25 Mar 2016

HATIMAYE baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, Zanzibar ilifanya marudio ya uchaguzi wake Jumapili iliyopita na Dk. Ally Mohamed Shein kushinda kiti cha urais kwa asilimia takriban 91.

Bila ‘kuuma maneno,’ uchaguzi huo ni mzaha wa kidemokrasia. Ni mzaha kwa sababu ingewezekana kabisa kutofanya marudio ya uchaguzi huo na matokeo ya sasa – yaani CCM kushinda – yakabaki kuwa yale yale.


Yayumkinika kuhitimisha kuwa upande unaoshikilia madaraka visiwani humo umedhamiria kwa dhati kuwa upande pinzani kamwe hautoruhusiwa kutawala, kwa amani au kwa shari.

Kwa lugha nyepesi, ‘piga ua’ chama cha CUF hakitoruhusiwa kutawala Zanzibar hata kama kitashinda uchaguzi kwa asilimia 99. Na tunapozungumzia asilimia ya ushindi, ni vigumu mno kwa sasa kwa chama chochote visiwani humo kupata ushindi mkubwa wa kukipa uhalali wa kutosha kutawala, sababu kuu ikiwa ni mgawanyiko sugu kati ya Waunguja na Wapemba.


Wengi wetu tunachukizwa na kinachoendelea Zanzibar lakini yaelekea hakuna mwenye uwezo wa kushauri nini kifanyike. Nami ninaangukia katika kundi hilo. Sababu za kihistoria zimeendelea kuitesa Zanzibar miaka nenda miaka rudi. Tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, visiwa hivyo vimeendelea kugawanyika kiitikadi kwa misingi ya Upemba (CUF) na Uunguja (CCM).

Japo inaweza kutopendeza kutumia mfano huu, lakini yayumkinika kulinganisha siasa za Zanzibar na mgogoro kati ya Wapalestina na Wayahudi. Kikubwa kinachowaogopesha Waisraeli kukubali amani ya kudumu na Wapalestina ni hofu ya kisasi.

Kwa bahati mbaya, siasa za chuki na ubaguzi visiwani Zanzibar nazo zinajenga mazingira hayo ya hofu, kwamba laiti ‘Wapemba wa CUF’ wakiingia madarakani watalipiza kisasi.

Na hoja hiyo inazidi kuchochewa na ukweli kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu visiwani humo na unaofumbiwa macho na vyombo vya dola, huku kila upande ukitupa lawama kwa wapinzani wake.

Inapotokea waathirika wa siasa za chuki kukamatwa na kudhalilishwa wakiwa rumande, ni wazi watoto na wajukuu zao watabaki na chuki ya muda mrefu, chuki ambayo huko mbele sio tu itazidisha uhasama bali pia yaweza kuzua balaa kubwa.

Tukirejea kwenye uchaguzi huo wa Jumapili iliyopita, nimeeleza hapo awali kuwa ‘mshindi anajulikana’ kabla haya ya kupigwa kura kwa sababu zilizo wazi. Kwanza, CUF kilishatangza msimamo wake kususia uchaguzi huo. Kwa maana hiyo, asilimia kubwa ya waliopiga kura ni wana-CCM, ambao ni dhahiri wamekipigia kura chama chao.


Kwa kuzingatia kanuni ya demokrasia ya wengi wape, ushindi wa CCM utakuwa halali kwa vile wapigakura wengi wamekipigia chama hicho. Lakini wengi hapo haimaanishi Wazanzibari wote kwa ujumla bali wengi kwa maana ya wana-CCM.


Pili, hata kama CUF wasingewakataza wafuasi wao kushiriki uchaguzi huo, ni wazi kuwa CCM ingefanya kila iwezalo – na ina uwezo mkubwa tu – kuhakikisha kuwa CUF haiibuki na ushindi. Hicho, kimsingi, ndicho kilichosababisha kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Hali hiyo haipendezi lakini ndio hali halisi. Ni ukweli mchungu, lakini ukweli una sifa kuu moja: uwe mchungu au mbaya unabaki kuwa ukweli. Ingependeza kuona Wapemba na Waunguja wakiungana kwa maslahi ya Zanzibar lakini hilo si rahisi kwa sasa.


Ugumu wa kuzungumzia siasa za Zanzibar unachangiwa na ukweli kwamba sio rahisi japo kushauri nini kifanyike angalau kupunguza migogoro isiyokwisha ya kisiasa visiwani humo.

CCM wakishindwa, CUF watasusia matokeo. Hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu mpaka zifanyike jitihada mpya za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Kibaya zaidi, mtu pekee anayewezesha uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa ni mgombea wa kudumu wa urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad. Hata jitihada zilizofeli za kutatua mgogoro uliosababisha kurudiwa uchaguzi huo zilitegemea zaidi jitihada za Seif.

Je, hali itakuwaje iwapo Seif akiondoka kwenye ulingo wa siasa? Lakini hata kama ataendelea kuwepo, je, wafuasi wa CUF wataendelea kumvumilia milele kila atakapojaribu kutafuta mwafaka kwa kukubali serikali ya umoja wa kitaifa? Hatari inayomkabili Seif kwa kuwa msuluhishi wa kudumu ni uwezekano wa yeye kuonekana msaliti miongoni mwa wafuasi wa chama chake.

Lakini ukweli kwamba Seif ni miongoni mwa viongozi wa zamani wa kitaifa, na hivyo kuwa mnufaika wa stahili mbalimbali kutoka serikalini unaweza kumkwaza kuelemea zaidi maslahi upande wa chama chake. Tumeshuhudia majuzi jinsi serikali ilivyogharimia matibabu yake. Sasa busara kidogo tu zapaswa kutukumbusha kuwa ni vigumu kwa mtu kukata mkono unaomlisha.

Baadhi yetu tunadhani hakukuwa na haja ya kupoteza fedha sio tu kurudia uchaguzi huo bali hata kufanya uchaguzi mwezi Oktoba mwaka jana kwa sababu imekwishakuwa kama kanuni ya siasa za Zanzibar kuwa lazima mshindi wa urais atoke CCM.


Sasa kuna haja gani ya kupoteza fedha kwa ajili ya mchakato ambao hautabadili chochote? Sawa, demokrasia ina gharama zake lakini gharama nyingine zinaepukika.

Nihitimishe makala hii kwa kubashiri kwamba jitihada zikifanyika, Zanzibar itapata tena serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo, mwaka 2020 visiwa hivyo vitajikuta kwenye hali tata kama iliyojiri katika kila chaguzi katika mfumo wa vyama vingi.


Ningetamani sana kuhitimisha makala hii na ushauri wa nini cha kufanya lakini ninatambua bayana kuwa njia pekee (na isiyofaa) ni CUF kuendelea kuvumilia ubabe wa CCM katika kila uchaguzi, na kukubali kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa (ikiundwa). Lakini njia hiyo (ukitoa serikali ya umoja wa kitaifa) ndio sababu kuu ya mgogoro huo wa kudumu wa kisiasa huko Zanzibar. Na kama tunavyofahamu sote, tatizo haliwezi kutatuliwa na tatizo jingine.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube