2 Aug 2014

Nakumbuka siku moja nilikupokuwa 'rafiki' na ndugu yangu flani huko Twitter (kwa sasa hatupo karibu) aliwahi kunambia, (namnukuu), "Tatizo lako Bwana Chahali ni kuamini kuwa unajua kila kitu, na kudhani siku zote upo sahihi." Maneno haya hujirudia kichwani mwangu mara kwa mara. Japo nilimshukuru kwa maelezo hayo, kiukweli nilibaki na mwaswali mengi tu, moja likiwa "hivi kujua kila kitu (kama inawezekana) ni dhambi?" Na pia "je kuna tatizo kuamini upo sahihi hususan iwapo umefanya jitihada za kuwa sahihi?"

Kuna baadhi ya wenzetu, licha ya kuwa mtandaoni kwa muda mrefu hawajaweza kutambua kuwa ni rahisi sana kuishi maisha ya 'namna flani' mtandaoni. Kwa mfano, ni rahisi kuwa sahihi 'kila wakati' iwapo utakuwa makini katika mada unazozungumzia mtandaoni. Ni vigumu kuwa sahihi katika kila mtihani kwa sababu hata ukijianda vipi bado kuna uwezekano wa mtihani kuja tofauti. Lakini, kwa mfano wa Twitter, kwanini ushindwe kuwa sahihi kila mara ilhali kila unapokutana na jambo flani una muda wa kutosha ku-Google au kurejea notes zako binafsi? Binafsi, nina tabia ya kuto-post kitu chochote kile mtandaoni kabla sijapata uhakika kuwa kipo sahihi kwa asilimia 100. Na kinachonirahisishia ni ukweli kwamba nina muda wa kutosha kufanya hivyo. Mtu akikukuuliza swali kwenye Twitter, kwa mfano, una muda wa kutosha kutafuta facts kwenye Google au Wikipedia, au kurejea uelewa wako binafsi, kabla ya kukurupuka kumjibu.

Anyway, nimeandika hayo kwa sababu makala hii inaweza kuzua maswali kama hayo ya 'rafiki yangu mstaafu' kwamba "ah huyu nae anakuja na 'mbinu za maisha' kana kwamba anayajua sana maisha." No, tunaishi katika dunia ya uchaguzi wa kutaka kufahamu mengi au pungufu au kutofahamu kabisa. Ni suala la uchaguzi tu. Na kamwe sioni aibu kutamka bayana kuwa ninafahamu vitu vingi mno...kwa sababu ninajibidiisha mno kuvifahamu. Background yangu inanisaidia pia: awali nilisoma Sosholojia, baadaye nikahamia kwenye stadi za siasa, na kwa zaidi ya miaka 10 nimekuwa 'nikijisomea binafsi' katika maandalizi ya makala zangu magazetini na katika blogu hii...sambamba na majukumu mengine yaliyonilazimisha kuelewa mengi ya yanayonizunguka.

Twende kwenye mada husika. Hapa chini kuna orodha ya mambo 13 ambayo imethibitika kuwa usipoyadhibiti yanaweza kukwaza mafanikio katika maisha yako. Hebu tuyaangalie moja baada ya jingine.

1.UNAKWEPA MAJUKUMU: Kila jambo uliloshiriki kulifanya likizaa matokeo mabaya unakimbilia kumlaumu flani. Hata 'ukilikoroga' katika maisha yako binafsi, unatafuta wa kumlaumu, aidha mzazi wako, rafiki yako au hata Muumba wako. Kama kweli unataka kufanikiwa maishani mwako ni muhimu kubeba lawama hasa pale ambapo wewe ndio chanzo cha kutofanikiwa kwa suala husika. By the way, uzoefu unathibitisha kuwa lawama hazijengi, na kukwepa majukumu hakusaidii kumfanya mosaji aonekane yupo sahihi.

2. UNASUBIRI MUDA MWAFAKA MILELE: Muda una sifa moja kuu: waweza kuusbiri lakini ukifika hautokwambia 'Chahali, mie ndo muda uliyekuwa ukinisubiri.Sasa nimefika, nitumie ipasavyo.' No. Muda hauna muda huo. Waweza kuusubiri milele na ukifika hautokushtua. Kuna mesmo mmoja wa Kiingereza kwamba njia bora ya kuishi ni kuichukukulia kila sekunde katika maisha yako kama muujiza ambao kamwe hautojirudia. Waweza kusubiri muda milele, na pasipo jithada ya kutumia muda japo kiduchu unaojitokeza, utazeeka huku unasubiri muda mwafaka. Kumbuka ilipokuwa jana ulisema kesho, ambayo ndio leo, na leo ukisema kesho, itapofika itakuwa leo nyingine.

3. KUPANIA KUWA MTIMILIFU: Waingereza wanasema hakuna mtu mtimilifu kwa asilimia 100, yaani nobody is perfect. Haba na haba hujaza kibaba. Kidogo kinachopatikana leo kinaweza kuwa kingi kesho au baadaye. Kweli, inapendeza kuwa mtimilifu (perfect) lakini uzoefu unaonyesha kuwa ni vigumu mno kuwa mtimilifu kabisa kabisa (absolute perfection.). Wewe si malaika, na hata hao malaika pengine wana mapungufu flani.Cha muhimu ni kutambua mapungufu yako na kuyafanyia kazi ili uwe mtu bora zaidi.

. 4. UNAOGOPA KUKOSOLEWA: Ni hivi, hata ukifanya jambo zuri kiasi gani bado kuna wanaoweza kupata upenyo wa kukukosoa. Sasa kama umefanya jambo lisilostahili, kwani usikosolewe? Watu waliofanikiwa zaidi maishani ni pamoja na wale waliochukulia kukosolewa kama fundisho. Hapa simaanishi kuwa hata ukikisolewa kwa chuki ukubali.Ninachomaanisha ni kwamba pindi ukikosolewa waweza pia kupata fursa nzuri ya kutathimini wapi ulikose au kipi ulikosea.

5. UNAOGOPA KUSHINDWA: Maisha ni kama mechi ya mpira wa miguu: kuna kushinda, klushindwa au kutoka sare. Kuna utakavyovipata katika mihangaiko yako ya maisha, lakini pia kuna utakavyovikosa, au utakavyopata nusu na kukosa nusu. Lakini ni muhimu kutambua kuwa kama ilivyo kwenye mpira, huwezi kushinda au kutoka sare bila kuingia dimbani. Wengi wa waliofanikiwa maishani ni waliotambua kuwa kuna kufaulu na kufeli, na walipofeli walikaa chini kujiuliza tatizo liko wapi, na badala ya kuogopa kufeli tena, walitumia walichojifunza ili kupata matokeo bora zaidi. Ukiogpa kufeli hutoweza kujaribu, achilia mbali kufanya .

6. NI MVIVU/MZEMBE: Sheria moja ya maisha inasema 'ukifanya jambo kwa kiwango kilekile cha wanaokuzunguka, basi wewe ni mvivu/mzembe' Tunaishi dunia ya ushindani, na ukitaka uwe bora zaidi ya wengine basi sharti ufanye ziada zaidi ya hao wengine unaotaka kuwa bora zaidi yao. Kama wenzio wanafanya kazi masaa matano, kwanini usifanye masaa sita au hata kumi ikibidi, alimradi watambua kuwa kwa kufanya hivyo utakuwa bora zaidi yao? Kanuni nyingine ya mafanikio ni 'amka mapema,fanya kazi kwa bidii, fanikiwa.'

7. HUNA UHALISI WALA UBUNIFU: Unapaswa kuwa mtu wa kipekee, si kwa mabaya bali mema. Na njia nyepesi ni kutambua kinachowafanya wenzio waonekane bora kisha kufanya maradufu ya wafanyacho. Pia nimuhimu kuwa mbunifu, hata kama itamaanisha kukopi kwa wenzio na kuboresha 'kivyako.' Na njia nyepesi ya kuwa mbunifu ni kusoma wafanyacho wenzako kisha kutafuta namna ya kukiboresha zaidi.

8. KUN'ANG'ANIA KUFANYA MAMBO PEKE YAKO: Ukifanikiwa na 'timu ya ushindi' haimaanishi umefanikiwa kwa upungufu. Angalia wanasoka wa timu kubwa duniani. Mafanikio yao ni mchanganyiko wa jitihada za kipa,mabeki, viungo na washambuliaji, lakini hiyo haipunguzi  mafanikio yao. Kumbuka umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Ili uweze kufanikiwa kwa kiwango kikubwa maishani wahitaji ushirikiano na watu na vitu mbalimbali.

