 'kuwakoroga' UKAWA, wapoteza hadhi yao kwa Watanzania, na hiyo itapelekea umauzi wowote utakaofikiwa na CCM kuonekana ni wa maslahi ya taifa. Nani anataka kuhusiana na mtizamo wa chama cha wauaji?

Kuna tetesi kuwa mwana-Chadema mwingine aliyehusishwa na ajali iliyopelekea kifo cha Wangwe, Deus Mallya, nae yupo katika hatari ya kutumiwa na CCM kutangaza kuwa Chadema ilihusika na kifo cha Wangwe. Jitihada hizi za kuichafua Chadema kwa nguvu nyingi muda huu lazima ziwe na uhusiano na suala la Katiba mpya, na hii haihitaji usomi au kuwa mpenzi wa Chadema.

Ofkoz, CCM wana 'kisingizio cha asili' kinachosubiri muda tu kitumike ipasavyo. Hapa ninazungumzia tihsio la Ebola. Maji yakizidi unga, tutachanganywa akili kuhusu Ebola na kwa vile sie ni wepesi sana kuzugwa, tutasahau kila kitu kuhusu Bunge la Katiba na Katiba mpya. ;Lakini kwa vile Ebola ni ishu nyeti, na ni vigumu kuihusisha na Chadema, mkakati rahisi unaonekana kuwa huu wa kuinajisi Chadema kwa wana-UKAWA wenzie, na kwa upana zaidi, kwa wananchi.

Ninatambua kuna watakaohoji: "sasa Bwana Chahali, kwa vile unaipenda sana Chadema haimaanishi kuwa chama hicho hakiwezi kuwa cha kigaidi." Suala sio mie kuipenda Chadema, na kuipenda sio dhambi, na pia mie si mwanachama au mfuasi wa chama hicho bali ninaunga mkono harakati zake dhidi ya ufisadi. Suala la msingi ni jinsi mbinu za kihuni zinavyotumukia kutuzuwia kupata Katiba mpya 

Ni muhimu kuushughulisha ubongo, na umeumbwa kwa ajili hiyo. Yaani polisi wetu ni dhaifu mno kiasi cha muda wote huu kushindwa kufahamu kuwa miongoni mwao walitumiwa na Chadema kumuua Mwangosi? Kinachochukiza zaidi katika suala hili ni kutumia mauaji ya kinyama ya mwandishi huyo kama mtaji fyongo wa kisiasa. Hadi leo marehemu Mangosi hajatendewa haki, na hata ikitendeka haitmrejeshea uhai wake. Kwanini kumtesa huko alipo kwa kutumia kifo chake kwa minajili ya kisiasa?

Nimalizie makala hii kwa kukumbusha kuwa CCM imefika mahala pa kutumia njia yoyote kuendeleza maslahi yake binafsi. Ipo tayari kwa lolote. Na kimsingi sio suala la CCM kama chama bali maslahi binafsi. Katiba mpya inaonekana kama mkombozi wa walalahoi, chombo kitakachowarejeshea baadhi ya nguvu walizoporwa na wanasiasa. Sasa ni wazi kuwa chama ambacho uhai hake unategemea katika kuwakandamiza walalahoi hao lazima kitafute kila mbinu ya kuhakikisha aidha Katiba halisi-kwa maana ya yenye maslahi kwa mlalahoi haipatikani, au ikipatikana basi iendelee kuwa ya maslahi ya watawala wetu na CCM kwa ujumla.

Pengine kuna maneno niliyotumia katika makala hii ni makali na ya kukera, kwa mfano kuita watu 'wazembe wa kufikiri.' Lengo sio kumdhalilisha mtu yeyote bali kuamsha tafakuri. Ni muhimu tusiruhusu wahuni wa kisiasa kutupelekesha kama maboya. Ni muhimu kujenga na kuimarisha uwezo wa independent thinking, tafakuri inayojitegemea, isiyosukumwa na matukio-halisi au ya kubuni- bali hali halisi.  


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube