
Mwaka 1981, nikiwa darasa la tatu,
marehemu baba aliamua kustaafu kazi, japo alikuwa amebakiwa na miaka kama 10
hivi ya utumishi katika Shirika la Posta. Wakati huo tulikuwa tunaishi Kigoma.
Marehemu baba alikuwa na ndoto za kuwa mkulima mkubwa baada ya kustaafu maana
tulikuwa na hekari kama 50 hivi za mashamba ya mpunga huko Ifakara. Kwahiyo,
aliamini kuwa savings zake na mafao ya kustaafu vingekuwa mtaji wa kutosha
kumwezesha atimize ndoto yake hiyo.
Hata hivyo, wanasema 'kuwa na ndoto ya
kitu flani ni kitu kimoja, kuitimiza ndoto hiyo ni kitu kingine kabisa.' Mwaka
mmoja baada ya kustaafu na familia yetu kurudi kijijini Ifakara, hali ya uchumi
ilikuwa mbaya. Tatizo kubwa lililomkabili marehemu baba ni ukubwa wa ukoo huko
kijijini ambao ulimtegemea yeye kwa msaada. Na wazazi wangu, yaani marehemu
baba na marehemu mama, walikuwa watu wenye huruma mno. Kwahiyo waliona kuwa
hawawezi kuacha kuwasaidia ndugu na ukoo kwa ujumla kwa vile tu wana mipango ya
kilimo kikubwa. Pengine si wazo la busara lakini upendo ni kitu chenye nguvu
mno na kikizidi chaweza kuvuruga kila mpango.
Maisha yangu kama mwanafunzi hapo
Ifakara nilipohamia darasa la tatu hadi nilipomaliza darasa la saba, yalikuwa
magumu mno. Kuna nyakati tulipitisha usiku kwa kunywa uji wa chukuchuku (usio
na sukari wala chumvi), kuna nyakati tulilalia ndizi bukoba za kuchemsha na
kikombe cha maji tu, mlo wa mchana ulikuwa wa kubahatisha, na mara kadhaa
mchana ulipita kwa kunywa maji tu. Pia kuna usiku kadhaa tuliokwenda kulala
bila kutia kitu tumboni.
Nilisoma kwa shida maana hatukuwa na
umeme, japo umeme ulifika Ifakara mapema kabla ya sehemu nyingi za Tanzania kwa
vile mradi wa umeme wa Kidatu ulikuwa jirani na mji huo. Familia iliyokuwa
inahangaika na mlo wa siku moja isingeweza kumudu gharama za umeme ambazo
wakati huo zilikuwa shilingi elfu kadhaa tu. Lakini licha ya kujisomea kwa
kutumia koroboi na mara moja moja taa ya chemli pale tulipoweza kumudu kununua
mafuta ya taa, Mungu alinijaalia nikafaulu kidato cha nne na kupata division
one. Laiti ningefeli, ndio ungekuwa mwisho wa safari yangu kielimu maana
familia isingemudu kunisomesha shule ya private.
Nikachaguliwa kujiunga na high school
Tabora. Namshukuru Mungu kwani shule hiyo ilikuwa ya mchepuo wa kijeshi, maana
niliondoka nyumbani nikiwa na nguo chache tu lakini pale shuleni tulitumia muda
mwingi tukiwa kwenye yunifomu zetu za magwanda. Na hapo shuleni nilikwenda
mikono mitupu, lakini bahati nzuri marafiki walinisaidia hela za matumizi. Na
sikujali sana kwa sababu milishazowea shida.
Bahati ilinijia shuleni hapo
nilipofanikiwa kuchaguliwa kuwa kiranja mkuu. Kwa vile ilikuwa shule ya
kijeshi, 'cheo' changu kilifahamika kama Kamanda Mkuu wa Wanafunzi, kwa kimombo
Students' Chief Commander, au kwa kifupi 'Chief.' Mpaka leo baadhi ya niliosoma
nao huko Tabora wameendelea kuniita 'chifu.' Kupata ukiranja mkuu Tabora Boys'
ilikuwa sio kazi rahisi hata kidogo. Mfumo wa uchaguzi ulihusisha uraia na
ujeshi. Sikuomba kugombea bali nilipendekezwa tu. Na kimsingi haukuwa uchaguzi
as such kwa sababu final say ilikuwa ni ya utawala wa shule na maafande.
Nikabahatika kupata 'wadhifa' huo nikiweka historia ya kuwa 'chifu' mwenye umri
mdogo zaidi katika historia ya shule hiyo (kwa muda huo).
Uchifu ulinisaidia sana kukabiliana na
ugumu wa maisha shuleni hapo kwani licha ya privileges kadhaa zilizoambatana na
'wadhifa' huo, pia nilikuwa nikipewa zawadi mbalimbali na wanafunzi wenzangu.
Ndo raha za uongozi hizo.
Nilihitimu masomo yangu vizuri na kupata
Division Two ya pointi 10. Ninaamini laiti nisingekuwa nakabiliwa na ugumu wa
maisha, ningeweza kupata Division One nyingine.
Kutoka hapo nikaenda JKT Maramba, Tanga,
na hiyo ilimaanisha maisha mengine ya kijeshi kwa mwaka mzima (ukichanganya na
miaka miwili ya ujeshi Tabora Boys'). Lakini bahati ikaendelea kuwa nami kwani
baada ya miezi michache tu nikateuliwa kuwa miongoni mwa vijana waliotakiwa
kujiunga na Jeshi la Wananchi JWTZ kuwa marubani na mainjinia wa jeshi. Kwahiyo
takriban robo tatu ya maisha yangu ya JKT yalikuwa kwenye kambi ya mafunzo ya
RTS Kunduchi. Huko ilukwa ni kula na kulala tu tukisubiri utaratibu wa mchujo
wa urubani na uinjinia wa jeshi. Mwishowe, sikuchaguliwa na nikarudi JKT Ruvu
(kambi ya watoto wa vigogo) kumalizia muda wangu. Hapo napo maisha yalikuwa
mtihani kwa sababu licha ya kambi kujaa watoto wa vigogo lakini pia ilikuwa
karibu na Dar. Nashukuru Mungu nilipata marafiki kutoka familia zenye kujiweza
ambao walinistiri.
Nilipomaliza nikaenda Tanga, na baada ya
muda mfupi nikaajiriwa kuwa mwalimu katika sekondari ya Eckenford. Sikupata nafasi
ya kujiunga na chuo kikuu mwaka huo kwa vile kwa wakati huo, kujiunga na UDSM
ulihitaji Division One ya Form Six, na mie nilikuwa na Division Two ya point 10
(yani kasoro point moja tu kuwa Division One).
Nikafundisha hapo kwa miaka miwili,
kisha nikateuliwa kujiunga na Idara ya Usalama wa Taifa. Jinsi nilivyoteuliwa
ni kama muujiza, lakini ninahisi walikuwa wakinifuatilia tangu nilipokuwa
Tabora Boys' kwa sababu kuna wakati niliwahi kutembelewa na Afisa Usalama wa
Taifa wa Mkoa huo.
Baada ya mwaka mmoja wa mafunzo ya kazi
hiyo, nikaingia mtaani, lakini kwa vile nilikuwa na kiu ya elimu, baada ya
miezi 9 'mtaani' nikachaguliwa kujiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hata hivyo, wakati nikiwa chuoni niliendelea
na kazi pia. Nilipomaliza nikarudi ofisini na takriban mwaka mmoja baadaye
nikapata promosheni iliyodumu hadi nilipoteuliwa kuja kusoma huku Uingereza.
Japo baadaye yalijitokeza matatizo
yaliyopelekea mie kuachana na kazi hiyo, utumishi wangu wa miaka 13 mfululizo
haukuwa na doa, na ninajivunia rekodi yangu. Kilichoniponza ni kukataa umimi.
Tulikuwa tukilipwa vizuri kabisa, kiasi kwamba nilionekana mjinga kuanza
kukosoa maovu mbalimbali yaliyopaswa kukaliwa kimya. Siku zote nilikuwa
nikiwaambia maafisa wenzangu, "tusiwe wabinafsi wa kufikiria hii mishahara
mikubwa na posho tunazopewa ilhali huko mtaani ndugu, jamaa na marafiki zetu
wanataabika. Basi angalau tutimize wajibu wetu na si kuendeshwa na maslahi
binafsi." Pengine 'kimbelembele' ndo kiliniponza. Pengine ni ujinga tu,
kama baadhi ya watu walivyohitimisha. Lakini deep in my heart, naamini
nilifanya kitu sahihi, yaani kusimamia nilichoamini.
Fast forward miaka kadhaa mbele, leo
japo sijafanikiwa kuhitimisha safari yangu ya elimu, kwa maana ya Shahada ya
Uzamifu ambayo imenichukua kitambo sasa (nililazimika kusitisha masomo kutokana
na matatizo niliyokumbana nayo kati yangu na mwajiri/mdhamini wa masomo yangu
yaani taasisi niliyokuwa nafanya kazi.) Panapo majaliwa, mwaka huu, jina langu
litaanza na "Dokta..."
Leo hii namshukuru Mungu, nimefanikiwa
kuendelea kuwatumika Watanzania wenzangu kwa kutumia maandiko yangu, kitu
nilichoanza rasmi mwaka 1998. Lakini pia namshukuru sana Mungu wangu na wazazi
wangu kwa kuniwezesha kupata shahada tatu, na hii ya nne ndio naihangaikia.
Nimepita katika vipindi vigumu mno, kulala na njaa, kusoma kwa koroboi, na
kushindwa kuishi kama vijana wenzangu kwa vile nilitoka familia masikini.
Bahati nzuri, nikiwa hapa Uingereza,
nilivutowa pia na wazo la kufanya kazi za kujitolea (volunteering). Na baadaye
niliajiriwa kwenye taasisi zinazoshughulikia masuala ya wakimbizi. Fursa hizi
zimeniwezesha kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, kutoka Somalia
hadi Iraki, Venezuela hadi China, Zimbabwe hadi Kuwait, Eritrea hadi Sri Lanka.
Nimejifunza mila na utamaduni wa mataifa mbalimbali. Lakini pengine kubwa
zaidi, nimeweza kuwasaidia mamia na pengine maelfu ya watu waliokuja hapa
kusaka ukimbizi. Laiti dua na sala zingekuwa zampatia mtu utajiri hapo kwa
hapo, basi leo hii ningekuwa bilionea maana nimepata nyingi mno kwa kuwasaidia
watu hao ambao wengi walikuja hapa kuokoa maisha yao.
Kwanini nimeandika yote haya? Kwa sababu
licha ya kila shida niliyopata katika masiha ya umasikini niliokulia,
nilijifunza kuhusu utu. Nimejifunza mengi kuhusu wale waliojinyima kwa ajili
yangu, waliogawana nami kidogo walichokuwa nacho, walionishirikisha katika
utajiri wa familia zao, walionijali licha ya kutoka familia masikini. Na pia
nimejifunza kuwa wema hauozi. Mamia kwa maelfu ya wakimbizi niliowasaidia hapa
Uingereza, ninapokutana nao mpaka natamani kujificha kwa jinsi
wanavyonimwagia shukrani, sala na dua. Nimejifunza kuhusu utu.
Leo ninamiliki kampuni japo ndo imeanza
tu mwezi uliopita. Jana nilikutana na mwalimu wangu (mentor) wa masuala ya biashara,
akaniuliza matarajio yangu kwa mwaka huu
2016. Nijamjibu kwa utani "ninataka hadi kufikia mwisho wa mwaka huu niwe
nimetengeneza paundi milioni moja za kwanza kwa kampuni yangu..." kisha
nikacheka. Hakupendezwa na kicheko hicho.Akaniambia "japo unaona kama
mzaha, lakini una kila nyenzo ya kukuwezesha kutimiza hilo. Cha muhimu, amini
katika uwezo wako wa kiakili, upeo wako mkubwa, na historia yako ulivyotoka
kwenye umasikini hadi kufikia hapa." Hawa 'wazungu' hawana tabia ya kumpa
mtu sifa asizostahili. Kama wewe ni 'bomu' watakwambia, kama wewe ni mzuri
watakwambia. Hakuna 'kuzugana.'
Huko nilikotoka na nilikopitia ndo
kwanifanya kuwa mtu niliye leo: namchukulia kila mtu kuwa ana thamani yake.
Siangalii tofauti ya kielimu kama sababu ya kumdharau mtu ambaye hakubahatika
kuelimika sana. Digrii zangu hazina thamani kama sina utu. Kidogo ninachomudu
kukipata hapa (ambacho pengine ni kikubwa sana kwa shilingi yetu huko nyumbani)
hakinifanyi kujiona tofauti na wanaopata pungufu ya changu.
Namshukuru Mungu kwa baraka zake,
nawashaukuru marehemu wazazi wangu kwa kunifundisha kuwa humble (mtu
asiyejikweza) na kuwa mtu wa msaada, nawashukuru wote walioniwezesha kupitia
safari yangu ndefu iliyojaa milima na mabonde, hasa wale walionifundisha kujali
utu badala ya kitu.
Kwa sie Wakristo, tunafundishwa katika Biblia Takatifu kuwa 'wajikwezao watashushwa, na wajishushao watakwezwa.' Naomwomba Mungu aniwezesha kuwa mtu niliye leo hata nikitokea kufanikiwa kimaisha kiasi gani.
Ndoto yangu ya utotoni ni kuwa daktari wa utabibu ili niweze kuwasaidia watu wengi kadri iwezekanavyo. Bahati mbaya sikufanikiwa. Ndoto yangu ya pili ilikuwa kuwa shushushu (kwa hamasa za Willy Gamba), nilifanikiwa kuitimiza, nikalitumikia taifa langu kwa nguvu zangu zote. Bahati mbaya mambo yakaenda 'kushoto.' Ndoto yangu ya sasa ni kutumia elimu, kipaji, ujuzi na uzoefu wangu kuendelea kuwasaidia watu wengine hususan wale wanaoishi katika hali kama niliyokulia.
Ninatumaini msomaji mpendwa waweza
kujifunza kitu kimoja au viwili katika stori hii.
Happy new year!
0 comments:
Post a Comment