21 Apr 2016


MAJUZI nilibandika habari mbili kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook zilizohusu ufisadi na umasikini. Habari moja ilihusu taarifa za vyombo vya habari kwamba wabunge wameshtushwa na ripoti inayoonyesha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetumia shilingi bilioni 18 kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha.

Niliambatanisha habari hiyo na nyingine iliyoonyesha ‘shule ya kipekee’ ambayo madarasa matatu yanalazimika kutumia jengo moja, kitu ambacho kinaweza kuiingiza shule hiyo katika rekodi ya miujiza ya Guinness.

Lengo lilikuwa kuonyesha kuwa wakati TCRA ikitumia mabilioni hayo kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha, kuna wanafunzi wanaosoma katika mazingira magumu kwa kulazimika ‘kuchangia’ jengo la darasa.

Watumiaji wengi wa mtandao huo wa kijamii waliguswa na habari hiyo, lakini kilijitokeza kikundi kidogo kilichoitetea TCRA kwa nguvu zote. Hoja yao kuu ni kuwa majukumu ya taasisi hayo ni muhimu na teknolojia inabadilika kwa kasi, kwa hiyo ni sahihi kutumia fedha nyingi kuiwezesha taasisi hiyo kwenda na wakati.

Kilichonisikitisha zaidi ni pale wanahabari wawili wakongwe (mmoja wa gazeti hili) ‘walipomvuta’ kiongozi mmoja wa TCRA, sio kwa minajili ya kumbana kuhusu taarifa hiyo bali kuvilaumu vyombo vya habari vilivyoripoti habari hiyo, sambamba na kutetea matumizi hayo ya mabilioni kwa mafunzo, semina na warsha.

Nilikerwa mno na utetezi wa wanahabari hao kwa sababu laiti wangerejea ripoti za nyuma kuhusu matumizi ya taasisi hiyo wangetambua tukio hilo sio la mara ya kwanza. Mwaka 2011, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilikagua hesabu za TCRA na kugundua madudu ya kutisha, ikiwa ni pamoja na mamlaka hiyo kusomesha nje wafanyakazi wake watatu kwa gharama ya shilingi bilioni 2.2

Na hata kama TCRA ingekuwa haijawahi kuingia matatizoni kutokana na matumizi hayo makubwa ya fedha za umma, bado isingehalalisha taasisi hiyo kutumia shilingi bilioni 18 kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha. Sio kwa Tanzania yetu hii ambayo ni moja ya nchi masikini kabisa duniani.

Lakini kingine kilichonikera kuhusu matumizi hayo ya ‘anasa’ ya TCRA ni ukweli kwamba mamlaka hiyo kwa kiwango kikubwa imekuwa butu hususan katika eneo la udhibiti dhidi ya makosa ya mtandaoni. Taasisi hiyo ilikuwa mstari wa mbele kutetea muswada wa sheria ya makosa ya mtandao (Cybercrime Bill 2015) hadi ilipopitishwa kuwa sheria kamili.

Binafsi niliunga mkono muswada huo na hatimaye sheria husika kwa sababu, kwa upande mmoja, nilikwishawahi kuwa mhanga wa unyanyasaji mtandaoni, na kwa upande mwingine, nilikuwa nikikerwa mno na matumizi mabaya ya uhuru mtandaoni yaliyojumuisha matusi, picha za utupu na vitendo vingine visivyofaa, hususan katika mtandao wa kijamii wa Instagram.

Sasa, tangu sheria hiyo dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ipitishwe imeishia kuungana na lundo la sheria nyingine kali lakini zisizo na ufanisi wowote. Ni kweli kwamba hoja za waliokuwa wakiipinga sheria hiyo zilikuwa na mantiki, hususan hofu kuwa itatumika vibaya, hususan uwezekano wa kutumika kisiasa zaidi kuliko kisheria.

Inatusikitisha baadhi yetu tuliotumia nguvu kubwa kuunadi muswada wa sheria hiyo ambao ulipata upinzani mkali kutoka kila kona ya Tanzania, lakini hatimaye ulifanikiwa na kuwa sheria kamili.

Majuzi, sheria hiyo imeonekana kufanya kazi ‘ghafla.’ Kijana mmoja amekamatwa na kufikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali kabisa, kwa kosa la kumtukana Rais John Magufuli.

Hakuna Mtanzania mwenye akili timamu anayeweza kuunga mkono kuwatusi viongozi wetu, awe Rais au mwenyekiti wa kijiji. Tatizo ni kwamba sheria hiyo dhidi ya uhalifu mtandaoni inaonekana kuwa na meno pale tu ‘wakubwa’ wanapoguswa.

Kwa yeyote anayetaka kuthibitisha jinsi gani sheria hiyo ‘ina upendeleo’ atembelee mtandao wa kijamii unaohusu picha, yaani Instagram, ambapo huko kuna kila aina ya laana: kuna ushoga wa waziwazi, kuna lundo la akaunti zinazobandika picha za utupu, kuna ‘ligi kuu’ ya matusi ambapo kadri watu wanavyoonyesha umahiri wa matusi ndivyo kadri wanavyopata wafuasi wengi.

Hali huko Instagram ni mbaya mno kiasi kwamba ni rahisi kudhani kuwa wanaofanya ‘madudu’ huko wapo katika nchi isiyo na sheria (lawless country). Kwa vile ‘wakongwe’ wa matusi wameendelea kupata umaarufu kwa kutukana pasipo kuchukuliwa hatua zozote, mtandao huo umewavutia hata watu ‘wasio na matusi’ kujaribu fursa ya kujipatia umaarufu wa bure.

Na umaarufu huo una ‘faida’ kwani akaunti zinazosheheni matusi pia hufanya matangazo ya biashara mbalimbali, kuanzia ‘video za ngono’ hadi tiba za ajabu ajabu.

Wakati fulani niliwajulisha watu wa TCRA kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, lakini ‘bosi’ wa mamlaka hiyo aliishia kutoa ‘darasa’ refu lisilo na maana akidai kuwa ni muhimu Watanzania watambue sheria zilizoianzisha Mamlaka hiyo na shughuli zake kwa ujumla. Alidai kuwa jukumu la udhibiti wa matusi na uchafu mwingine huko Instagram ni la polisi. Kichekesho ni kwamba kesi ya huyo jamaa aliyemtukana Rais inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya polisi na TCRA.

Kwa hiyo si kwamba TCRA haina mamlaka ya kupambana na ‘laana’ inayoendelea huko Instagram, lakini kinachoonekana ni kwamba haina muda na adha zinazowakumba wananchi wa kawaida. Uvunjifu huo wa sheria ukimgusa kiongozi, basi mamlaka hiyo na sheria dhidi ya uhalifu wa mtandaoni vinafufuka ghafla. Hii sio sawa hata kidogo.

Nimalizie makala hii kwa kuisihi serikali ifanye jitihada za makusudi kukomesha hali mbaya inayoendelea katika mtandao huo wa kijamii. Haihitajiki kukamata kila mhusika lakini vinara wachache tu wakitiwa nguvuni itasaidia kufikisha ujumbe kwa wenzao.

Suala hili linaweza kuihusu wizara yenye dhamana na masuala ya afya pia, kwa sababu mtandao huo umegeuka kuwa duka lisilo rasmi la dawa za aina mbalimbali, suala ambalo linaziweka afya za Watanzania shakani.

Penye nia pana njia, pasipo na nia pana kisingizio. 

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.