31 Dec 2015

KUTOKANA na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu, wiki mbili zilizopita nilishindwa kuwaletea makala kwenye safu hii. Hata hivyo, kwa bahati nzuri nilichopanga kuandika katika makala hiyo kimechukua sura mpya kati ya wiki iliyopita na muda huu ninapoandika makala hii.
Nilidhamiria kuzungumzia maoni ya wananchi mbalimbali kuhusu uteuzi wa baraza la mawaziri la Rais Dk. John Magufuli. Kimsingi, japo baraza hilo limepokelewa na wengi kama linaloweza kumsaidia Rais kutekeleza kauli-mbiu yake ya ‘Hapa ni Kazi Tu,’ baadhi ya sura zilizomo kwenye baraza hilo zilionekana kama zinazoweza kuwa kikwazo.
Uteuzi ulionekana kuwagusa wengi ulikuwa wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Nikiri kwamba nami nilikuwa miongoni mwa walioshtushwa na uteuzi huo japo tetesi ziliashiria mapema kuhusu uwezekano wa msomi huyo kuwamo katika baraza hilo jipya.
Wakati wengi waliohoji kuhusu Profesa Muhongo kupewa uwaziri walielemea kwenye ukweli kwamba alilazimika kujiuzulu katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow, binafsi nimeendelea kutatizwa na kauli yake ‘ya dharau’ kuwa Watanzania hawana uwezo wa uwekezaji mkubwa, na wanachomudu ni biashara ya juisi tu.

Kwa bahati mbaya au pengine kwa makusudi, Profesa Muhongo hajawahi kuona haja ya kuifuta kauli hiyo au pengine japo kujaribu kuifafanua. Wanaomfahamu, wanadai ni mchapakazi mzuri. Lakini kwa kuzingatia taratibu za ajira kwa hapa Uingereza, miongoni mwa sifa za uchapakazi ni uhusiano mwema na watu (people skills) na uwezo wa kuwasiliana nao kwa ufanisi (communication skills).
Ili uchapakazi ulete ufanisi, ni lazima mtendaji amudu kuelewana na watu wengine, kwa maana ya uhusiano bora unaojali utu na heshima. Kadhalika, ni muhimu kwa mhusika kuweza kuwasiliana nao kwa ufanisi. Sasa, kiongozi anayedharau uwezo wa wenzake, kama hiyo kauli ya Muhongo kuwa uwezo wa Watanzania katika uwekezaji unaishia kwenye kuuza juisi tu, anajiweka katika wakati mgumu katika utendaji kazi wake.
Hata hivyo, kwa bahati nzuri inaelekea Profesa Muhongo ameanza kubadilika. Majuzi, nilikutana na habari inayomhusu na ambayo ilinipa faraja kubwa. Alinukuliwa na vyombo vya habari vya huko nyumbani akihamasisha Watanzania wazawa kujitokeza na kushiriki kuwekeza katika sekta ya umeme.
Kwa tafsiri ya haraka, ni wazi kauli hiyo inaashiria kuwa Profesa Muhongo sasa ana imani na Watanzania, kwamba wanaweza kuwekeza sio kwenye biashara ya juisi pekee bali hata kwenye sekta ya umeme.
Japo hajaomba radhi wala kutolea ufafanuzi kauli hiyo ya awali, kuna umuhimu wa kuangalia suala hilo katika mtizamo wa ‘yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.’
Rai hiyo ya Waziri Muhongo kuwataka wazawa wajitokeze kuwekeza katika sekta ya umeme ni ya kizalendo na inaendana na jitihada zinazofanywa na nchi kama Nigeria na Rwanda ambazo zimekuwa zikihamasisha sana wazawa kujitokeza na kushiriki kwenye uwekezaji katika sekta mbalimbali, badala ya kuliacha suala la uwekezaji kuwa la wageni tu.
Lakini wakati Profesa Muhongo ‘akijisafisha,’ kwa bahati mbaya kuna Waziri mwingine mpya ameanza kuonyesha mkanganyiko katika kauli zake, hali inayoleta wasiwasi iwapo anamudu kuendana na kaulimbiu ya ‘Hapa ni Kazi Tu.’
Mwishoni mwa wiki mbil zilizopita. Vyombo vya habari vya huko nyumbani vilimnukuu Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, akiutaka uongozi wa Jeshi la Polisi kumfikishia taarifa kuhusu tatizo sugu la biashara haramu ya dawa za kulevya. Kauli hiyo ya waziri iliamsha furaha na matumaini kwa Watanzania wengi, hususan katika mitandao ya kijamii.
Cha kushangaza, baada ya hapo, Waziri Kitwanga alinukuliwa akitoa kauli za kuvunja moyo ambapo alidai, namnukuu, “Sina listi ya wauza dawa za kulevya, na orodha hainisaidii zaidi ya kuwa na mfumo mzuri wa kuyadhibiti.” Hivi hizo dawa za kulevya zinajiuza zenyewe au kuna watu wanaohusika kuziingiza au kuzisafirisha? Kama kuna wahusika, iweje waziri adai orodha ya wahusika haimsaidii katika jitihada za kudhibiti biashara hiyo haramu inayogharimu maisha ya vijana wengi wanaoyatumia?
Na kauli yake kwamba hana orodha inaashiria upungufu wake. Anataka orodha ijilete yenyewe ofisini kwake? Angejihangaisha kidogo tu kwenda mtandaoni au kupitia mafaili ya Jeshi la Polisi hususan Kitengo cha Dawa za Kulevya au huko Usalama wa Taifa, angeweza kupata kirahisi orodha hiyo. Binafsi, ilinichukua dakika mbili tu kwenye Google kukutana na orodha kadhaa za wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo.
Waziri Kitwanga aliendelea kudai, namnukuu, “Sijui kama Rais alipewa orodha, hajawahi kuniambia ila kama mna ushahidi mnisaidie nilifanyie kazi.” Japo ni mapema mno kumhukumu, lakini kauli hii haiendani kabisa na kaulimbiu ya Dk. Magufuli ya ‘Hapa ni Kazi Tu.’ Kama Waziri Kitwanga hajui iwapo Rais alipewa orodha hiyo, na kama hajamwambia, kwa nini asimuulize bosi wake iwapo yeye Waziri ana dhamira ya kweli kushughulikia suala hilo?
Halafu kwa vile katika nukuu ya kwanza ametanabaisha kuwa orodha hiyo
(ya wahusika katika biashara ya dawa za kulevya) haimsaidii katika jitihada za kuidhibiti biashara hiyo, sasa anataka wananchi wamsaidieje? Na pengine kinachovunja moyo zaidi ni hilo la kudai ushahidi. Si kazi ya wananchi kutafuta ushahidi kwani kuna watendaji wanaolipwa mishahara kwa ajili ya kazi hiyo. Na hata ingekuwa ni jukumu la wananchi, Waziri Kitwanga si raia wa kigeni, ni mwananchi pia, na kwa maana hiyo wito wake kwa wananchi unamhusu yeye pia.

Moja ya vikwazo vyetu katika matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu ni ukosefu wa nia ya dhati ya kupambana na matatizo husika. Sambamba na hilo ni kukosekana kwa ubunifu. Laiti Waziri Kitwanga angekuwa mbunifu, asingekurupuka kutoa kauli hizo za juzi kwani kimsingi zinahusu majukumu ambayo Watanzania na Rais Dk. Magufuli wanataraji ayatekeleze kwa ufanisi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge jipya, Rais Magufuli alieleza bayana kuwa vita dhidi ya ufisadi, rushwa na dawa za kulevya ni ngumu na hatari kwani inahusisha wakubwa. Na wiki mbili zilizopita, Waziri Kitwanga alinukuliwa akijigamba kwamba hahofii kufa (akimaanisha kuwa hatishwi na nguvu kubwa ya wahusika katika biashara hiyo ya dawa za kulevya). Lakini kauli zake katika siku zilizofuata zinaweza kujenga picha ya mtendaji mwenye hofu ya kukabiliana na tatizo hilo.
Wengi tunaitakia kila jema Serikali ya Rais Magufuli, na makala hii inatekeleza hilo lakini kwa kukosoa upungufu uliojitokeza. Kama kweli tuna nia ya kumsaidia Rais wetu na serikali yake, basi tusiishie kusifia tu bali pia kukosoa pale inapobidi.
Nimalizie makala hii kwa ushauri kwa Waziri Kitwanga, mamlaka zinazohusika na suala la dawa za kulevya na serikali kwa ujumla: ni vigumu kuwakamata wahusika wakuu wa dawa za kulevya kwa urahisi. Wanatumia mbinu nyingi ikiwa ni pamoja na kuficha au kuharibu ushahidi. Moja ya njia zilizoonyesha mafanikio sehemu mbalimbali duniani ni kuwabana wahusika kwa ukwepaji kodi na kile Waingereza wanaita ‘proceeds of crime,’ yaani mali zilizopatikana kutokana na uhalifu. Njia hiyo sio tu husaidia kuwapunguzia wauza dawa za kulevya uwezo wao kifedha, lakini pia huwezesha kubaini utajiri wao ulivyopatikana (na hivyo kuleta uwezekano wa kubaini uhusika wao katika biashara haramu) na pia kuwalipisha fidia kutokana na maovu yao.
Penye nia pana njia, pasipo na nia pana visingizio0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube