8 Jul 2016

Ilikuwa masaa, siku, wiki, miezi na sasa mwaka. Ni vigumu sana kuamini kuwa baba umeondoka moja kwa moja. Kila siku nakumbuka, lakini kuna kitu kingine kinachonikumbusha kila wiki: makala zangu katika gazeti la Raia Mwema. Ulikuwa 'shabiki nambari wani' wa safu yangu katika gazeti hilo, na ulihakikisha unasoma kila toleo la gazeti hilo.

Pamoja na mengi uliyotuachia wanao, moja ninalofanya kila siku ni kusoma na kuandika, vitu viwili ulivyonisisitiza mno tangu nikiwa mtoto mdogo. Na kwa hakika kama ulivyopenda sana kusoma na kuandika, ndivyo ambavyo kwangu vitu hivyo vimekuwa sehemu muhimu ya maisha yangu ya kila siku.

Pia wewe na marehemu mama mlinisisitza mno kuhusu umuhimu wa elimu.Nawashukuru sana mlivyojinyima ili kuhakikisha ninatimiza ndoto zangu za kielimu. Ninasikitika kwamba wakati wewe na mama mlikuwa na kiu sana ya kuniona nahitimu shahada ya uzamifu (PhD), kwa bahati mbaya nyote mmeondoka kabla sijahitimu. Hata hivyo, nime-dedicate thesis yangu kwenye.

Nakushukuru pia wewe na marehemu mama kwa kutuhimiza mno watoto wenu kuhusu upendo, kuthamini utu na kubwa zaidi, kumtanguliza Mungu katika kila tufanyalo. Upendo wako baba ulikufilisi mapema mara baada ya kustaafu mwaka 1981, ambapo mipango yako ya kuwekeza katika kilimo ilizidiwa nguvu na moyo wako wa kuwasaidia ndugu na jamaa pale Ifakara. 

Miaka kadhaa baadae, marupurupu yako ya utumishi wako katika Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo yaliishia kwenye kuwasaidia ndugu, jamaa na marafiki. Siku zote ulikuwa unasisitiza kuwa utu ni muhimu ziadi kuliko vitu (including pesa). 

Iliniuma mno kushindwa kuja kukuaga katika safari yako ya mwisho. Lakni nakumbuka sana maeneo yako kuwa "lolote likinitokea, hakikisha kwanza usalama wako..." Wewe baba na marehemu mama siku zote mlikuwa mnahofia kuhusu kazi niliyokuwa naifanya lakini kwa vile mlinipenda mno, mlikuwa mkiniombea kila siku ya Mungu.

Kama kuna kitu kinaniumiza mno ni mapacha Kulwa (Peter) na Doto (Paul). Kwa vile wao walizaliwa wakati umri umeshawapita mkono nyie wazazi wetu, mapacha hawa walikuwa kama wajukuu zenu. Lakini kubwa zaidi, walikuwa ndio marafiki zenu wakubwa. Kila ninapoongea nao najiskia uchungu sana kwa sababu sio tu wamepoteza wazazi lakini pia wapoteza their best friends. Ninaendelea kuwasapoti ili wasielemewe na huu uyatima tulionao.

Kama kuna kitu kimoja nilikuangusha mno ni kutofuata matakwa yako nijiunge na seminari ya Kasita baada ya kuwa mmoja wa wavulana wanne tu waliochaguliwa kujiunga na seminari hiyo. Ulitamani sana niwe padri. Hata hivyo, japo nilikuangusha, angalau mdogo wangu, Sista Maria Solana aliweza kujiunga na utawa, na yeye sasa ndio guide wetu mkuu katika sala.

Pamoja na uchungu nilionao kutokana na kifo chako baba, faraja pekee ni kuwa ninaamini muda huu upo na mkeo mpendwa, mama yetu mpendwa, marehemu Adelina Mapango a.k.a Mama Chahali. Tangu mama afariki, baba ulikuwa ukisononeka mno, kwa vile mama hakuwa mkeo tu bali pia rafiki yako mkuu. Siku zote baada ya kifo cha mama ulijisikia kuwa wewe ndo ulistahili kutangulia kabla yake kwa vile ulikuwa umemzidi umri.

Kipimo cha upendo wako baba ni kipindi kile mama alipopoteza fahamu kuanzia mwishoni mwa Januari 2008 hadi alipofariki Mei 29, 2008. Baba ulikuwa unafunga mfululizo kumwombea mama apate nafuu.Nakumbuka nilipokuja kumuuguza mama tulikushauri upunguze kufunga mfululizo hasa pale sauti yako ilipoanza kukauka na nguvu kupotea kutokana na mwili kukosa lisha na maji. Ulimpenda mno mkeo, na kwa hakika mmetachia fundisho kubwa sana.

Mwaka 2005 niliwarekodi wewe na mama, katika maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa yenu. Bado ninayo video ile lakini nashindwa kuiangalia kwa sababu inanitia uchungu sana. Hata hivyo, kila siku ninazingatia yote mliyoniusia katika video hiyo, na ndio mwongozo wa maisha yangu.

Basi baba, nakuombea uendelee kupumzuka kwa amani na marehemu mama na mwanga wa milele uangaziwe na Bwana. Mie ninawakumbuka kwa sala kila siku kabla ya kulala. Sie tulikupenda wewe baba na mama, lakini Baba yenu wa Mbunguni aliwapenda zaidi, akawachukua. Jina lake lihimidiwe milele. AMINA0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.