9. HUNA SHUKRANI: Ukosefu wa shukrani waweza kukukwaza kwa kiasi kikubwa kupata mafanikio maishani.Nani anataka kumsaidia mtu asiye na shukrani.Kama nilivyoeleza hapo juu kuwa mafanikio yanahitaji ushirikiano, lakini ni vigumu kumpata mshirika anayefahamu kuwa huna shukrani. Kuwa mwepesi wa kusema asante hata pasipostahili asante. Huna cha kupoteza kwa kushukuru, na kila shukrani unayotoa yaweza kukurejeshea fadhila nyingine lukuki kwa sababu kwa silika yetu binadamu twapenda kuwasaidia wenye shukrani. Na shukrani si tu kwa wanaotutendea mema, wakati mwingine mshukuru hata anayekukosea kwa sababu unampa mtihani wa 'kwanini kanishukuru?' Next time mtu yuleyule alokutenda vibaya aweza kukutenda vyema kwa vile alipokutenda vibaya ulimshukuru, je akikutenda mema shukrani si zitakuwa maradufu?

10.HUTAKI KUJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA: Mara nyingi kikwazo cha kujifunza kutokana na makosa ni aidha kuyachukia makosa hayo pasi dhamira ya kujipanga ili kutoyarudia, au silika ya kupuuza makosa na kukazani akuangalia mafanikio pekee. Uzoefu umeonyesha kuwa wakati mwingine makosa ni mwalimu mzuri, kwani yatuelekeza wapi tulipaswa kufanya hiki lakini tukafanya kile au hatukufanya kitu kabisa. Ili ufanikiwe ni muhimu kuyaangalia makosa kama fursa ya kujirekebisha. 

11.HUJIAMINI: Ni hivi, usipojependa hakuna atakayepoteza muda wake kukupenda. Vivyo hivyo, usipojiamini, hakuna atakayepoteza muda wake kukuamini. Ili uaminike shurti ujiamini mwenyewe kwanza. Kujiamini kwakujengea uwezo wa kusema 'Ninaweza.' Na kutojiamini kwakuleta swali 'Ntawezaje?' Ni muhimu kutambua kuwa ili uweze kujiamini ni sharti la muhimu kujielewa na kutambua uwezo na mapungufu yako. Boresha uwezo wako, jifunze katika makosa yako na kwa watu wengine, tumia maosa kama darasa na jaribu kujiamini. Yes you can!

12. HUNA MSIMAMO: Mshika mawili moja humponyoka, wahenga walituasa. Lakini licha ya kuwa mshika mawili, kuna busara kwamba kuwa na 'lan B' pia kwaweza kukufanya ushindwe kusimama katika jambo moja. Ndio ni vema kujitengenezea mazingira ya 'likishindikana hili ntafanya lile' lakini wakati mwingine ni muhimu kuliangalia jambo lilipo mkononi kama ndio fursa pekee, na hakuna njia mbadala. Ni rahisi kutambulika na hata kukubalika katika jamii iwapo una msimamo, na ni vigumu kupata wafuasi iwapo unayumba kama bendera kufuata upepo.

13.UMEACHA KUKUA: Watu wenye mafanikio hutambua umuhimu wa kuboresha vipaji na/au uwezo wao. Waingereza wanasema 'ukiambiwa upo vizuri basi jibidiishe kuwa vizuri zaidi.' Kama kuna jambo moja linaloweza kusababisha utuame kimaendeleo ni kubweteka. Mifano ni mingi, tuna wasanii, kwa mfano, walofikia hatua kubwa za mafanikio, kisha wakabweteka. Sote twajua hatma yao. Endelea kukua hata kama jamii yakutambua kama ulofikia mafanikio ya hali ya juu. Japo pengine ni sahihi kutaka zaidi na zaidi, lakini wewe ni nani wa kuihukumu kuwa ulichonacho ni zaidi? Na kuwa na zaidi alimradi ni chema kuna ubaya gani?

Natumaini makala hii itakuwa na msaada kwako katika azma yako ya kufikia mafanikio. Usikose kutembelea blogu hii ili kupata mengi yahusianayo na MAISHA, bonyeza hapo kwenye section ya MAISHA kujifunza mengi zaidi.

Makala hii imetafsiriwa kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube